Thursday, July 12, 2018

Utafiti Twaweza waibua mapya

Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze

Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze (kulia)  akitangaza matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam, Julai 5, mwaka huu. Picha na Said Khamis 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Twaweza ikipewa siku saba kujieleza ni kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeahidi kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Jana kupitia mitandao ya kijamii ilisambaa barua inayoonyesha Julai 9, Costech iliiandikia taasisi hiyo ikitaka maelezo kutokana na kutoa matokeo ya utafiti wa Sauti za Wananchi bila kuruhusiwa.

Baadhi ya maofisa wa Twaweza waliozungumza na Mwananchi pasipo kutaka kuandikwa majina gazetini walisema barua hiyo imepokewa ofisini kwao na wataijibu kwa maandishi.

Akizungumza na gazeti hili, kaimu mkurugenzi mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu ambaye barua iliyosambaa inaonyesha ndiye aliyeisaini alisema leo watakutana na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusu barua na utaratibu unaopaswa kufuatwa na watafiti.

Awali, Dk Nungu alisema sheria kuhusu mamlaka ya Costech ipo kwenye mtandao wa tume ambayo ikisomwa itatoa majibu juu ya barua hiyo iwapo ni yao au la.

Barua hiyo inasema Twaweza iliomba kibali cha kufanya tafiti nne na kati ya hizo moja imekamilika na tatu wanaendelea kuzifanyia kazi.

Pia inaeleza Costech ndicho chombo kikuu cha kutoa ushauri katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi, na moja ya majukumu yake ni kusajili na kutoa vibali vya tafiti zote za muda mfupi na mrefu zinazofanywa nchini.

Inaelezwa katika barua hiyo kuwa, mwishoni mwa wiki Twaweza ilitoa utafiti uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi’ ambao tume hiyo haina rekodi zilizoruhusu kuchapishwa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Twaweza ilitoa ripoti ya utafiti wa Sauti za Wananchi ukielezea maoni ya wananchi kuhusu siasa nchini.

Utafiti huo umeonyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu yake tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.

Kauli za wadau

Wakili wa kujitegemea Peter Mshindilwa alisema tangu sheria ya matumizi ya takwimu kuanza kutumika, hakuna taasisi au mtafiti anayeweza kuchapisha utafiti bila kupata kibali cha Costech kwa ule wa kisayansi au Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Alisema lengo la tafiti ni kuchunguza matatizo ya jamii na kutolea majibu lakini kutokana na sheria hiyo, haitakuwa rahisi kutoa majibu ya utafiti ulio kinyume cha Serikali.

“Sheria hii ilipigiwa kelele na ni sheria kandamizi itakayoathiri maeneo mengi, hata watafiti wa vyuo vikuu hawaruhusiwi kuchapisha chochote bila kufuata sheria,” alisema wakili Mshindilwa.

Kauli hiyo iliungwa mkono na katibu mkuu wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Nacongo), Ismail Suleiman aliyesema: “Nafikiri Costech hawakukosea, wamezungumzia utaratibu wa kufuatwa na mashirika yasiyo ya kiserikali. NGOs zinahamasishwa kufuata sheria na kanuni wakati wa kutekeleza majukumu yao. Kama hao Costech wanaona Twaweza hawakufuata utaratibu, basi watashirikiana nao ili kutekeleza majukumu yao.”

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema wanasikitishwa na hatua ya Costech kuwaandikia barua Twaweza kutaka wajieleze kuhusu utafiti, akisema hilo linaminya haki za raia kujieleza.

“Jambo hili si sawa kwa sababu suala la maoni ya wananchi huwezi kuzuia, lazima waachwe wazungumze kwa sababu hayo ni maoni na si suala la takwimu,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema: “Kama barua hiyo ni ya kweli, basi ni aibu kubwa kwa Serikali kudhibiti utafiti. Tutasimama imara kulinda na kutetea hadhi ya utafiti ili mradi utafiti huo uwe unakidhi vigezo.”

Alisema kwa miaka mingi Twaweza wamekuwa wakifanya tafiti na Costech walikuwapo, akidai kwa sababu utafiti wa hivi karibuni umeigusa Serikali, wamejitokeza wakisema hawajafuata taratibu.

“Ninavyofahamu taasisi yoyote ikitaka kufanya utafiti lazima iwasiliane kwanza na NBS (Ofisi ya Taifa ya Takwimu). Ni jambo la kushangaza kama utafiti hauwezi kufanyika kama haujapata approval (kibali) ya Costech, suala hili linaibua mjadala,” alisema.

Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Elias Msuya na Peter Elias

-->