100 wakamatwa Uganda wakipinga kukamatwa kwa Bobi Wine

Muktasari:

Inadaiwa kuwa katika tukio hilo mtu mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa na polisi walikuwa wakizuia maandamano hayo.


Kampala,Uganda. Polisi nchini Uganda wamewakamata watu 103 waliokuwa wakiandamana kupinga kukamatwa kwa mbunge wa upinzani,  Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine pamoja na wabunge wengine kadhaa na wanaharakati nchini humo.

Inadaiwa kuwa katika tukio hilo mtu mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa na polisi walikuwa wakizuia maandamano hayo.

Waandamanaji hao waliwasha matairi ya magari, huku wakirusha mawe kwa askari hao waliokuwa wanawazuia.

Wanajeshi na polisi wakiwa katika magari walipita katikati ya mji wa Kampala huku sehemu nyingine za mji huo maofisa usalama walipita na kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji.

Taarifa zinazeleza kuwa mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki mashuruhi aliteswa akiwa mikononi mwa wanajeshi. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amekana madai kuwa Bobi Wine alijeruhiwa.