Kujeruhiwa kwa Kibanda kwaahirisha kesi
Muktasari:
“Mheshimiwa Hakimu tunaomba tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hii kutokana na mshtakiwa namba mbili kuvamiwa na watu ambao hawajafahamika na kisha kujeruhiwa
KESI inayomkabili aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Theophil Makunga na wenzake wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirishwa hadi Machi 26, mwaka huu kutokana na mshtakiwa namba mbili, Absalom Kibanda (45), kutofika mahakamani baada ya kujeruhiwa na watu wasiojulikana.
Wakili wa Serikali, Peter Maugo alidai mbele ya Hakimu Waliarwande Lema kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa upande wa ushahidi upande wa mashtaka.
“Mheshimiwa Hakimu tunaomba tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hii kutokana na mshtakiwa namba mbili kuvamiwa na watu ambao hawajafahamika na kisha kujeruhiwa ambapo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Makunga anadaiwa kufanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(a) cha sheria ya magazeti, sura ya 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kaganda alidai kuwa Novemba 30,2011 Makunga akikaimu nafasi hiyo alichapisha waraka wenye kichwa cha habari “Waraka maalumu kwa askari wote” ambao uliandikwa na Samson Mwigamba kwenye gazeti la Tanzania Daima toleo la 2553.