Uwoya alivyoshiriki kuaga mwili wa Masogange

Muktasari:

  • Uwoya ndiye aliyemsindikiza mtoto wa Masogange kuaga mwili wa mama yake

Msanii wa filamu, Irene Uwoya ameonekana kuwa ngangari katika kuaga mwili wa rafiki yake wa karibu, Agnes Gerald ‘Masogange’.

Uwoya ni miongoni mwa marafiki wa karibu wa Masogange na walipanga nyumba moja eneo la Makongo Juu jijini Dar es Salaam.

Katika shughuli za kuaga mwili wa Masogange leo Aprili 22, 2018 katika viwanja ya Leaders Club, Uwoya alishiriki kuchukua mwili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuupeleka viwanjani hapo.

Uwoya alikuwa ndani ya gari lililobeba mwili wa Masogange na baadaye alibeba msalaba wakati wa kuingia viwanjani ilikofanyika ibada.

Wakati wa kuaga mwili, Uwoya ndiye aliyemsindikiza mtoto wa Masogange kumuaga mama yake.

Mtoto huyo aliinamia jeneza la mama yake akilia, huku Uwoya akimbembeleza naye akitokwa machozi.

Wawili hao walisaidiwa na waombolezaji wengine kuondoka lilipokuwa jeneza.