Askari waliopigana vita ya pili ya dunia wataka kumuona Rais Magufuli

Muktasari:

  • Chama Cha Askari Wastaafu ambao wamepigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia (TLC , wamedhamiria    kumuona  Rais John Magufuli , wametaka kupatiwa bima ya afya na majengo ya ofisi

Chama Cha Askari Wastaafu ambao wamepigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia (TLC), wameiomba serikali kuwajali na kuwakumbuka katika kuwapatia kiinua mgongo, bima ya afya na majengo ya ofisi huku wakiazimia kukutana na Rais John Magufuli.

Akizungumza leo  na waandishi wa Habari Mwenyekiti wa TLC Taifa, Rashidi Ngonji amesema wastaafu hao wameshasahaulika  kitendo ambacho kinawasikitisha kwa kukosa haki hizo huku wengi wao wakiwa ni masikini wasiojiweza.

“Sisi tumepigana vita kuu ya pili ya dunia kuanzia 1939 hadi 1945, wakati huo Mwingereza alikuwa mkoloni kwa kuona kazi tulioifanya alitujengea majengo yetu na kutupa fedha lakini kwa sasa majengo hayo tumepokonywa na kuambiwa wameyarithi jambo ambalo siyo kweli,” amesema Ngonji.

Ngonji amesema wamesahaulika na hakuna anayewajali katika hali waliyokuwa nayo ili hali walishirikiana na Mwingereza kumuondoa Mjerumani ndio ilipopatikana Tanganyika na kuahidiwa  kujengewa majengo ambayo yangekuwa ofisi zao na kutambulika.

“Mwingereza ametuahidi  kutusomesha kwani awali tulikuwa tunazolewa kipindi hicho tumerudi jeshini baada ya kumuondoa Mjerumani na Mwarabu walioshirikiana lakini tangu tumepata uhuru hakuna anayetujali hivyo tumebaki kama ombaomba na hali za maisha yetu ni ngumu  hata kiiunua mgongo hatupewi,” amesema mwenyekiti huyo ambaye ni Askari Mstaafu.

Mmoja wa Askari wastaafu Peter Mteregure amesema viongozi wote ambao wamepita na kumaliza muda wao hawajawahi kuzungumza nao hivyo kujikuta kama siyo mashujaa waliofanikisha nchi kuwa huru.

Amesema maisha yao yamekuwa ya taabu huku akiwataja baadhi ya wanajeshi saba ambao hawawezi kutembea na muda wowote wanaweza kufa kwa kukosa matunzo stahiki ikiwemo mafao yao kama wastaafu.

“Chama hiki kina miujiza kwa sababu  viongozi hawawajibiki na leo katika mkutano huu moja ya ajenda ni kupata viongozi wapya ili watuwezeshe kukutana na Rais,” amesema Mteregure.

Katibu wa Kaimu Katibu Mkuu TLC, Charu Lubala amesema tayari wameshamwandikia rais barua tangu mwezi wa saba kwa ajili ya kukutana naye.

Amesema  ‘’Sisi kama mashujaa tunataka kumuona Rais tumueleze matatizo lukuki ambayo tunayo na lengo ni kufuta machozi na taabu ambazo tulizopitia tangu muda huo’’amesema na kuongeza kwamba b

“Barua tumeandika kama chama kwa Rais Magufuli mwezi wa saba na habari njema ni kwamba ilijibiwa na kutuelekeza kupata viongozi ambao wataonana naye kwa ajili ya mazungumzo kuhusu kusaidiwa matakwa yetu amesema Lubala.