Tishio la ebola sasa laiamsha Serikali

Muktasari:

Shirika la Afya Duniani (WHO) likitangaza hali ya hatari ya kuenea kwa ugonjwa wa ebola katika nchi za Afrika Mashariki, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kuchukua tahadhari.

Nchi zinatajwa na WHO kuwa hatarini kuenea kwa ugonjwa huo ni Rwanda, Uganda, Burundi na Sudani Kusini.

Mwanza. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likitangaza hali ya hatari ya kuenea kwa ugonjwa wa ebola katika nchi za Afrika Mashariki, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kuchukua tahadhari kwa kutoa mafunzo kwa makundi sita kutoka mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kuhusu ugonjwa huo.

Nchi ambazo zinatajwa na WHO kuwa hatarini kuenea kwa ugonjwa huo ni Rwanda, Uganda, Burundi na Sudani Kusini.

Watu zaidi ya 271 kutoka mikoa ya Kagera, Kigoma na Mwanza wamenufaika na mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza, hii pia imetokana na kuwapo mlipuko mkubwa wa ugonjwa huo eneo la Kivu ya Kaskazini mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambako zaidi ya wagonjwa 207 wamegundulika.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku sita kila siku na kundi lake, yalihusisha waratibu waelimishaji jamii, waandishi wa habari, waganga wa tiba asili, viongozi wa dini, watendaji wa kata, mitaa na vijiji, vyama vya wavuvi na waendesha bodaboda kutoka mikoa hiyo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Elimu ya Afya kwa umma kutoka wizara hiyo, Dk Ama Kasangala alisema elimu hiyo imetolewa kwa makundi hayo ili nayo yakaelimishe jamii kwenye maeneo yao kuhusu ebola.

Dk Meshack Chinyuli wa wizara hiyo, alisema kwamba takwimu zinaonyesha kwamba, hadi sasa wagonjwa 207 wameripotiwa DRC, kati ya hao 172 wamethibitika kuwa na ebola, huku wengine 35 wakidhaniwa.

“Kati ya wagonjwa hao tayari vifo 130 vimetokea, kati ya hivyo 95 vimethibitika ni kutokana na ebola, kwa hiyo utaona kasi ya mlipuko huo na ndio maana tunajipanga,” alisema Dk Chinyuli

“Ugonjwa wa ebola unaanza kuonyesha dalili baada ya siku mbili hadi 21 tangu mtu alipoambukizwa na huambukizwa kwa njia ya damu, matapishi, jasho, kinyesi na majimaji mengine ya mwilini,”alisema Dk Chinyuli.

Alitaja baadhi ya dalili za ebola ni homa kali, kuhara, maumivu ya kichwa, kutapika, uchovu, maumivu ya tumbo na kutokwa damu masikioni.