‘Ukosefu wa nishati ya uhakika ni kikwazo’

Muktasari:

  • Miradi hiyo ni Kinyerezi I na II pamoja na Stiegler’s Gorge ambayo baadhi inakaribia kukamilika na kupunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali.

Wakati wafanyabiashara wakitumia mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kueleza jinsi ukosefu wa umeme wa uhakika nchini ulivyo kikwazo kwao, taarifa za Serikali zinaonyesha kuwapo kwa miradi mikubwa ya nishati hiyo itakayomaliza tatizo hilo.

Miradi hiyo ni Kinyerezi I na II pamoja na Stiegler’s Gorge ambayo baadhi inakaribia kukamilika na kupunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali.

Katika mkutano huo uliofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara waliopewa fursa ya kueleza kero zao na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli wengi waligusia changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Raymond Kamtoni, kutoka Mkoa wa Katavi alisema changamoto iliyopo ni umeme akisema mradi wa umeme wa Wakala wa NIshati Vijijini (Rea) awamu ya tatu haujafika katika maeneo mengi mkoani humo.

“Tunaomba uwezekano wa kupata uememe kwenye gridi ya Taifa eneo la Mkoa wa Katavi. Mpanda kuna maeneo ya uchimbaji wa dhahabu pale, ipite pale ili iwasaidie wachimbaji hao,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte naye aligusia suala la umeme na kuitaka Serikali kutoa motisha kwa wazalishaji wadogo wa nishati hiyo ili kusaidia juhudi za uchumi wa viwanda.

Akitolea mfano nchi ya Afrika Kusini, Shamte alisema kiwango cha mwananchi mmojammoja kupata umeme katika nchi hiyo ni kikubwa ikilinganishwa na Tanzania na kutaka juhudi zaidi kumaliza pengo hilo.

Wakati wafanyabiashara hao wakieleza hayo, baadhi ya miradi ya umeme inayosimamiwa na Serikali utekelezaji wake umefikia asilimia 80 inatarajiwa kutoa umeme unaoweza kufikia Megawati 2,500 huku mradi wa Stiegler’s Gorge ukitupiwa macho zaidi kutokana na kuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100, huku Serikali ikitenga Sh700 bilioni zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, bwawa na njia za kupitishia maji katika bajeti ijayo.

Mradi mwingine unaotekelezwa ni wa makaa ya mawe Mchuchuma ambao unatarajiwa kuzalisha Megawati 220. Katika bajeti ya mwaka 2018/19, Serikali imetenga Sh5 bilioni kwa ajili kufanikisha mradi huo.

Eneo lingine ambalo linatarajia kupunguza machungu ya kukosekana kwa nishati hiyo ni miradi ya Kinyerezi I na II ambayo utekelezaji wake unatajwa kufikia hatua za mwisho.

Hivi karibuni, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema utekelezaji wa miradi hiyo unakwenda sambamba na kiu ya Serikali ya kujenga Taifa la viwanda.

“Tunataka kujenga Tanzania ya viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2019/20 tufike Megawati 5,000. Tanzania ya viwanda inahitaji umeme, mradi kama huu (wa Stiegler’s Gorge) na ile ya Kinyerezi itawezesha kufikia lengo letu,” alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, malengo ya Serikali ni kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kama sera ya Nishati ya mwaka 2015 inavyoeleza.

Mradi wa Stiegler’s Gorge ulikuwa umechelewa kuanza kwa muda mrefu lakini Juni mwaka jana, Rais John Magufuli akiwa ziarani katika Mkoa wa Pwani, alitangaza kwamba utaanza kutekelezwa.

“Stiegler’s Gorge ni mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwalimu Julius Nyerere, tutautelekeza. Nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda, ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia” alisema Rais.

Hadi kukamilika kwake, mradi huo unatarajia kugharimu Dola 2 bilioni za Marekani ambazo zitatolewa na Serikali ya Tanzania.

Miongoni mwa miradi mingine mikubwa ya umeme inayotekelezwa ni pamoja na upanuzi wa Kinyerezi III, Kinyerezi IV. Mingine ni ule wa Malagarasi ulioko Mkoani Kigoma na Lusumo Falls Mkoani Kagera.