Wanaosaka ajira hii inawahusu

Baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu hapa nchini

Muktasari:

Katibu wa sekretarieti hiyo, Xavier Daudi alitoa taarifa hiyo jana baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna utoaji wa ajira mpya 1,101 katika Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Dar es Salaam. Wakati wahitimu wengi wa vyuo nchini wakiendelea kutafuta kazi, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeendelea kutangaza kuwa ajira mpya serikalini zimesitishwa hadi uhakiki wa watumishi utakapokamilika.

Katibu wa sekretarieti hiyo, Xavier Daudi alitoa taarifa hiyo jana baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna utoaji wa ajira mpya 1,101 katika Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Daudi alisema Septemba 29 na 30 mwaka huu waliona tangazo hilo la upotoshaji kwenye mtandao wa Whatsapp na Facebook, likiwataka Watanzania wenye sifa na uwezo waombe nafasi hizo kwa waajiri ambao ni katibu mkuu wa wizara hiyo na mtendaji mkuu wa TFS.

“Mtu aliyeanzisha uzushi huo aliingia kwenye tovuti yetu na kuchukua tangazo la Julai 9, mwaka jana la Kiingereza na Kiswahili. Alilibadilisha tarehe tu za kutangaza, matangazo hayo yaliyokuwa yametolewa na taasisi hii (sekretarieti) kwa niaba ya TFS, wizara, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB),” alisema.