Bodi iliyovunjwa TBS yaeleza mazito

Muktasari:

“Pale TBS kuna matatizo makubwa mawili, kwanza wafanyakazi ni wachache, hivyo waliopo wanashindwa kufanya kazi ipasavyo kwa kuwa majukumu ya kazi ni mengi kuliko idadi ya wafanyakazi.”

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Oliver Mhaiki amesema walijua wazi kuwa Bodi hiyo itavunjwa kwa kuwa ilitoa maamuzi yaliyopingwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.

Bodi hiyo ilivunjwa juzi na Dk Kigoda huku akieleza kuwa lengo ni
kuweza  kutekeleza nia ya wizara hiyo ya kuboresha utendaji kazi wenye tija na ufanisi katika shirika hilo.

Alieleza kuwa Shirika hilo ni nyeti katika taifa,, hivyo ni lazima liimarishwe ili kuhakikisha inafanya kazi kama anavyotarajiwa na wananchi.
Bila kueleza maamuzi iliyoyatoa, Mhaiki aliliambia Mwananchi kuwa Dk Kigoda ameivunja bodi hiyo kwa sababu zake mwenyewe.
Bila  kuweka wazi mambo ambayo waliyapendekeza lakini yakapingwa na waziri huyo alisema, “Tulijua lazima ataivunja bodi na ndio maana wajumbe wa bodi hawakushangazwa na maamuzi aliyoyachukua.”

Alipoulizwa sababu za TBS kulalamikiwa na wadau mbalimbali kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake alisema, “Pale TBS kuna matatizo makubwa mawili, kwanza wafanyakazi ni wachache, hivyo waliopo wanashindwa kufanya kazi ipasavyo kwa kuwa majukumu ya kazi ni mengi kuliko idadi ya wafanyakazi.”

Alisema, “Pia TBS hakuna vitendea kazi vya kutosha jambo linalowafanya wafanyakazi washindwe kufanya kazi kikamirifu, haya matatizo ndio yanayolifanya shirika hili kulalamikiwa kila siku.”

Alisema kuwa mashirika ya Viwango la Kenya na Uganda yameizidi ubora TBS kwa asilimia 75 na kwamba hilo ndio suala ambalo bodi hiyo ilikuwa ikilifanyia kazi, lengo likiwa ni kuirejesha TBS katika ubora unaotakiwa.

Alipoulizwa kuwa kuna habari kuwa moja ya sababu ya kuvunjwa kwa bodi hiyo ni kutoa ripoti ya kumsafisha aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege alisema jambo hilo sio la kweli kwa maelezo kuwa uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo bado zinaendelea kufanyika.

“Hilo sio kweli kwa kuwa Ekelege alituhumiw na Kamati ya Bunge ambayo ilitaka ufanyike uchunguzi na CAG akatekeleza agizo hilo na kupeleka ripoti bungeni, sasa hapo tunausika kwa lipi” alisema Mhaiki
Ripoti yenyewe
Mei mwaka huu Bodi hiyo iliwahi kutoa ripoti iliyodaiwa   kumsafisha aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Charles Ekelege.

Mapema mwaka huu Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) ilitembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China na kubaini kuwa shirika hilo lina ofisi hewa.

Baada ya kurejea safari hiyo, kamati hiyo ilimlipua Ekelege bungeni ikitaka awajibishwe kwa sababu sio mkweli na kwamba fedha za ukaguzi zimekuwa zikiishia mifukoni mwa wajanja wachache.

Tuhuma hizo zilimfanya Dk Kigoda takribani miezi sita iliyopita  kuiagiza bodi hiyo kumsimamisha kazi  Ekelege ili kupisha uchunguzi.

Lakini siku chache baada ya Ekelege kusimamishwa kazi baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo walitembelea maeneo hayo na kueleza kuwa vituo vya ukaguzi vilikuwepo.
Ujumbe huo wa watu wanne ambao ulijumuisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Masharika ya Umma, Mahmoud Mgimwa ilifanya ziara hiyo katika nchi za Japan na China kuanzia Mei 6 hadi Mei 14 mwaka huu.

Rasimu ya ripoti ya Kamati hiyo ambayo Mwananchi inayo inaeleza kuwa ujumbe huo uliridhishwa na kazi nzuri ambayo inafanywa na mawakala wa TBS waliopo katika nchi mbalimbali ikiwamo Japan na China.

Wajumbe wengine waliokuwa katika msafara huo, Mhaiki, Mkurugenzi Mkuu wa TBS aliyeondolewa, Charles Ekelege, na Mdhibiti wa Ubora wa TBS, Kezia Mbwambo.
Mbali ya kutembelea Japan pia timu hiyo ilitembelea Uswisi na Ufaransa ambako walikagua kampuni zinazofanya kazi ya uwakala kwa niaba ya TBS katika maeneo hayo.

Ujumbe huo katika ripoti yake unaeleza wazi kuwa kila maeneo waliyotembelea walikutana na viongozi wa makampuni hayo na kutembelea karakana na maabara na kwamba walishuhudia kazi ya ukaguzi wa magari yaliyotumika ikifanyika kwa ufanisi.

Baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari yaliyotumika nchini Japan timu hiyo ilitoa maoni yake ikieleza kuridhishwa  utaratibu huo na kwamba unafaa kuendelea kwa manufaa ya nchi.

“Utaratibu wa kukagua ubora wa magari yaliyotumika kabla ya kuingia nchini ni mzuri kwa manufaa ya nchi na faida zake ni nyingi,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:

“Hivyo ni vyema ukaguzi wa magari yanayoingizwa  nchini kutoka nchi za nje uendelee kufanyika  katika maeneo husika. kwa kuwa vituo vya ukaguzi kwa niaba ya TBS viko katika nchi tatu kwa sasa yaani Japan, Uingereza na Dubai ni vyema kuongeza  wigo kuhakikisha huduma  hii ya ukaguzi wa magari yaliyotumika  kabla ya kusafirishwa kuja nchini inapatikana dunia nzima.”

Alipoulizwa kama ripoti hiyo ni moja ya chanzo cha kuvunjwa kwa Bodi hiyo alisema, “Hayo mambo yameshapita ndugu yangu tuachane nayo.”

Waliokuwa wa wajumbe wa bodi hiyo iliyovunjwa ni mwenyekiti wa bodi Oliver Mhaiki, Donald Chidomu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Rashidi Salimu kutoka wizara ya Viwanda Zanzibar, Dr Bertha Maegga kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Odilo Majengo kutoka wizara ya Viwanda na biashara.

Wengine ni Prof Ntengwa Mdoe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Peter Mahunde kutoka Shirika la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Mariki kutoka Tume ya Ushindani, Suzi Leizer kutoka shirikisho la mashirika madogo naya kati (SMEs) na Elpina Mlaki kutoka wizara ya Fedha.