Waliosoma Jangwani walizwa na matokeo mabaya ya kidato cha sita

Muktasari:

  • Miongoni mwa waliofadhaishwa na matokeo hayo ni waliowahi kusoma sekondari kongwe ya wasichana ya Jangwani iliyopo jijini Dar es Salaam yenye takribani miaka 90.

Dar es Salaam. Matokeo ya kidato cha sita yaliyotolewa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), yamepokewa kwa mtazamo tofauti, baadhi ya wananchi wakiyafurahia na wengine kufadhaika.

Miongoni mwa waliofadhaishwa na matokeo hayo ni waliowahi kusoma sekondari kongwe ya wasichana ya Jangwani iliyopo jijini Dar es Salaam yenye takribani miaka 90.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1928 na jiwe la msingi liliwekwa Mei 28 mwaka huo na Gavana wa Kiingereza, Sir Donald Cameroon.

Kwa sasa Sekondari ya Jangwani ina wanafunzi zaidi ya 1,000.

Necta ilitangaza matokeo hayo na kuitaja shule hiyo kuwa miongoni mwa kumi zilizofanya vibaya katika matokeo hayo.

Shule nyingine zilizotajwa kushika mkia ni Forest Hill (Morogoro), Jang’ombe (Mjini Magharibi), St James Kilolo (Iringa) na White Lake ya Dar es Salaam.

Nyingine ni Aggrey (Mbeya), Nyailigamba (Kagera), Musoma Utalii (Mara), Ben Belle (Mjini Magharibi) na Golden Ridge (Geita).

Mwananchi lilizungumza na wanafunzi waliowahi kusoma Jangwani ambao walieleza masikitiko yao baada ya matokeo hayo mabaya.

Mmoja ya waliolizwa na matokeo hayo ni Jiang Alipo, mke wa mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda.

“Jangwani yetu imekumbwa na nini? What happened to our skirts (nini kimetokea kwa sketi zetu?). Siamini,” alisema Jiang akimaanisha sketi wanazovaa wanafunzi wa shule hiyo za rangi ya machungwa.

Alisema alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule hiyo kuanzia mwaka 1995 hadi 1998.

“Natamani kama nikiamka leo nikiwa na miaka 13, nikiambiwa nichague shule niichague Jangwani tena. Jangwani Girls, sketi zetu za machungwa zinaingia madoa. Njooni tuungane tuokoe shule yetu, njooni tutafute suluhisho.”

Sara Msuta, mkazi wa Morogoro aliyesoma shule hiyo kidato cha kwanza hadi cha nne (2001-2004), alisema, “imeniuma kwa sababu ni shule ambayo tulijisikia fahari kusoma, tulikuwa na ndoto kubwa tukitaka kusoma pale.”

Alisema matokeo hayo yanafifisha taswira ya Jangwani kuwa shule bora ya wasichana nchini. “Nimepigiwa simu na wenzangu niliosoma nao kila mmoja anashangaa, inasikitisha. Nadhani Serikali inatakiwa kufanya jambo ili kurudisha hadhi ya hii shule,” alisema Sara.

Mwanafunzi mwingine aliyewahi kusoma katika shule hiyo, Matrida Erick ambaye kwa sasa ni ofisa lishe wa Taasisi ya Tunajali iliyopo Morogoro, alisema ni ajabu shule iliyowahi kutoa viongozi wengi wanawake wakiwamo mawaziri kushika mkia katika mtihani wa kidato cha sita.

“Nimeumia jamani nisidanganye. Nimetamani hata kujificha niliposikia Jangwani imekuwa kati ya shule za mwisho. Kuna tatizo gani hapo shuleni? Najua sio wakati wa kulaumu lakini lazima (suala hili) lifanyiwe kazi kuirudisha shule hiyo kwenye ubora wake,” alisema.

Halima Makonganya aliyemaliza kidato cha nne mwaka 2011, alisema matokeo mabaya ya shule hiyo yanachangiwa na mambo mengi akiutaja miongoni mwayo kuwa ni uhaba wa walimu.

“Niliposikia Jangwani ni kati ya shule za mwisho niliumia hasa ukizingatia ukongwe na ubora wake. Nimetafakari nikagundua zipo sababu za matokeo hayo ambazo lazima tu zirekebishwe,” alisema.

Alisema pamoja na uhaba wa walimu, kushuka kwa nidhamu ya wanafunzi na kutojituma kwao kama ilivyokuwa kipindi chao kumechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa shule hiyo.

Marry Mpangala, mkazi wa Mwanza na mfanyabiashara aliyesoma shuleni hapo miaka ya 1990, alisema kilichosababisha kufanya vibaya ni mfumo wa elimu ambao unaendeshwa na Serikali.

“Hivi sasa shule za binafsi zimechukua nafasi kubwa sana. Watu wengi hasa wenye vipato vya juu wanapeleka watoto wao shule za binafsi wakiamini kwamba kuna mfumo mzuri wa elimu,” alisema.

Marry alisema Jangwani imekosa watu wa kuitetea kwa sababu wenye uwezo wa kufanya hivyo wamekimbizia watoto wao shule binafsi.

“Jangwani imetoa viongozi wengi sana na wakati huo tunasoma ilikuwa miongoni mwa shule bora ya wasichana ambayo ilikuwa inafanya vizuri, lakini matokeo haya yamenishtua kidogo. Kwa nini Jangwani?” alihoji Marry.

Alisema katika kipindi chao hata kupata nafasi ya kusoma Jangwani ilikuwa vigumu.

“Kama jitihada za makusudi hazitafanyika kuirejeshea hadhi yake ya zamani shule hii itabaki jina tu.”

Mwalimu wa Sekondari ya Ufundi Mtwara, Lucy Ismail alisema: “Nimeshtuka jana (juzi) baada ya kuona Shule ya Jangwani imekuwa katika kumi za mwisho, sikuamini. Nini kimeikumba shule hii?”

“Nilitegemea itakuwa katika shule kumi bora lakini haikuwa hivyo, jamani kwa nini Jangwani, wapo wapi mawaziri waliokuwa wanasomesha watoto wao huko? Ina maana hawaioni hii shule? Mbona imeshuka hadhi kiasi hicho?”

Lucy aliyemaliza kidato cha nne mwaka 1995, alisema wakati huo ilisifika kwa kutoa elimu bora na wanafunzi viongozi.

“Nakumbuka shule hii ilikuwa inasifika kuanzia ubora kielimu hadi miundombinu. Hata viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri na wabunge (walisoma hapo),” alisema.

Juzi, mwalimu mkuu wa Sekondari ya Jangwani, Geradine Mwaisenga hakutaka kuzungumzia matokeo hayo akieleza kuwa na wageni na ana mgonjwa hospitali.

Imeandikwa na Asna Kaniki, Tumaini Msowoya na Bakari Kiango.