Vilivyomo ndani ya Dreamliner ya ATCL

Muktasari:

Ndege hiyo ni miongoni mwa ndege kubwa na ya kisasa kwani kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mwishoni mwa mwaka 2009 lakini ilianza kutumika katika mashirika mbalimbali mwaka 2011. Spidi yake hufikia mpaka kilomita 956 kwa saa.

Julai 29 ndege aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner) ya Shirika la Ndege la ATCL ilianza safari yake ya kwanza tangu ilipotua nchini Julai 8 mwaka huu ikitokea Marekani ambako ndiko ilikoten-genezwa.

Ndege hiyo ni miongoni mwa ndege kubwa na ya kisasa kwani kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mwishoni mwa mwaka 2009 lakini ilianza kutumika katika mashirika mbalimbali mwaka 2011. Spidi yake hufikia mpaka kilomita 956 kwa saa.

Dreamliner imekuwa ikitumiwa na mashirika makubwa ya ndege duniani ikiwemo Fly Emirates, Qatar Airlines, Japan Airlines na kwa Afrika zipo katika mashirika ya ndege ya Ethiopia na Kenya.

Kwa sehemu kubwa ndege hiyo ya ATCL yenye injini mbili za jet, imeten-genezwa na Kampuni ya Boeing Commer-cial Airplanes ya nchini Marekani lakini injini zake zimetengenezwa na kampuni ya Rolls-Royce ya Uingereza.

Urefu wake ni mita 56.72, kimo kwenda juu ni mita 16.92 na upana wa mabawa yake ni mita 60.12, madirisha yake yana upana wa sentimita 27 kwa 47. Uwezo wa ndege hiyo mpya ni kubeba abiria 262 na mizigo yenye kilo za ujazo 136.7.

Kama kawaida ya ATCL, ndege zao hupambwa kwa rangi nyeupe na bluu huku picha ya mnyama twiga ikiwa kwa nyuma, maneno yanayosomeka ‘Air Tan-zania the wings of Kilimanjaro’ yamean-dikwa ubavuni mwa ndege zote za ATCL lakini imeongezewa lingine la ‘Hapa kazi tu’.

Kwa ufupi ndege hiyo yenye uwezo wa kutumiKa kwenye viwanja vyenye eneo la kukimbilia la kuanzia kilometa 2.6, mwonekano wake wa nje ni mzuri na wa kupendeza, hata ipitapo angani unaweza usichoke kuitazama.

Kama ambavyo mtu anayeitazama ikiwa angani hawezi kuchoka, vilevile msafiri aliyepo ndani ya ndege hiyo naye hawezi kutamani kufika mwisho wa safari yake.Nikiwa miongoni mwa abiria 257 walio-safiri na ndege hiyo wakati ilipofanya safari yake ya kwanza ikitokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza kwa kupita Kilimanjaro, nilianza kufurahia huduma ya ndege hiyo tangu nikiwa uwanja wa ndege.

Ukarimu wa watoa huduma sehemu ya ukaguzi ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ulikuwa wa kiwango kikubwa hata katika dirisha la ATCL la kutolea pasi za kuingia ndani ya ndege.

Kulikuwa na changamoto ya wingi wa watu waliokuwa wamepanga kusafiri na ndege hiyo ambayo ilikuwa inafanya safari yake ya kwanza nchini lakini watoa huduma walijitahidi kutoa huduma kwa haraka zaidi.

Sehemu ya ukaguzi wa abiria wa safari za ndani ilikuwa na watu wengi kuliko kawaida kiasi kwamba mtu alitakiwa kusubiri kwa dakika takribani 20 ili kukaguliwa suala lililosababisha muda wa kuanza kuingia kwenye ndege (Boarding time) kuchelewa.

Baada ya ukaguzi chumba cha kusubiri muda wa kuingia kwenye ndege nacho kilikuwa na idadi kubwa ya watu ambao walipungua ghafla baada ya ndege hiyo kuanza kupakia.

Muda wa kuanza kuingia kwenye ndege ulikuwa saa 11:20 alfajiri lakini kutokana na kuchelewa kwa ukaguzi uliosababishwa na wingi wa abiria, watu walianza kuingia kwenye ndege saa 11:35 wakitanguliwa na waandishi wa habari na viongozi kadhaa.

Tiketi za ndege hiyo zilionyesha kuwa ingeondoka uwanjani saa 12 kamili lakini kutokana na wingi wa watu uliosababisha kuchelewa kwa ukaguzi, ndege hiyo iliruka dakika 35 baadaye (saa 12:35).

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali walikuwa miongoni mwa abiria wa ndege hiyo ambayo iliruka umbali wa futi 28,000 juu wakati ikielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Ndani ya ndege kulikuwa na wahudumu wengi (kwa idadi ni takribani 10) waliokuwa wakarimu kwa wateja wote. Walimkaribisha kila mmoja kwa kumtaja jina lake kisha kumuonyesha mahali alipopaswa kukaa.

Kabla ya ndege hiyo kuondoka abiria wote walihesabiwa na baadaye wahudumu walitoa matangazo ya usalama.

Tofauti na ndege nyingine za ATCL (Bombardier Q400) matangazo ya usalama katika ndege hii yanatolewa kwa njia ya video kupitia ‘screen’ iliyopo mbele ya kila kiti.

Screen hiyo pia inatumika kutoa taarifa za umbali ndege iliyopo kutoka usawa wa bahari, muda unaotarajiwa kukamilisha safari, mwendo kasi na hali ya hewa na burudani tofauti.

Abiria wengi waliokuwa katika ndege hiyo siku ya kwanza ya safari walikuwa wakipiga picha za selfie na kusifia uzuri wa ndege ambayo viti vyake vimekaa kwenye mstari wa viti tisa kwa upana (3 by 3 by 3).

Ukiachilia mbali spika ambazo zinatumika kwa ajili ya matangazo ndani ya Dreamliner kila kiti kina sehemu ya kuchomeka ‘eaphone’ kwa ajili ya kuendelelea kupata burudani mbalimbali na matangazo yanapoanza kama ulikuwa unasikiliza muziki utasimama kwa muda kupisha tangazo.

Kwa walioozoea kusafiri na ndege ndogo wanaweza wakapata tabu wakati wa jua kali kwa kushindwa kujua namna ya kufunga kioo. Ndani ya dreamliner hakuna kitu cha kuvuta ili kufunga kioo bali mambo yapo kielektroniki.

Ni mwendo wa kubonyeza batani ambazo hujaza giza katika kioo na ukitaka kufungua vilevile ni kubofya tu.

Upande wa utulivu ndege hiyo imetulia hata inapopita katika mawingu madogo, muundo wake huwafanya abiria wasisikie kelele na mitetemo hata wakati wa kutua na kupaa ndege hiyo imetulia.

Kwa waliosafiri na ndege hiyo kwa mara ya kwanza wakitokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza au Kilimanjaro walipata zaidi ya safari kwani walifanya na utalii katika Mlima Kilimanjaro.

Wakati wa kutoka uwanja wa ndege wa Kia, muda uliotangazwa kuwa ungetumika kutoka Kia mpaka Mwanza ulikuwa ni dakika 40 lakini ndege hiyo ilitumia dakika 70 kwani dakika 30 zilitumika kuvinjari mandhari ya mlima huo mrefu kuliko yote Afrika.

Wakati Dreamliner ikikatiza juu ya mlima Kilimanjaro abiria walionyesha shauku ya kutaka kuuona vizuri mlima, ndipo rubani wa ndege hiyo akawafurahisha kwa kuuzunguka mara mbili kwa spidi ndogo na ndege ikiwa kwa chini zaidi.

Tukio hilo liliwavutia watu wengi, kuna ambao walichukua picha kupitia kamera na simu zao za mkononi na wengine walidiriki kusema kuwa hawana haja ya kupanda mlima huo kwani wameutalii kiasi cha kutosha.

Ukiachilia mbali burudani hiyo abiria wa ndege hiyo waliburudishwa na burudani ya muziki, sinema, michezo (games) kwa kadiri walivyohitaji kwani mambo yote yalikuwa kwenye ‘screen’ ya mbele ya kiti walichokuwa wamekalia.

Hata hivyo lugha inayotumika katika kifaa hicho cha burudani ni Kiingereza hata nyimbo zilizopo ni za Kiingereza lakini kuna kipande kidogo cha filamu ya Kiswahili kiitwacho Inside Bongowood. Hivyo wapenzi wa nyimbo za Kiswahili na filamu za hapa nyumbani kwao haikuwa habari njema.

Upande wa viburudisho vingine (vyakula) abiria wa ndege hiyo waliosafiri asubuhi walipewa juisi/maji na kipande cha keki na kwa abiria wa jioni walipatiwa korosho na vinywaji zikiwemo bia na mvinyo hivyo kwa wapenda vileo hufurahia wakati huo kwani hakuna idadi kamili ni kunywa mpaka unapomaliza safari yako.

Huenda tangazo linalovutia zaidi katika ndege hiyo na nyingine za ATCL ni lile linalotoa nafasi ya mtu kuomba jambo lolote kutoka kwa wahudumu wa ndege ambalo litamfanya afurahie safari ya ndege zao.

WiFi haikupatikana

Wakati ndege hiyo ikipaa kutoka JNIA kuelekea Kia abiria walitangaziwa kuwa kuna huduma ya WiFi ambayo ikiwa tayari wataarifiwa lakini hilo halikufanyika, ilikuwa vivyo hivyo wakati wa kutoka Kia kuelekea Mwanza.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa ATCL, Joseph Kagirwa anafafanua kuwa sababu ya kukosekana kwa huduma hiyo ni kwa kuwa ndege hiyo haijakaa angani muda mrefu kwa safari zote hizo mbili.

“Ili WiFi iweze kufanya kazi ndege inabidi ikae angani saa nzima ndipo inaweza kufanya kazi kwa sababu inatumia satellite, lakini tunaangalia kama kuna maboresho yanaweza kufanyika ili ifanye kazi muda wote,” anasema Kagirwa.

Kagirwa anasema kwamba mfumo mwingine wa simu unaotajwa ni kwa ajili ya matumizi ya watoa huduma za ndege si abiria.