‘Vijana watumiaji wakubwa wa viroba’

Muktasari:

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema zuio la viroba litasaidia kupunguza ajali kwa madai madereva wengi wa bodaboda wanatumia kilevi hicho.

Dar es Salaam.  Matumizi makubwa ya pombe za viroba yapo kwa vijana, wakiwamo madereva wa bodaboda, daladala na makondakta, imebainika.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema zuio la viroba litasaidia kupunguza ajali kwa madai madereva wengi wa bodaboda wanatumia kilevi hicho.

“Kila tukivamia kijiwe cha bodaboda na kufanya ukaguzi tulikuta baadhi wakiwa wamehifadhi viroba kwenye mifuko ya suruali. Viroba viliwafanya wawe na ujasiri, kutoogopa, kukimbiza bodaboda na kuhatarisha maisha yao na abiria,” amesema.

Baadhi ya bodaboda, akiwamo Athuman Hamis wa Ubungo, wamesema wanatumia pombe hiyo ili kuongeza ujasiri kazini licha ya kuwa wanajua ni hatari.

Daktari Bingwa Mwandamizi wa Tiba na Afya ya Akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Frank Masao amesema kitu chochote chenye uwezo wa kubadili ufanyaji kazi wa ubongo wa binadamu ni dawa za kulevya.