Shule saba zafunguliwa

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Muktasari:

  • Hatua ya Mongella ilitokana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kufunga shule hizo kinyume cha sheria, kwani mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni mkurugenzi wa elimu ambaye hushauriana na mkuu wa mkoa husika.

Mwanza. Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe limesababisha shule saba kati ya 11 zilizofungwa kwa kukosa vyoo kufunguliwa jana.

Hatua ya Mongella ilitokana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kufunga shule hizo kinyume cha sheria, kwani mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni mkurugenzi wa elimu ambaye hushauriana na mkuu wa mkoa husika.

Taarifa ya kufungwa kwa shule hizo zilibainika wakati wa kikao cha Kamati ya Bodi ya Barabara Mkoa Machi 9.

 Shule zilizofungwa ni Muhza, Murutanga, Bukindo, Busangu, Mugu, Buzegwe, Kilongo, Murutunguru, Mubele na Chakamba zote za msingi. Katika orodha hiyo pia ipo Sekondari ya Lugongo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Myamaha alisema jana kuwa kufunguliwa kwa shule hizo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita.