Wagombea wanane wapitishwa Monduli

Muktasari:

Baadhi ya wagombea hao ni Julius Kalanga (CCM), Yonas Laizer(Chadema) na Omar Kawanga(DP).

Wengine ni Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini),Fransis Ringo(Ada-Tadea).

Arusha. Jumla wa wagombea wanane wamepitishwa kuwania ubunge jimbo la Monduli mkoa wa Arusha.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, leo Agosti 21 Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo la Monduli, Stevin Ulaya amesema wagombea wote wamepitishwa baada ya kukidhi matakwa ya uchaguzi.

Ulaya amewataja wagombea hao kuwa ni Julius Kalanga (CCM), Yonas Laizer(Chadema) na Omar Kawanga(DP).

Wengine ni Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini),Fransis Ringo(ADA-TADEA).

Ulaya amewataja wagombe wengine waliopitishwa kuwa ni pamoja na Elizabeth Salewa (AAFP) na Wilfred Mlay (ACT-Wazalendo).

Hata hivyo katika uchaguzi huo,Upinzani mkubwa upo kati ya wagombea wa CCM na Chadema ambao wanatoka kata moja ya Lepurko.

Laizer ambaye pia ni diwani wa kata alipitishwa kugombea kwa tiketi ya Chadema na atachuana na Kalanga wa CCM katika uchaguzi wa Septemba 16.

Mkazi wa Monduli, Lenana Mollel alizungumzia kinyang’anyiro hicho na kusema hata kabla ya Kalanga kuhamia Chadema alikuwa akipambana na Laizer hivyo wao kuwania jimbo hili kunaongeza makali.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Loota Sanare ametamba kuwa tayari CCM imeshinda uchaguzi huo kwani inakubalika Monduli.

"Monduli wamejua makosa waliyofanya sasa wameona kazi nzuri za serikali na wanaiunga mkono," amesema.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa Arusha, Aman Golugwa ametaka uchaguzi uwe huru na haki na kusema kuwa  wanauhakika wa ushindi asubuhi.

"Tumejipanga kutetea jimbo tunajua wana Monduli wanahasira baada ya Kalanga kurubuniwa na kuwatoroka ila hasira zao zitaonekana siku ya uchaguzi," amesema.

Uchaguzi huo utafanyika Septemba 16 baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Kalanga, kutangaza kukihama Chadema na kuhamia CCM.