Shaffih Dauda, Maua Sama, Soudy Brown wengine watano wasota rumande

Muktasari:

  • Maua Sama, meneja wake Fadhili Kondo na mtangazaji wa Clouds Soud Brown wanashikiliwa wakituhumiwa kufanya makosa ya kuharibu mali baada ya kurusha video katika mtandao wa Instagram inayowaonyesha mashabiki wa mwanamuziki huyo wakirusha noti na kuzikanyaga.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Maua Sama, watangazaji wa Clouds Shaffih Dauda, Soud Brown, msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, mshereheshaji Antony Luvanda na watu wengine watatu wameendelea kusota rumande kwa zaidi ya saa 72 katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam wakituhumiwa kufanya makosa ya mtandao.

Maua Sama, meneja wake Fadhili Kondo na mtangazaji wa Clouds Soud Brown wanashikiliwa wakituhumiwa kufanya makosa ya kuharibu mali baada ya kurusha video katika mtandao wa Instagram inayowaonyesha mashabiki wa mwanamuziki huyo wakirusha noti na kuzikanyaga.

Luvanda maarufu Mc Luvanda, Shaffih Dauda na wengine wanne wanashikiliwa kwa makosa ya kuendesha mitandao ya kijamii bila kusajili.

Wengine wanaoshikiliwa ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene kwa uchunguzi ili kujua uhalali na maudhui ya blog anayodaiwa kuiendesha.

Akizungumza kukamatwa kwa Maua Sama, Msemaji wa Nyumba ya Vipaji (THT), Rehema Jones alisema mpaka jana, msanii huyo pamoja na Soud na Kondo walikuwa rumande ikiwa ni siku ya tatu tangu wakamatwe.

Alipoulizwa kuhusu maendeleo yao na iwapo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani alisema, “Sisi tunasubiri maelekezo tu kwa kuwa suala hilo lipo katika vyombo vinavyohusika. Tunasubiri kuona nini kitaendelea kwa sasa hatuna zaidi cha kuzungumza.”

Jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema bado wanashikiliwa na kwamba jeshi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA) watahakikisha wote wanaofanya makosa ya mtandao wanakamatwa.

“Nitatoa taarifa zaidi kuhusu watuhumiwa hao, lakini jua operesheni ndio imeanza na haitakuwa na mwisho. Tutahakikisha wote wanaofanya makosa tunawakamata hadi waishe,” alisema Mambosasa.

Kuhusu idadi ya waliokamatwa alisema hadi kufikia jana, watu wanane walikuwa wameshakamatwa na kwamba wataendelea kuongezeka kwa kuwa kazi ni endelevu.

“Hadi kufikia asubuhi tulikuwa tumeshakamata watu wanane na kwa mchana huu sijapokea taarifa lakini wanaweza kuwa wameongezeka,” alisema.

Kuhusu majina ya waliokamatwa Mambosasa alisema: “Siwezi kuyataja kwa kuwa nitaita waandishi wa habari ili kuzungumza nao.

Juzi, akizungumza na Mwananchi, Mambosasa alisema wanamshikilia mwanamuziki Maua Sama na mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, Soudy Brown kwa kosa la uharibifu wa mali.

Alisema wanawashikilia baada ya kuona wakiwa wamerusha picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wakiwa baa wakirusha fedha juu na kisha kuzikanyagakanyaga.

Akitoa taarifa juzi, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa Makene alipokea wito kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu (ZCO) na baada ya mahojiano aliendelea kushikiliwa kwa mahojiano.