Tasnia ya filamu iliumwa goti ikapasuliwa kichwa

Muktasari:

Hatua hiyo ilikuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu hali duni za wasanii na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuamua kuchukua hatua kwa kuziita Ikulu taasisi zote zinazohusika kwa namna moja ama nyingine na wasanii.

Urasimishaji ni neno lililokuwa maarufu sana katika tasnia ya filamu kipindi cha miaka ya 2012/13. Neno hili lilitokana na hatua ya Serikali kuanzisha sheria mpya ya ushuru inayotaka kazi za filamu na muziki zibandikwe stempu za TRA.

Hatua hiyo ilikuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu hali duni za wasanii na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuamua kuchukua hatua kwa kuziita Ikulu taasisi zote zinazohusika kwa namna moja ama nyingine na wasanii.

Kwa mujibu wa mmojawapo wa maofisa walioshiriki, Rodgers Fovo wa TRA mbali na wao TRA, taasisi za Basata, Cosota, Bodi ya Filamu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hata polisi walishiriki.

Kwenye wito huo, Rais aliwaagiza waangalie namna watakavyoweza kuisaidia tasnia za filamu na muziki. Kuna mengi yanaongelewa lakini kimsingi watendaji wa taasisi hizo sijui ilikuwaje baada ya agizo hilo mpaka wakaja kuibuka na mpango wa urasimishaji kwa namna ulivyo, tena bila hata kufanya utafiti wa kutosha pamoja na mara kadhaa Rais mstaafu, Kikwete kutamka hadharani kuwa Serikali iliwezesha suala la utafiti.

Awali, Serikali kupitia watendaji hao walioaminiwa na Rais iliinadi hatua hiyo kama muhimu kudhibiti wizi wa kazi za wasanii kutokana na kilichoitwa kilio cha wasanii dhidi ya uharamia wa kazi zao, japo wadau wengi wenye ufahamu wa kutosha katika tasnia ya filamu waliupinga mpango huo mara tu baada ya kutangazwa kwa kuwa haukuwa na dalili ya kutatua matatizo ya msingi ya tasnia ya filamu. Na sasa ni zaidi ya miaka mitano na mpango huo unaonekana dhahiri kuwa umefeli.

Tuanze kwa kujiuliza swali, wasanii wa filamu walikuwa na kazi ambazo zinaibwa? Wakati ikianzishwa sheria hiyo ya ushuru wa stempu katika tasnia ya filamu kazi zote zilizokuwa zikiingia madukani zilikuwa zinamilikiwa na wasambazaji ambao wanafahamika. Kwa nini Serikali ilidhani inasaidia wasanii?

Viongozi wa Serikali walikuwa karibu na wasanii maarufu ambao karibu wote walikuwa wakifanya filamu na mmoja wa wasambazaji wakubwa ambaye alikuwa akitoa fedha kwa wasanii na wao walikuwa wakisimamia na kuigiza, lakini haki zote zilikuwa za msambazaji huyo. Hivyo kelele za wasanii hao kuibiwa, zilikuwa ni za kampuni hiyo kupitia wao.

Watendaji wa Serikali waliopewa jukumu la utafiti wangetimiza wajibu wao japo kwa asilimia ishirini wangeligundua hili kwa kuwa liko wazi.

Kutokana na kukosekana kwa sera ya filamu, hakuna taasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa ajili ya utengenezaji, hivyo kusababisha changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa watayarishaji.

Kuna wakati Serikali ilikuwa inawahamasisha wadau wa filamu kujiunga katika vikundi ili kupatiwa mikopo na taasisi za kifedha, lakini imekuwa ngumu kutokana na wahusika kuweka wazi kuwa hawajaingia katika ukopeshaji kwenye eneo hilo.

Hivyo, Serikali ilitakiwa kufahamu kuwa inapozungumza na wasanii waliopo katika mfumo huo ilikuwa ni kama inaongea na wafanyakazi wa kampuni ya mtu binafsi. Yaani ni sawa na Serikali itake kuwakwamua kiuchumi wamachinga halafu kujua changamoto zao ikaongee na wauzaji wa maduka ya Kariakoo.

Katika kampuni zote, kampuni ya usambazaji iliyokuwepo kwa maana halisi ya usambazaji ni Proin Promotion tu, lakini nyingine zote zilikuwa zinasambaza kazi zao wenyewe kwa kuwa hata zile ambazo zilitengenezwa kwa nguvu ya watayarishaji, wakati wa kusambaza walilazimika kuuza hakimiliki kwa wasambazaji ndipo iweze kuingizwa sokoni.

Mtayarishaji filamu yeyote aliyekuwa akileta ukaidi wa kutouza hakimiliki alikuwa akishughulikiwa kwa njia mbalimbali hadi filamu hiyo ifanye vibaya sokoni.

Njia hizo ni pamoja na kufanyiwa uharamia kwa kuzalishwa kazi zake nyingi feki na kumwagwa mitaani (sijui kama ni kampuni kubwa zilikuwa zikifanya hivyo au ni sababu tu kulikuwa hakuna udhibiti kama unaofanywa na kampuni kubwa kwa kazi zao).

Mbinu nyingine ni kwa kampuni nyingine kutoa filamu nyingi kipindi unapotoa yako ili mgawane wateja.

Kimsingi hatua ya urasimishaji ilikuwa na makandokando mengi. Kuna mambo kadhaa yaliyoambatana na urasimishaji, moja ilikuwa ni kampeni za wazi za kuikataa Cosota, kampeni ambayo ilikuwa ikichombezwa na wasambazaji.

Wakati huo tayari Cosota walikuwa na sheria ya stika ambayo ndiyo sahihi katika kukabiliana na uharamia na hata kwa Serikali kupata takwimu sahihi za nakala za filamu zinazoingia sokoni, lakini wasambazaji hawakuipenda kwa kuwa ilikuwa kikwazo kwao kwa kuwa ilikuwa inahawamasisha watu wasiuze hakimiliki za kazi zao pamoja na kunusa nusa mikataba kati ya watayarishaji wa filamu na wasambazaji.

Hivyo, ili kuikwepa Cosota wakafanya ushawishi mkubwa kupitia wasanii maarufu na wadau wanaowamiliki ili TRA ndio iwe msimamizi mkuu wa nakala za filamu.

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya ni mwongozaji na mtayarishaji wa filamu kazi aliyoifanya tangu 1997.