Thursday, July 12, 2018

Wadau wahofia utekelezaji mwongozo wa biasharaMkurugenzi wa kampuni ya PwC, Joseph Lyimo

Mkurugenzi wa kampuni ya PwC, Joseph Lyimo 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadau wa sekta binafsi wameeleza kuhofia utekelezaji wa mwongozo wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Hofu hiyo inatokana na muda wa kuanza kutumika kwa mwongozo huo kukaribia lakini wafanyabiashara wakiwa hawafahamu anayeuratibu mwongozo huo.

Akizungumza kwenye mkutano wa uchambuzi wa bajeti uliondaliwa na Umoja wa Watendaji wa Kampuni Binafsi (Ceort), mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya PwC, Joseph Lyimo alisema mwongozo ni mzuri lakini haijafahamika nani atasimamia utekelezaji wake.

Alisema ni muhimu suala hilo lingefahamika mapema ili wafanyabiashara wajiandae na kujua ni yupi watafanya naye kazi na itafanyika vipi.

“Mwongozo una mambo mengi mazuri lakini haijawekwa wazi ni nani atakayeuendesha na kusimamia utekelezaji wa mambo yote yaliyomo ndani, hapo ndipo tunaona kuna changamoto ikizingatiwa waziri alisema utaanza kufanya kazi mwaka huu wa fedha,” alisema mkurugenzi huyo.

Mwenyekiti wa Ceort, Sanjay Rughani alisema: “Jitihada zinazofanywa na Serikali zinatupa moyo hasa ukiangalia mipango ya maendeleo inavyotekelezwa ila kuna maeneo yanatakiwa yaangaliwe kwa umakini zaidi mfano ukusanyaji kodi, uendeshaji biashara na utungaji wa sera,” alisema.

-->