‘Afya ya Lwakatare tete’

Mkuu wa Usalama na Ulinzi wa Chadema, Wilfred Lwakatare

Muktasari:

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakili Kicheere alisema amehangaika sana katika kuhakikisha kuwa mteja wake anapata dhamana lakini imeshindikana, hali ambayo inamtia hofu kutokana na hali aliyomwona nayo.

Dar es Salaam. Hali ya afya ya Mkuu wa Usalama na Ulinzi wa Chadema, Wilfred Lwakatare anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwahamasisha watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia mitandao ya jamii, imezorota.

Gazeti hili imemshududia jana akizungumza na wakili wake Nyaronyo Kicheere, huku akilalamikia hali yake kuwa si njema kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao.

Alikuwa akitembea kwa kujivuta, na alidai kuwa ameshindwa kula chakula inavyotakiwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakili Kicheere alisema amehangaika sana katika kuhakikisha kuwa mteja wake anapata dhamana lakini imeshindikana, hali ambayo inamtia hofu kutokana na hali aliyomwona nayo.

“Mteja wangu ni mgonjwa wa kisukari, kwa kawaida hutakiwa kula chakula na kunywa maji mengi, lakini nimehangaika sana, leo (jana) nilikuwa na matumaini kwamba atapelekwa mahakamani ambapo nilijipanga kwa kuandaa watu makini wenye hati za nyumba nikiwa na imani kwamba angepata dhamana, lakini wamemrudisha mahabusu,” alisema Kicheere.

Kicheere muda mwingi alionekana kuhaha kuwasiliana na viongozi wa Chadema kwa simu yake ya mkononi, pamoja na kuwasiliana na baadhi ya wanasheria akiwamo Tundu Lissu na Peter Kibatala ambao walijipanga katika kuhakikisha kuwa wanapata wadhamini watakaoweza kumdhamini Lwakatare.

Wakili huyo alisema kuwa kinachotendeka kwa mteja wake ni kinyume cha sheria kwa kuwa ni tuhuma ndizo zimemfanya akamatwe.

Alisema mteja wake ana haki ya kupewa dhamana hasa kwa kuzingatia kuwa saa zaidi ya 24 zimepita na hali yake si njema, na kwamba kuendelea kuwa mahabusu ni kuhatarisha usalama wa afya yake.

Maofisa wa juu kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelelezi wa Makosa ya Jinai, waliwasili Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam ambapo walikutana na wakili Kicheere na mtuhumiwa huyo na kufanya mazungumzo.

Taarifa za kuaminika zilizopatikana awali zilieleza kuwa juzi saa 11 jioni maofisa kadhaa wa polisi, walimchukua mtuhumiwa huyo na kwenda naye nyumbani kwake wakiwa na lengo la kufanya upekuzi kwa mara ya pili lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya kutokuwa na kibali cha upekuzi.

“Wakili wake anawabana maofisa wa polisi akitaka wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria hivyo juzi hawakuweza kuingia ndani, pia walizuiwa na wakili huyo huyo kumhoji kwa kumrekodi kwa video, ambapo kulitokea hali ya majibishano ya kisheria, lakini hatimaye akahojiwa bila kurekodiwa,” kilieleza chanzo cha habari.

Lwakatare alikamatwa Jumatano ya wiki hii katika makao makuu ya chama hicho na tangu siku hiyo anaendelea kushikiliwa na polisi kwa mahojiano.