Tanga Cement yaikumbusha Serikali kuhusu gesi ya Mtwara

Muktasari:

Meneja udhibiti mitambo wa kiwanda hicho, Pamphil Mumwi alisema jana kuwa iwapo nishati ya gesi itafikishwa Tanga, itakiwezesha kiwanda kuacha kutumia makaa ya mawe, hivyo kuwapo uwezekano wa mfuko mmoja wa saruji kuuzwa kwa Sh9,000 badala ya Sh13,000.

Tanga. Kiwanda cha Tanga Cement kimeiomba Serikali kuharakisha mipango yake ya kufikisha nishati ya gesi mjini hapa kutoka Mtwara ili gharama za uzalishaji ziweze kupungua.

Meneja udhibiti mitambo wa kiwanda hicho, Pamphil Mumwi alisema jana kuwa iwapo nishati ya gesi itafikishwa Tanga, itakiwezesha kiwanda kuacha kutumia makaa ya mawe, hivyo kuwapo uwezekano wa mfuko mmoja wa saruji kuuzwa kwa Sh9,000 badala ya Sh13,000.

Mumwi alisema nishati ya gesi itakiokoa kiwanda hicho kuondokana na gharama za kununua na kusafirisha makaa ya mawe kutoka Liganga mkoani Songea au Afrika Kusini.

“Kila siku lazima tutumie kuanzia tani 400 hadi 500 za makaa ya mawe, lori moja linabeba tani 30 ina maana lazima kila siku yasafiri malori zaidi ya 16 ya makaa ya mawe kutoka Liganga au Afrika Kusini,” alisema Mumwi.

Meneja huyo alisema nishati ya gesi ikipatikana kiwandani hapo itakuwa mbadala wa makaa ya mawe kiwandani hapo.

Kuhusu umeme alisema mitambo iliyopo kiwandani hapo ni megawati 30 kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Alisema umeme huo hautakuwa na mbadala hata kama gesi kutoka Mtwara itafikishwa kiwandani hapo.

“Ifahamike kwamba umeme wa Tanesco hauna mbadala tunachosisitiza kila mara ni kuepuka kutukatia kwa sababu mitambo yetu ikizimika ghafla ni hasara kubwa kutokana na mzunguko mitambo ya saruji ambayo ikiwashwa haihitaji kuzimwa,”alisema Mumwi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Monica Kinala aliwataka wahandisi kuondoa hofu kuhusu nishati ya gesi kutoka Mtwara kwa sababu Serikali ipo katika mikakati ya kuhakikisha inasambaza gesi mikoa mbalimbali.

“Niwaondoe wasiwasi, Tanga Cement pamoja na wawekezaji wengine waliopo na wanaotarajia kuja kuwekeza ni kwamba, Serikali inaweka mikakati itakayohakikisha nishati inatosheleza kuendesha viwanda,” alisema Monica.