Serikali yataifisha ng’ombe 114 walioingia Pori la Kigosi

Muktasari:

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Chiganga Mashauri baada ya kuwatia hatiani washtakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbili tofauti zenye makosa yanayofanana.

Watuhumiwa watano wamelipa faini ya Sh400, 000 kila mmoja na kukwepa kifungo cha mwaka mmoja jela

Tabora. Serikali imetaifisha ng’ombe 114 kati ya 320 kwa idhini ya Mahakama waliokamatwa ndani ya Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi huku wamiliki wake watano wakihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh400,000 kila mmoja.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Chiganga Mashauri baada ya kuwatia hatiani washtakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbili tofauti zenye makosa yanayofanana.

Watuhumiwa waliotiwa hatiani ni Bahati Yusuph, Robert Kitapondya, Amos Masha waliokutwa na ng’ombe 100 ndani ya pori na wengine ni Mashine Mwandu na Issack Mashine waliokuwa na ng’ombe 14.

Watuhumiwa wote watano wamelipa faini ya Sh400,000 kila mmoja na kukwepa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuingia na kuchungia mifugo ndani ya hifadhi ya Taifa.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali Idd Mgeni, ulidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo Septemba 6 mwaka huu baada ya kuingia ndani ya pori la akiba bila kibali.

Wakili Mgeni alidai kuwa katika shtaka la pili, washtakiwa watatu walikutwa wakichunga ng’ombe 100 na wawili walichungia ng’ombe 14 bila kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

Wakati huohuo; ng’ombe wengine 206 waliokutwa ndani ya hifadhi hiyo ambao mwenyewe hajulikani alipo na bado wanashikiliwa hadi kibali kitakapotolewa na Mahakama ili wapigwe mnada kufidia uharibifu waliofanya katika pori hilo la akiba.