Wito matumizi mazuri ya mitandao watolewa

Muktasari:

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbassi aliwasihi watumiaji mitandao kuitoitumia kuitusi Serikali, badala yake wajikite kunufaika nayo kimaendeleo.

Dodoma. Wito kwa vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii umetolewa huku wakitakiwa waitumie iwawezeshe kujikwamua kiuchumi na si kufanyia vitendo vya kihalifu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbassi aliwasihi watumiaji mitandao kuitoitumia kuitusi Serikali, badala yake wajikite kunufaika nayo kimaendeleo.

Dk Abbasi aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho ‘Uchumi wa Viwanda’ kilichotungwa na Yuda Kemincha, ambapo aliwasihi pia kutumia elimu waliyonayo kwa maendeleo ya nchi na kutoshinda mitandaoni kuitukana Serikali yao.

Hata hivyo, akizungumza jana wakati akiwajengea uwezo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kwenye semina ya stadi za maisha, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Green Hope Organisation, Manjale Makongoro alisema wataitumia mitandao hiyo kwa ajili ya kujiingizia kipato

Alisema wakiitumia vizuri mitandao ya kijamii wanaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa jamii inayowazunguka badala ya kuitumia kuangalia mambo yasiyofaa. Awali, Makongoro aliwataka vijana waliopo vyuoni na wale waliomaliza masomo kutumia elimu waliyoipata kujiajiri na si kutegemea ajira kutoka serikalini.

Baadhi ya wanafunzi waliopata elimu hiyo, walisema imewanufaisha maana walikuwa na fikra za kupata ajira serikalini baada ya kumaliza masomo yao.

Alex Ramadhani alisema kuwa vijana wengi wanaotoka vyuoni wanaweza kuitumia elimu waliyoipata kujiajiri hata kwa shughuli za kawaida na si lazima za ofisini.

Moreen Minja alisema kuwa amejifunza kujitathmini na kuwa na maono kwa jamii inayomzunguka na kwamba yuko tayari kujiari mwenyewe.

Meneja wa Vodacom Mkoa wa Dodoma, Balikulije Mchome ambao ndiyo wadhamini wa semina hiyo kupitia mfuko wao wa Vodacom Faoundation alisema wamekuwa wakitoa elimu hiyo ili kuwajengea uwezo vijana.