Sunday, February 18, 2018

‘Wakorea Weusi’; kundi hatari lililogeuka tishio mjini Mbeya

Ofisa Matangazo wa Kampuni ya Mwananchi

Ofisa Matangazo wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ldt (MCL) wa mkoa wa Mbeya, Amos Chuma akiwa nyumbani kwake eneo la Mwakibete Jijini Mbeya akiuguza majereha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana kisha wakampiga na kumpora fedha na vitu mbalimbali juzi usiku. Picha na Godfrey Kahango 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Ukitaja neno ‘Panya Road’ wakazi wa Jiji la Dar es Salaam watakuelewa unazungumzia kundi hatari la vijana waliokuwa wakifanya uhalifu mitaani na kuhatarisha amani na usalama wa wananchi.

Katika kila eneo ambalo makundi haya yamekuwa yakiibuka na Serikali imekuwa ikitumia vyombo vyake vya dola kukabiliana nayo na kuyasambaratisha ili wananchi waendelee kuishi kwa amani na utulivu.

Katika siku za hivi karibuni, makundi ya aina hiyo pia yameanza kuibuka jijini Mbeya huku yakiwa yamejipachika majina ya ‘Wakorea Weusi’ na ‘Wanyamanyafu’ ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa raia na mali zao, mchana na usiku.

Kwa sasa wakazi wa jiji hilo wamejawa na hofu ya kuvamiwa, kuporwa, kuibiwa na kuumizwa nyakati hizo na kuvunjiwa nyumba zao.

Maeneo ambayo ni hatari kwa kuwa na makundi hayo ni Kabwe, Mwanjelwa, Soweto, Mama John, Mwakibete, Ilemi, Isanga, Ilomba na Mafyati ambapo makundi hayo yakiwa na silaha za jadi huvamia watu, kisha kuwapiga na kuwapora mali wanazokuwa nazo.

Wakati mwingine makundi hayo huingia kwenye nyumba za watu mchana na kuiba vitu mbalimbali hasa vinavyobebeka kwa urahisi.

Miongoni mwa watu waliovamiwa na kujeruhiwa kabla ya kuporwa fedha na simu ni mkazi wa Mwakibete, Amos Chuma ambaye ni ofisa matangazo wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd mkoani Mbeya, aliyevamiwa saa moja usiku akiwa mita chache kabla ya kuingia nyumbani kwake siku ya Jumanne ya wiki hii.

Akisimulia tukio hilo, Chuma anasema: “Wakati natoka kazini, nilishuka katika usafiri wa bajaji eneo la Mwambene na kabla ya kwenda nyumbani kwangu niliingia kwenye moja ya vibanda vya M-pesa, niliweka Sh300,000 kwenye simu na kiasi kidogo kama Sh260,000 nilibaki nacho mfukoni kwa sababu nilipanga kuja kuwalipa mafundi wangu hapa nyumbani,” anasema Chuma.

Anasema kwamba baada ya kuweka fedha hizo alianza kuelekea nyumbani kwake na hakujua kama kulikuwa na watu wanamfuatilia nyuma yake.

Chuma anasema alipokaribia nyumbani kwake ghafla alijikuta anavamiwa na watu wanne ambapo alipigwa kitu kizito kichwani na kupoteza fahamu.

“Kwa kweli baada ya kupigwa tu sikujua kilichoendelea kwani nilipoteza fahamu, lakini baada ya muda niliinuka nikaanza kurudi nilikotoka nikijua nakwenda nyumbani huku nikiwa nimetapakaa damu mwilini,”anasema na kuongeza: “Ndipo watu wa mtaa huu (wa Mwakibete) wakanifahamu na kuanza kuniuliza imekuaje? Hapo hata sikuwaambia chochote, kwani nilikuwa sijui kilichotokea.Wakanileta hadi nyumbani.”

Chuma anasema alipopelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, alishonwa nyuzi tisa kichwani na jicho lake la kulia lilionekana kuathiriwa kwa ndani.

Anasema baada ya kutulia kwa muda ndipo alipobaini kwamba ameporwa simu, fedha taslimu pamoja na pochi iliyokuwa na vitambulisho vyake.

Mkazi huyo anasema, “kwa muda mrefu kuna vijana wamejipachika jina la Wakorea Weusi, wapo eneo la Mabanzini, hawa watu wamekuwa tishio sana wanazunguka nyakati za usiku na kufanya uhalifu wa kupora na kupiga watu, yaani sasa hivi watu katika sehemu za kazi unakuta wanaambizana tuwahi kurudi nyumbani kabla Wakorea Weusi hawajaanza kazi yao.”

Wenyeviti wa mitaa walonga

Mwenyekiti wa Serikali mtaa wa Kati katika Kata ya Ruanda, Bryton Ndibinze anazungumzia kundi jingine la kihalifu linalojiita Wanyamanyafu akidai kuwa ni tishio na wamefikia hatua ya kuvunja nyumba za watu na kuiba mchana.

“Si siri hali kwa sasa si shwari kabisa, watu wanapigwa na kujerhusiwa sana na watu hawa nyakati za usiku, lakini kama haitoshi wamefikia hadi kuiba mchana kweupe,” anasema Ndibinze.

“Huku kwangu kuna sehemu inaitwa Kagera, vijana hatari wanashinda kwenye car wash wanajifanya wanaosha magari, lakini hiyo si kwa wote wengine kazi yao ni kuchungulia nyumba za watu, wakiona hakuna mtu basi wanavunja na kuiba tv, redio na wakitoka wanabeba mkononi tu. Ukiwauliza wanakwambia imeharibika, wanaipeleka kwa fundi wakati wametoka kuiba.”

Wananchi walalamikiwa

Ndibinze anasema tatizo kubwa wanalokumbana nalo kama viongozi wa mtaa ni kutopata ushirikiano wa kukomesha vitendo hivyo kutoka kwa wananchi, ambao wamekuwa wanawaficha licha ya kuwa wanaishi nao mitaani.

“Na si kwamba vijana hawa hawafahamiki, wanafahamika vizuri tu na wananchi, lakini shida kubwa niliyoigundua ni kulindana kwa misingi ya ukabila. Hapa mjini kuna makabila makubwa mawili (anayataja), sasa sisi viongozi tukimfahamu mhalifu tukimkamata wanakuja juu na kuanza kumtetea eti huyu ni mtoto wa fulani, ni ndugu yetu hawezi kufanya hivyo, mnamuonea tu,” anasema kiongozi huyo. Hata hivyo, inapofika usiku watetezi wenyewe hugeukwa kwa kupigwa mapanga na kuporwa.

Waanzisha sungusungu

Mwenyekiti wa Mtaa wa Makunguru, Emiliana Siulanga anasema kutokana na tishio la makundi hayo mtaani kwake wameanzisha ulinzi wa jadi mfano wa sungusungu unaoendeshwa kimyakimya ambao umesaidia kupunguza watu kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa.

“Kweli huko nyuma huu mtaa ulikuwa haukaliki, kila siku asubuhi lazima usikie fulani kavamiwa usiku wakati anarudi nyumbani kwake au alfajiri wakati anakwenda kwenye majukumu yake. Lakini tangu auawe na wananchi mmoja wa vibaka wale waliokuwa wanavunja duka eneo la Mwenge, wenzake hawajarudi tena, hivyo kumetulia kidogo,” anasema.

RPC alia na watetezi

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema kuna kikundi cha vibaka waliojiita ‘Wakorea’ na tayari walishatiwa mbaroni tangu Desemba na kesi yao ipo mahakamani.

Mpinga anasema mbali na vijana hao, pia polisi waliwakamata vijana wengine wanaojihusisha na uvamizi na kuwapiga watu kwa lengo la kupora nyakati za usiku.

Anasema kwa sasa wanaendelea na msako wa kubaini kama watu hao wanatumiwa na watu fulani kufanya uhalifu huo ikiwa ni pamoja na wanaokwenda kuwauzia mali za wizi. “Hao wanaojiita Wakorea tulishawatia mbaroni na tulipowahoji tulibaini ni wavuta bangi, labda kimeibuka kikundi kingine hicho cha Wakorea Weusi, lakini tunaendelea kuimarisha ulinzi kwa kufanya doria muda wote,” anasema.

Pia, Kamanda Mpinga anaunga mkono kauli ya mwenyekiti Ndibinze akiwatupia lawama wananchi kuwalinda na kuwatetea watu wanaokamatwa kwa kufanya uhalifu, jambo ambalo linawafanya kuwapa kiburi wahalifu hao.

“Kuna wakati tuliwakamata vijana wengi sana maeneo ya Mafyati na kuwaweka ndani, lakini wananchi walikuja juu sana kutulaumu na wakatugeuzia kibao eti tunakamata wanaovaa milegezo na wanaonyo staili za ajabu ajabu wakati si kweli. Wale ndio wanaowaumiza watu usiku kwa kuwapiga na kuwapora,” anasema.

“Hivyo niwaombe sana wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kutupa taarifa za wahalifu na uhalifu unapotokea mara moja.

“Askari wanafanya doria saa 24, lakini ni wachache hivyo hawawezi kuwepo kila eneo la tukio au kujua ni wapi kuna watu wa aina hiyo isipokuwa wananchi wanawajua hawa (wahalifu) kwani wanaishi nao kwenye nyumba zao, hivyo watupe ushirikiano, lakini vilevile wale wenye mtindo wa kuwatetea wanaokamatwa kwa uhalifu waache mara moja.”

-->