‘TTCL kukusanyeni madeni’

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kusimamia ukusanyaji wa madeni wanayodai ili kuleta ufanisi wa shirika hilo.

Profesa Mbarawa alisema jana kuwa kasi ya ukusanyaji wa madeni ya shirika hilo bado ni ya kusuasua.

Alisema hayo jana ikiwa ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa sheria mpya ya TTCL inayoibadilisha kampuni hiyo kuwa shirika.

Hatua hiyo inafuata mabadiliko ya sheria namba 12 iliyopitishwa mwaka 2017 na kusainiwa na Rais John Magufuli Novemba 28,2017.

“Achaneni na utaratibu wa zamani, maofisa walikuwa wanakwenda kudai madeni lakini wanaishia kupewa rushwa badala ya kukusanya madeni,” alisema Mbarawa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema shirika hilo lilikuwa linadai Sh10.9 bilioni, limekusanya Sh6.8 bilioni na zimebaki zaidi ya Sh3 bilioni.

Mwenyekiti wa bodi ya iliyokuwa kampuni ya TTCL, Omar Nundu aliishauri bodi mpya itakayoteuliwa, kulisimamia shirika badala ya kusubiri maelekezo kutoka serikalini.