Takukuru yampandisha kizimbani Ofisa Afya

Muktasari:

  • Mshtakiwa alifikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni leo mbele ya Hakimu Frank Moshi na kufunguliwa mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu namba 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Dar es Salaam. Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, Mkoa wa Kinondoni imemfikisha Mahakamani Ofisa Afya wa kata ya Mbweni,Manispaa ya Kinondoni Amos Ndalawa (26) kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.

Mshtakiwa alifikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni leo mbele ya Hakimu Frank Moshi na kufunguliwa mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu namba 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Veronika Ndeoya aliieleza Mahakama kuwa Mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Kinondoni kama Ofisa Afya wa Kata ya Mbweni Mnamo Machi 21 mwaka huu alishawishi na kupokea rushwa ya Sh300, 000 toka kwa Leticia Lubala ili asimchukulie hatua za kisheria baada ya kumkagua kwenye biashara yake.

Mshtakiwa alikana mashtaka yote mawili na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alitakiwa kuweka saini ya shilingi500, 000 na kesi kutajwa tena Aprili 10.