Friday, February 17, 2017

Watu 11 washikiliwa kwa kuiba kompyuta 12 za Chuo cha Utumishi

 

By Hawa Mathias, Mwananchi

Mbeya.  Polisi mkoani hapa  inawashikiliwa watu 11 akiwamo mlinzi wa Kampuni ya New Imara, (majina yanahifadhiwa) kwa tuhuma za kula njama na kuiba kompyuta 12 mali za Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya.

Kamanda wa polisi mkoa Dhahiri Kidavashari amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo kuwa  watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Kidavashari alisema kuwa kompyuta hizo zilikamatwa nyumbani kwa mwanamke (jina limehifadhiwa ) anayejihusisha na biashara ya pombe haramu aina ya  gongo katika Kata ya Nonde jijini hapa.

Alisema kuwa mara baada  polisi kupata taarifa waliweka mtego nyumbani kwa mwanamke huyo na ndipo walipofanikiwa kuwanasa  na baada ya kupekuwa walifanikiwa kukuta vitu mbalimbali vya wizi zikiwemo kompyuta 11  za chuo cha utumishi wa umma ambapo moja ilikuwa imeuzwa kwa bei ya Sh 20,000

-->