Wadau waeleza kwa nini ni muhimu kushiriki Top 100

Aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mashindano ya kwanza ya Top 100 wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Lazaro Nyalandu (kushoto) akiwa meza kuu na wageni wengine. Kushoto kwake ni aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara, Raymond Mbiinyi na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam, Gabriel Kitua. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Wajasiriamali na watalaam wabobezi wa masuala ya biashara na uwekezaji pamoja na baadhi ya wshiriki wa mashindano ya Top 100 wamebainisha jinsi jukwaa hilo lilivyo muhimu kwa wafanyabiashara wa kati kukuza miradi hayo na kuongeza mchango wao kwenye uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wakati fainali za shindano la kampuni za kati (Top 100) zikitarajiwa kufanyika Alhamisi hii, wadau wameeleza umuhimu wake kwa washiriki na uchumi kwa ujumla.

Mwaka huu, itakuwa ni msimu wa nane wa mashindano hayo ambayo hutoa tuzo kwa kampuni 100 bora zenye mpato kati ya Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni.

Aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mashindano hayo mwaka 2011, Ali Mafuruki anasema Top 100 huwakumbusha wamiliki nidhamu ya uendeshaji wa kampuni.

Na, kwa miaka saba iliyopita, anasema Top 100 imesaidia kampuni nyingi kuelewa umuhimu wa kutunza kumbukumbu zao kwa kuwa ni miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa kwa washiriki wote ambao wanapaswa kuwa na hesabu za miaka miwili zilizokaguliwa.

“Kwa kampuni ambazo hazikuwa na utamaduni wa kuhifadhi hesabu za fedha na kukaguliwa kwa kuhofia umma kujua kiasi cha fedha zao, mchakato wa Top 100 unazijengea uwezo na kuondoa woga huo na kuanza kufuata mifumo sahihi ya uendeshaji wa biashara,” anasema Mufuruki.

Hofu nyingine iliyopo, anasema ni kampuni kuamini kuwa endapo zikibainisha hesabu zake Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaanza kuzidai kodi kubwa zaidi ndiyo maana washiriki wa awamu ya kwanza walikuwa wachache hadi pale walipoanza kuona manufaa.

Mufuruki ambaye pia ni mwenyekiti wa kampuni ya Infotech Investnment Group anasema: “Kwa ujumla Top 100 imesaidia kuziibua kampuni ambazo zilikuwa zinaogopa kuweka wazi taarifa zake kwa ajili ya umma, hata hivyo zilikuwa hazikui.”

Licha ya kuboresha taarifa za fedha hivyo kujiongezea nafasi za kufanya biashara kimataifa na kukopesheka hivyo kuwa na uhakika wa kukua zaidi, Mufuruki anasema ni fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara, sekta binafsi, Serikali na vyombo vya habari ili kukuza biashara.

Fursa hizo muhimu hupatikana hasa kwa kuzingatia kanuni za uendeshaji biashara kisasa.

Mufuruki anasema tuzo hizo zimesababisha kampuni kuweka wazi taarifa zake za fedha hivyo kukua zaidi na kulipa kodi ya Serikali ambayo ni muhimu katika uchumi endelevu wa nchi yoyote duniani.

Si Mufuruki pekee anayeziona faida kemkem za mashindano hayo, wapo wadau wengine pia wakiwamo washiriki, waandaaji na wadhamini wanaoitazama Top 100 kama kipimo cha kujitathmini na daraja la kuelekea kuwa kampuni kubwa.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya BQ Contractors iliyokuwa mshindi wa kwanza shindano la Top 100 mwaka 2011, John Bura anasema hivi sasa wamepata mafanikio makubwa tangu walipotangazwa kutwaa taji hilo.

Licha ya changamoto za fedha, utaalamu na vifaa, anasema bado wameweza wanakua kwa kasi kubwa huku wakijikita zaidi katika ukandarasi wa mafuta na gesi ambako wanaamini kuna fursa nyingi zaidi za kukua na kujitanua.

“Nina ushahidi juu ya manufaa ya ushiriki wa kampuni yetu katika mashindano ya Top 100 kwani tulipata zabuni za kutekeleza miradi mingi. Tulikuwa hatukosi zabuni mbili kubwa kwa mwaka,” anasema.

Kwa kipindi baada ya kutangazwa washindi, anasema walianza kupata miradi mikubwa na midogo ambayo ni zaidi ya 40 kwa mwaka tofauti na ilivyokuwa awali kutokana na kuongezeka kwa uaminifu wa wadau kwa kuiona nembo ya Top 100.

Bura anasema mwaka huu kampuni yake imetunukiwa cheti cha ubora wa kimataifa ISO 9001:2015 hivyo sifa yake imeendelea kuwa kubwa na kuaminiwa na wengi zaidi hasa kampuni za kimataifa.

Siku chache baada ya kufanyika kwa mashindano ya Top 100, kampuni ya Puma ilitangaza zabuni ya kujenga bomba la mafuta kutoka bandarini hadi kwenye eneo lao la kuhifadhia nishati hiyo lakini licha ya kampuni nyingi za ndani na nje kuomba kazi hiyo, wao ndio walioshinda.

Anasema walishinda ingawa bei yao ilionekana kubwa lakini Puma waliwataka waipunguze kwani walitaka kufanya kazi na mshindi wa Top 100.

Mkurugenzi mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando anasema kampuni yoyote ndogo inayotaka kujipima na nyingine au kujipima yenyewe suluhisho ni jukwaa la Top 100 lenye washauri wenye utaalamu unaohitajika kufanikisha nia hiyo.

“Top 100 kwa wafanyabiashara ni kipimo cha hatua waliyopiga tangu walipoanzia mpaka walipofika na kutambulika kutokana na tija yake kwa wamiliki na Taifa. Ni kipimo cha ufanisi wa maendeleo ya biashara,” anasema Mhando.

Azam TV ni mdau muhimu wa mashindano hayo kwani hurusha kilele cha Top 100 pamoja na kutoa nafasi ya washiriki kueleza shughuli zao pamoja na kuwakutanisha kwa ajili ya mazungumzo ya kubadilishana uzoefu.