‘Ukiiga maisha yake utapasuka msamba’

Muktasari:

Mbali na muziki anatamba kuwa mmiliki wa kampuni ya usafirishaji watalii ya Akothee Safaris


Akothee anafahamika kwa majina mengi lakini maarufu ni Madam Boss na President of Single Mothers (Rais wa wanawake wanaolea watoto bila baba zao).

Mbali na muziki anatamba kuwa mmiliki wa kampuni ya usafirishaji watalii ya Akothee Safaris. Chini ya kampuni hii huratibu safari za watalii, ukatishaji wa tiketi za ndege na hoteli.

Katika mahojiano haya Akothee anafunguka kuhusu mafanikio akijigamba kuwa ndiye mwanamuziki tajiri namba moja nchini Kenya.

“Kila shilingi iliyomo katika akaunti yangu benki niliitafuta kwa jasho.” Ndivyo anavyoanza kujinasibu mwanamuziki huyo mama wa watoto watano.

Mashabiki wanakufahamu kama mwanamuziki na pia kufuatilia maisha yako ya kawaida katika mtandao, je, mbali na muziki unafanya nini?

Muziki wala sio biashara yangu kuu, ninafanya vitu vingi sana. Mimi ni mkulima mkubwa ninajishughulisha na kilimo cha miti katika shamba kubwa linaloitwa Akothee Forest.

Ninamiliki miti aina ya Eucalyptus Grandis 40,000 katika shamba hilo na kila mmoja una thamani ya Sh1,000 (wastani Sh22,704 ya Tanzania). Pia, ninamiliki kampuni ya usafirishaji watalii ya Akothee Safaris inayosimamia hoteli ya Morning Star Diani.

Kuna dhana kuwa fedha ulizonazo zimetoka kwa ‘masponsor’, je, ni kweli?

Nimepata kwa jasho langu kila senti niliyonayo. Haikuwa rahisi na wala sikuamka siku moja kutoka katika kitanda cha sponsor na kupewa fedha zote hizi.

Unasemwa sana katika mitandao ya kijamii, unawezaje kuhimili maneno ya watu?

Ajabu sasa ni watu wazima wanaofanya hivyo lakini mimi naona ni watu waliovurugwa na maisha. Kama maisha yako yamekuchanganya tafadhali usitolee hasira zako katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii.

Nini ushauri wako kwa vijana kuhusu lugha za kuudhi katika mitandao ya kijamii?

Kuna vijana wanajiua kwa sababu wanaoa wenzao kwenye mitandao wakiishi kifahari na wao hawawezi kumudu gharama hizo. Inaitwa mitandao ya kijamii na kazi yake ni kufahamiana na kubadilishana mawazo na sio kipimo cha maisha yetu. Muhimu ni kutokuiga maisha ya watu unayoona kwenye mitandao kwa sababu hata wao wanadanganya hayapo hivyo.

Ni kweli ulikuwa ukiimba nyimbo za injili?

Ndio, nilikuwa mwimbaji kanisani lakini wenzangu walinigeuka wakaanza kunisema vibaya nikaamua kuondoka zangu. Kuna mambo mengi mabaya yanaendelea katika baadhi ya makanisa.

Baadhi wanasema wewe ni mtata wengine wanasema ni muwazi, wewe unajionaje?

Mimi ni muwazi sana kiasi kwamba ndio maana sipo kwenye kundi lolote la Whatsapp maana wananitoa kwa sababu na waambia ukweli. Hata katika makundi ya familia wamenitoa kwa sababu sikwepeshi nazungumza ukweli mtupu halafu watu hawapendi.

Hata hivyo, sipendi kuwaambia wasichana mashabiki zangu wafuate maisha ninayoishi. Mimi nimeshakubali kuwa niliwahi kukosea na maisha yameendelea, wao wasiige makosa yangu.

Kwa nini una walinzi wengi?

Maisha ya umaarufu ni magumu. Inabidi nitembee na msafara mrefu. Madereva na walinzi wananigharimu fedha nyingi. Nina kama walinzi 20 lakini huwa nawachukua nikiwa na kazi maalumu sio kwamba nakuwa nao muda wote.

Gari la bei ghali unazomiliki?

Mercedes Benz SLS ambayo naitumia nikiwa Lugano, Switzerland. Ina thamani ya takribani Sh660 milioni.

Unamiliki nyumba ngapi?

Nina miliki majumba ya kifahari (mansions) tano katika miji ya Rongo, Mombasa, Normandy (France), Lugano (Switzerland), Zurich (Switzerland).

Unafanyaje manunuzi ya nguo kila mwezi?

Ninanunua Ulaya kila mwezi husafiri mikono mitupu na kurudi na mabegi makubwa mawili yakiwa yamejaa nguo.

Unatumia simu gani?

Samsung Note 8.