“Wenye wagonjwa wa akili waitwa Hospitali ya Bugando’

Picha na MAKTABA

Muktasari:

  • Ofisa Ustawi wa Jamii wa BMC, Gasper Gaudensi alisema wapo wagonjwa 11 ambao ndugu zao hawajulikani huku wengine wakiwa na zaidi ya miaka miwili hospitalini hapo.

Mwanza. Ndugu wenye wagonjwa wa akili katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza (BMC) wameombwa kwenda kuwachukua wagonjwa wao walioruhusiwa kutoka ili kuipunguzia hospitali mzigo na gharama za kuwatunza.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa BMC, Gasper Gaudensi alisema wapo wagonjwa 11 ambao ndugu zao hawajulikani huku wengine wakiwa na zaidi ya miaka miwili hospitalini hapo.

Aliwataja baadhi ya wagonjwa hao kuwa ni John Sahari, Wandiba Kakwaya, Sesi Shabani, Selestine Charles, Elias Manyabili, Sabina Arobati, Heriwekeza Benedofula, Pili Msemakweli na Rebeca Umoja.

“Inawezekana watu hawa (wagonjwa) walipotea hata ndugu zao hawajui walipo, tunaomba waje wawachukue. Hospitali inaingia gharama kuwatunza wagonjwa wasiokuwa na ndugu kwani inatumia Sh1.8 bilioni kwa mwaka,” alisema. Daktari Bingwa Afya ya Akili, Kiyeti Hauli alisema wodi ina uwezo wa kulaza wagonjwa 50 lakini kwa sasa wapo 71 hivyo kusababisha msongomano na kukosa sehemu ya kuwalaza.