Vurugu tupu Tanzania

Vijana wakazi wa Dumila na vitongo vyake wakiangusha gari aina ya Land Cruizer T 241 AMS mali ya mfugaji katika barabara kuu ya Dodoma-Morogoro wakati wa vurugu zilizodumu kwa masaa sita kwa kuweka vizuwizi kwa lengo la kumshinikiza mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bebdera kusikiliza kero za wakulima.Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

Mkoani Mororgoro mtu mmoja aliyefahamiwa kwa jina la Mohamed Msigara (60) amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kutokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji Kijiji cha Dumila, wila yani Kilosa, baada ya wafugaji wa Jamii ya Kimasai kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima yaliyo katika Kitongoji cha Mfulu, Kilosa.

MAENEO ya mikoa ya Morogoro, Mtwara na Dar es Salaam, jana yaligeuka uwanja wa fujo na vurugu zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi.

Vurugu hizo zimehusisha wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa upande mmoja wa Morogoro, Mtwara Mikindani wananchi waliizingira nyumba ya Diwani wa Kata ya Mikindani kwa madai ya kuwahifadhi watu wanaodaiwa kuwa washirikina ndani ya nyumba yake, huku Dar es Salaam eneo la Kariakoo, polisi na Wamachinga wakipambamba na Mgambo wa Jiji.

Mkoani Mororgoro mtu mmoja aliyefahamiwa kwa jina la Mohamed Msigara (60) amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kutokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji Kijiji cha Dumila, wila yani Kilosa, baada ya wafugaji wa Jamii ya Kimasai kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima yaliyo katika Kitongoji cha Mfulu, Kilosa.

Pamoja na mauaji hayo, wasafiri waliokuwa wakitumia Barabara ya Morogoro – Dodoma, nao walionja machungu ya vurugu hizo, baada ya kukwama kwa saa 5 kutokana na wananchi wa kijiji hicho, kufunga barabara kwa mawe, magogo ya miti na kuchoma magurudumu ya gari.

Wananchi hao walichukua hatua hiyo huku wakisisitiza kutaka kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, ili kumaliza mvutano huo.

Katika vurugu hizo wanakijiji hao walivunja vioo vya madirisha ya baadhi ya nyumba tano za kulala wageni, kuharibu gari dogo aina ya Landcruser pamoja na kupora mali mbalimbali zi nazodaiwa kumilikiwa na wafanyabiashara wa jamii ya Kimasai.

Kabla ya kufanya uharibifu huo saa 2:30 asubuhi, wananchi hao walifanya maandamano sambamba na kusimama katikati ya barabara, hali iliyosababisha polisi kufika eneo hilo kwa ajili ya kuwadhibiti.

Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU), walifika eneo la tukio 5:20 asubuhi na kufanikiwa kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia mabomu ya machozi, hatimaye kufungua barabara hiyo.

Pamoja na barabara hiyo ya Morogoro – Dodoma, wananchi hao pia walifunga barabara ya Dumila- Kilosa, hivyo kuyafanya magari yaliyokuwa yakitumia barabara hiyo kukwama kwa zaidi ya saa sita na kusababisha usumbufu kwa wasafiri waliokuwa wakitumia barabara hiyo.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, wafugaji wa jamii ya Kimasai wakiwamo wanawake na watoto walionekana kukimbilia kwenye kituo kidogo cha Polisi Dumila kwa lengo la kujihami na kupata msaada wa polisi kutokana na hofu ya kushambuliwa na wananchi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyekuwepo kwenye eneo la tukio, mkulima aliyefahamika kwa jina Mauya Hamadi alisema kuwa wananchi wamelazimika kufanya vurugu hizo baada ya wafugaji wa jamii ya Kimasai kuingiza mifugo kwenye mashamba ambayo tayari yameshapandwa mazao na kufanya uharibifu.

Alisema kuwa tayari suala hilo walishalifikisha kwa uongozi wa kijiji, kata, wilaya hadi mkoa, lakini hakuna jitihada zozote zinazofanywa na viongozi, hivyo kulazimika kumtaka Mkuu wa Mkoa Joel Bendera, kwenda kuzungumzia suala hilo, ambapo hata hivyo mkuu huyo wa mkoa hakuwahi kufika eneo hilo hadi walipoamua kufanya maandamano hayo.

“ Sisi tunaishi kwa kilimo na wao wanaishi kwa mifugo, sasa kwa nini wanaharibu mashamba na mazao yetu ambayo tunategemea kwa chakula na hata kujipatia kipato?” alisema Hamadi akihoji na kuongeza:

“Kwanza ukiwakuta shambani kwako wanakuwa jeuri na wakali kwa kweli, tumechoka, tunaomba mkuu achukue hatua kuhusu tatizo hili.”

Alisema kuwa eneo la Mabwegere ni la mashamba, lakini cha kushangaza hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alidai kuwa eneo hilo ni la wafugaji, jambo ambalo wakulima walilipinga na kumtaka Mkuu wa Mkoa kubainisha maeneo ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza na baada ya kuwasili eneo la tukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema kuwa tayari baadhi ya watu ambao idadi yake haikuweza kufahamika wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba bado askari wa FFU pamoja na makachero wengine wa jeshi hilo wanaendelea kufanya doria katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi na usalama hasa nyakati za usiku.

Akizungumza kwenye kikao na wananchi wa eneo hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, aliwataka wananchi hao waendelee na shughuli za kilimo, wakati suala hilo likiendelea kushughulikiwa ili kila upande uweze kuendesha shughuli zake kwa amani na usalama.

Habari zilitotufikia wakati tukienda mitamboni zinapasha kuwa baadaye malori matatu aina ya Fuso yalipakia watu wanaodaiwa kuwa ni wakulima yaliingia katika Kijiji cha Mabwegere na kujificha kwenye mapori kwa lengo la kufanya vurugu, kuharibu mali na kuwashambulia wafugaji wa jamii ya Kimasai.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwabwegere, Shariff Kisenga alisema kuwa amepata taarifa kuwa makundi ya wakulima wa Jamii ya Kikaguru kutoka Kijiji cha Idibo, Tarafa na Wilaya ya Gairo, yameingia kijijini hapo kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa wafugaji wa jamii ya Kimasai.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilosa, Emanuel Gariyamoshi alisema kuwa polisi wataendelea kufanya doria katika mji mdogo wa Dumila ambako ndiko zilikotokea vurugu na kwamba bado wanahitaji nguvu kubwa ya askari hasa wa FFU, ambao watasaidia kutuliza ghasia yoyote itakayojitokeza.

Mtwara

Kutoka Mtwara habari zinasema kuwa polisi jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wa Kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani, baada ya kuizingira nyumba ya Diwani wa kata hiyo, Mohamedi Chehako kwa madai kuwa alikuwa amewahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Maria Nzuki hakupatikana kupitia taarifa ya simu yake ya mkononi.

Habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliingilia kati vurugu hizo na kuanza kutembeza mkong’oto kwa wananchi kwa lengo la kuwatawanya.

Taarifa zinasema kuwa askari hao waliingilia tukio hilo baada ya mwenzao aliyekuwa akipita eneo hilo kujeruhiwa na kutoa taarifa kwa wenzake waliofika na kutembeza mkong’oto kwa wananchi hao.

Baada ya askari hao kuondoka, wananchi hao walifunga kwa mawe makubwa njia zote kutoka eneo la mahakama, ambapo polisi waliegesha magari yao, hivyo kuwafanya polisi washindwe kutoka eneo hilo na wao kupata upenyo wa kuendeleza vurugu na uharibifu.

Habari ziliongeza kwamba wananchi hao walichoma jengo la choo cha mahakama na kuichoma moto nyumba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na kuvunja vioo vya nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Mohammed Sinani.

Wananchi hao walivamia nyumba ya diwani huyo baada ya kukuta ‘ungo’ unaodaiwa kutumiwa na watu wanaodaiwa kuwa wachawi kutoka sehemu moja kwenda nyingine pamoja na tunguri katika uwanja wa diwani huyo maeneo ya Makaburi Msafa.

Baada ya kushuhudia vitu hivyo, wananchi hao walijikusanya nyumbani kwa diwani huyo na kumshinikiza awatoe nje wachawi hao ili waweze kuwaadhibu, amri iliyopingwa na diwani huyo.

Kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo wananchi walivyozidi kuongezeka, ambapo baadaye kuliibuka kundi jingine la watu walioanza kuizingira nyumba ya diwani huyo, kumfanya diwani huyo kuomba msaada polisi.

Mashuhuda wa tukio walieleza kwamba polisi walipofika waliwasihi wananchi kutawanyika kwa kuwa ungo na tunguri hizo zilikuwa zimeteketezwa kwa moto na diwani huyo mbele ya wananchi hao.

“Wananchi waliendelea kupinga na kudai ndani ya nyumba kuna rubani na abiria wa ndege (ungo) wamehifadhiwa, kuona hivyo polisi wakawachagua wananchi watano na kuingia ndani ya nyumba kuwasaka watu hao, lakini hawakuona kitu, walitoka nje na kuwaeleza wenzao ambao hata hivyo walikataa kuamini maneno yao,” alisema Mussa Chehako na kuongeza:

“Walianza kurusha mawe katika nyumba ile na kuwafanya polisi kujibu mapigo kwa kurusha mabomu ya machozi .”

Alisema kuwa ni kawada yake kuamka alfajiri kwa ajili ya sala ya asubuhi, lakini asubuhi ya jana alishindwa kuamka mapema, hata hivyo hakuweza kuhisi jambo lolote.

Katika mapambano hayo ya wananchi na polisi, wananchi kwa kutumia mawe wamemjeruhi kwa jiwe kichwani Mwandishi wa Habari wa Channel Ten mkoani hapa, John Kasembe ambapo alitibiwa Zahanati ya Fajima na anaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa Kasembe alipigwa mawe kichwani akiwa kazini kukusanya habari na wananchi waliokuwa wakiwarushia mawe polisi.

Ofisa wa Polisi ambaye jina lake hakutaka litajwe kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa gari moja ya polisi limevunjwa kioo cha mbele kwa mawe.

Hadi saa 10.00 jioni bado polisi walikuwa wanaendelea kupiga mabomu ya machozi hewani huku wananchi wakionekana kujipanga katika makundi hali iliyotishia usalama wa maeneo hayo.

Jijini Dar es Salaam, askari mgambo wawili wa Manispaa ya Ilala wamejeruhiwa vibaya jana, baada ya kutokea mapambano kati yao na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga eneo la Kariakoo.

Katika vurumai hizo, wanamgambo watano wametiwa mbaroni na polisi kwa madai kuwa ndiyo chanzo cha vurugu hizo.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Kipolisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi aliliambia gazeti hili jana kuwa, vurumai hizo zilitokea baada ya kutokea mzozo baina ya mgambo hao na polisi.

Alisema polisi walifika eneo hilo kuwakamata mgambo, ambao wanatuhumiwa kuwapiga Wamachinga katika Mtaa wa Agrey, juzi.

Minangi alisema kuwa juzi Wamachinga walipigwa na mgambo hao na kupoteza mali zao, hivyo wakaamua kwenda kushtaki polisi.

“Polisi walipopata malalamiko ya wamachinga hao walienda leo (jana), kuwasaka mgambo hao na walipokuwa wanataka kuwakamata, mgambo wenzao wakapinga wakisema; hapa hatoki mtu,” alisema Minangi.

Alifafanua kuwa katika kujibizana mgambo hao walikuja juu ambapo miongoni mwao walitaka kuwanyang’anya polisi silaha walizokuwa nazo.

Kamanda huyo alisema polisi walionekana kuzidiwa nguvu na mgambo hao, ndipo wamachinga wakaingilia kati na kuwapiga.

Alisema kuwa Wamachinga hao walionekana kuwa wengi na waliwaelemea mgambo hao kwa kuwashushia kipigo kama cha wezi.

Alieleza kuona hivyo, polisi waliokuwepo eneo hilo walijaribu kuwaokoa, lakini ikashindikana ambapo ilibidi wawapigie simu wenzao ili kutoa msaada.

Minangi alisema Polisi wengine walipofika, waliweza kurejesha amani eneo hilo na kuwaokoa mgambo hao ambao wawili walionekana kujeruhiwa.

“Kiukweli kama polisi wasingeongezeka, katika kuamua ugomvi huo, sasa tungekuwa tunaongea lugha nyingine (vifo),” alisema Minangi akielezea kuwa wangeweza kuuawa.

Taarifa ambazo gazeti hili lili zilizeleza kuwa mgambo wawili walijeruhiwa vibaya na walipelekwa katika hospitali ya Muhimbili kwa matibabu.

Imeandikwa na Juma Mtanda,Hamida Sharif Kilosa, Abdallah Bakari, Mtwara na Bakari Kiango, Dar