Uchaguzi wa Kamati za Bunge:Vita Lowassa,Membe yakolezwa

Benard Membe

Muktasari:

Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo kunaibua upya vita kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge jana ilitangaza majina ya wenyeviti na makamu wapya wa Kamati za Kudumu za Bunge huku Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo kunaibua upya vita kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Awali, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo iligawanywa hivi karibuni na kuzaliwa kamati mbili; ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Mambo ya Nje.

Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja, baada ya wabunge wote wa CCM kukutana katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi wa Karimjee na kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwachagua wenyeviti na makamu wa kamati hizo.

Habari za ndani kutoka katika kikao hicho zilieleza kuwa moja ya ajenda zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge kuwachagua wenyeviti kwa kufuata taratibu na utendaji wao wa kazi.

Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia Mwananchi Jumamosi kwamba kikao hicho ni cha kawaida na walikuwa wakijadiliana matatizo yaliyopo katika majimbo yao na jinsi ya kuyawasilisha serikalini.

Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu ambaye alikuwa makamu wa Lowassa kabla ya kugawanya kwa kamati hiyo, amechaguliwa tena kushika nafasi hiyo.

Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao ulifanyika jana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya ofisi ya Bunge kutaja majina ya kamati mpya 16 pamoja na wajumbe wake.

Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja tangu kumalizika kwa mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo wakati zimeundwa kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Ulinzi na Usalama.

Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo zinaeleza kuwa Zitto ambaye alikuwa akichuana na John Cheyo, alipata kura 13 kati ya 17 zilizopigwa na wajumbe wa kamati yake, hivyo Zitto sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

Mbunge wa Ludewa, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe, amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa PAC.

Kushindwa kwa Cheyo kulianza kuonekana mapema kutokana na Zitto, ambaye alilalamikia kitendo cha kuvunjwa kwa kamati ya POAC, kuanza kampeni za chinichini ili kumtoa Cheyo, ambaye ameshikilia nafasi ya uenyekiti wa PAC tangu mwaka 2005.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel aliwataja walioshinda kuwa ni Mohamed Mgimwa ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ambapo makamu wake ni Luke Kitandula.

Alisema Kamati ya Bajeti, mwenyekiti wake ameteuliwa na Spika Anne Makinda kuwa ni Andrew Chenge katika utaratibu ambao haufanani na wa kamati nyingine.

Hata hivyo, alisema kwa upande wa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo atachaguliwa na wajumbe wa kamati kama ilivyo kwa kamati nyingine.

“Kwa leo (jana) uchaguzi wa makamu mwenyekiti umefanyika, lakini kura zikawa sawa hivyo makamu hakupatikana, hivyo uamuzi umefikiwa kuwa uchaguzi huo utarudiwa Jumatatu ijayo,” alisema Joel.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) amekuwa Rajab Mbarouk Mohammed na makamu wake ni Suleiman Zedi,” alisema Joel.

Awali, mwenyekiti wa LAAC alikuwa mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema ambaye katika uteuzi mpya amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Kwa upande wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, aliyekuwa makamu wake, Iddi Azzan amebwagwa katika uchaguzi huo, sasa ni mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi.

Joel alisema Margareth Sitta amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na makamu wake ni Stephen Ngonyani.Wengine waliochaguliwa ni Jenister Mhagama ambaye anakuwa Mwenyekiti Kamati ya Maendeleo ya Jamii na makamu wake ni Saidi Mtanda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ni Victor Mwambalasa na makamu wake ni Jerome Bwanausi. James Lembeli amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na makamu wake ni Abdulkarim Shah.

Peter Serukamba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu na makamu wake ni Profesa Juma Kapuya. Hamisi Kigwangalla amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na makamu wake ni John Lwanji.

Kamati ya Masuala ya Ukimwi mwenyekiti ni Lediana Mng’ong’o, makamu wake ni Diana Chilolo.

Anna Abdallah amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na makamu wake ni Mohammed Seif Khatib,.Pindi Chana amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, makamu wake ni William Ngeleja.

Kamati ya Maadili mwenyekiti ni Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi na makamu wake ni John Chiligati na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji mwenyekiti wake ni Profesa Peter Msolwa na makamu wake ni Said Nkumba.