‘Tafuteni njia rafiki ukusanyaji kodi’

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango 

Muktasari:

Waziri Mpango aliyasema hayo jana wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mawaziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara mjini Dodoma.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutafuta njia rafiki za kukusanya kodi kutoka kwa wadau wa sekta binafsi.

Waziri Mpango aliyasema hayo jana wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mawaziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara mjini Dodoma.

“Haiwezekani kukusanya kodi kwa watu wetu kama vile tupo kwenye misitu ya Congo, kila siku ni kukimbizana tu?.” Alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alisema anatambua kuwa sekta binafsi ni ‘injini’ ya uchumi, hivyo wizara yake haipo tayari kuona sekta hiyo inarudi nyuma.

Aliwataka wadau wa sekta binafsi kupiga vita rushwa zinazolalamikiwa kuombwa na watumishi wa taasisi za Serikali ili kuweka mazingira mazuri ya kukuza sekta hiyo kwa maendeleo ya nchi.

Akisoma hotuba ya wadau, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Salumu Shamte alisema kero kubwa inayowakumba ni utitiri wa taasisi za Serikali kuwaandama wafanyabiashara au wenye viwanda.

Shamte alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi(Osha) Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Chakula na Dawa,(TFDA)

“Ndani ya wiki moja, taasisi zaidi ya nane za Serikali zitakutembelea na mwisho wa siku, ni kukudai fedha, viwanda vingi vimefungwa kwa sababu ya kero zinazotokana na taasisi hizo,” alisema.

Hata hivyo, Shamte aliishukuru Serikali kwa kutoa fursa ya majadiliano kati yake na wadau wa sekta binafsi.

Shamte aliiomba Serikali kusikiliza kero za sekta hiyo ili kuifikia Tanzania ya viwanda tuitakayo.

Katika kujibu hoja mbalimbali za wadau hao, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alisema Serikali inayafahamu matatizo yanayoikabili sekta hiyo na kuna mipango ya kuyatatua.

“Rais (John Magufuli) hajaja na jipya, kilichopo kipya ni kasi ya kuondoa kauli za njoo kesho katika ofisi za umma na urasimu mwingine unaowachelewesha wafashabiasha kupata huduma kwa wakati,” alisema Waziri Mwijage.

Alisema Serikali iliamua kuanza na hilo huku akiwahakikishia kufanya kazi nao bega kwa bega kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarika.