Serikali yafuta hati za viwanja mitaa ya Ndachi, Muungano

kuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge

Muktasari:

Rais John Magufuli aliivunja CDA iliyodumu miaka 33 mwaka jana na kukabidhi shughuli za mamlaka hiyo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Dodoma. Serikali imefuta hati za viwanja ambavyo muda wake wa umiliki katika mitaa ya Ndachi na Muungano umeisha na kuingiza katika mali za Jiji la Dodoma ikiwa ni hatua ya kutatua mgogoro wa ardhi wa eneo hilo ulioachwa kiporo na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA).

Rais John Magufuli aliivunja CDA iliyodumu miaka 33 mwaka jana na kukabidhi shughuli za mamlaka hiyo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Akitoa maagizo ya Serikali yaliyotokana na mapendekezo ya kamati iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema pia wananchi ambao wamejenga bila kibali cha jiji na kufanya maendelezo tofauti na mpango uliokusudiwa wahakikiwe ili wafikiriwe kuingizwa katika mpango mji unaoandaliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alimuomba waziri mwenye dhamana (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi) kuangalia upya mabaraza ya ardhi ili yaweze kwenda katika maeneo husika ya ardhi yanayolalamikiwa kabla ya kutoa uamuzi.