Mwanaharakati akimbia vitisho vya kuuawa

Mwanaharakati, Albanie Marcossy ambaye amekimbia makazi yake na kwenda mafichoni akidai anaogopa vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.

Dar es salaam. Mwanaharakati Albanie Marcossy, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Civil and Political Right Watch (CPW) ameondoka nyumbani kwake Kimara Dar es Slaam akidai kilichomwondoa ni kupokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.

Marcossy, awali aliwahi kufanya kazi kwenye Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) ambako alikuwa mmoja wa waliopeleka mashtaka  kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Septemba 28, 2012 dhidi ya serikali kutokana na mauaji yenye utata ya watu 23 akiwamo Mwandishi wa habari  Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.

Akizungumza  jana kutoka alikokimbilia,  Marcossy alisema ameamua kuikimbia nyumba yake kwa ajili ya usalama na kubainisha kuwa taarifa ya vitisho vyake aliwasilisha kwa Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD-Coalition,) Onesmo Olengurumwa.

Olengurumwa alithibitisha kupokea taarifa hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa jana alisema polisi hawana taarifa kuhusiana na kutoweka kwa mwanaharakati huyo wala kutishiwa kutokana na kutopokea taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo .