‘Unga’, tindikali vyawa tishio kwa vijana

Muktasari:

  • Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mbeya, Dk Gloria Mbwire alibainisha hilo jana wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana baada ya Serikali kuendesha kampeni ya kupima afya bure kwa wananchi.

Mbeya. Vijana 105 wa kuanzia miaka 15 mkoani hapa wamebainika kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya na vinywaji vyenye viashIria vya tindikali, baada ya kupatiwa huduma ya upimaji vinasaba kwa binadamu (DNA).

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mbeya, Dk Gloria Mbwire alibainisha hilo jana wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana baada ya Serikali kuendesha kampeni ya kupima afya bure kwa wananchi.

Upimaji huo ulioanza Oktoba 14 hadi 18 ulifanyika kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe.

“Kimsingi hali si nzuri kwa wananchi wetu, kwa siku tano tu idadi hiyo ni zaidi ya watu 100 sasa tunaomba wazazi na jamii kuweni karibu na familia zenu katika kufuatilia nyendo shuleni,” alisema Dk Mbwire.

Mganga mkuu wa Mbeya, Dk Seif Mhina alisema wakati wakiendeelea na matibabu Serikali itaangalia namna ya kuwasaidia ili waepukane na matumizi ya dawa hizo na tindikali.

Dk Mhina aliwataka wazazi kutojikita katika shughuli za kiuchumi pekee na kushindwa kusimamia malezi bora kwa familia. hali inayozalisha kizazi kisichofaa na kushindwa kufikia malengo ya uchumi wa viwanda, kwani idadi kubwa ya vijana ni kuanzia miaka 15 ambao ni tegemezi kwa taifa.

(Hawa Mathias)