‘Waandishi wa habari kuweni na umoja’

Muktasari:

Akizungumza jana katika hafla ya kuiaga na kuikaribisha bodi mpya ya MCT jijini Dar esSalaam, Jaji Mihayo amesema tasnia ya habari kwa sasa inapita katika mawimbi makubwa, hivyo unahitajika ushirikiano ili kuyashinda.

Dar es Salaam. Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji mstaafu Thomas Mihayo amewataka waandishi wa habari kuwa na umoja na kuaminiana na Serikali ili kufikia lengo la kuwatumikia wananchi kwa pamoja.

Akizungumza jana katika hafla ya kuiaga na kuikaribisha bodi mpya ya MCT jijini Dar esSalaam, Jaji Mihayo amesema tasnia ya habari kwa sasa inapita katika mawimbi makubwa, hivyo unahitajika ushirikiano ili kuyashinda.

“Tunapita katika mtikisiko sana, pamoja na mawimbi vile vile, hata katika tasnia yetu tumeingiliwa, hata katika mitandao ya kijamii utaona, tumeingiliwa.

“Serikali yoyote iliyopo madarakani ni mdau wa habari kwa sababu lazima itegemee kufikisha ujumbe kwa wananchi na haiwezi kufanya kazi peke yake,” alisema Jaji Mihayo.

Akizindua bodi hiyo, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mwandishi Nguli, Hamza Kasongo alisema MCT imesaidia nchi kadhaa kushawishi kuanzishwa kwa Baraza la Habari.

Kasongo alisema: “Wanahabari wanapitia kipindi kigumu cha majaribio.”

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu ambaye ni mmoja wa wajumbe wa bodi ya MCT alisema vyombo vya habari na Serikali, Bunge au Mahakama wanapaswa kuwa wadau wanaotegemeana kutokana na umuhimu wake kwenye jamii.

“Waandishi wa habari wanapaswa kuwa na umoja kwani tasnia yetu inahusisha vyombo vinavyotoa uamuzi na tunaunganishwa na mihimili mitatu na ndiyo maana wanasema waandishi wa habari ni mhimili wa nne,” alisema Machumu.