Katibu Chadema awaponda Usalama wa Taifa

Muktasari:

“Enzi za Nyerere kulikuwa na Usalama wa Taifa wa kweli. Ulikuwa ukiwaza tu kufanya jambo fulani tayari umedakwa, sasa hivi makundi ya kimafya yanajiimarisha nchini, ni jambo la hatari sana,”

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimependekeza kusukwa upya kwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa madai kuwa, imezidiwa mbinu na makundi ya kimafya.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alipokuwa akizungumza na gazeti hili kutokana na matukio ya kutisha ya kutekwa na kuteswa kwa watu mbalimbali nchini.

Lema alisema Idara ya Usalama wa Taifa ya wakati wa  utawala wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, ilifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa kuliko ilivyo  sasa.

alisema.

Lema alisema matukio ya kutekwa nyara na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari, Dk Steven Ulimboka na wa Jukwaa la Wahariri, Absolom Kibanda yasingeweza kutokea enzi za Mwalimu Nyerere.

“Kwanza nalaani sana tukio hili la Kibanda na mimi nasema vyombo vyetu vya usalama visipoimarisha vitengo vya Intelijensia vitajikuta vikishindwa kuzuia makosa,” alisema Lema.

Alisema Usalama wa Taifa unapaswa kufanya kazi kama CIA ya Martekani  inayobaini mipango ya uhalifu kabla haijatendeka.“Leo hii wahamiaji haramu wanaingia nchini kila siku kana kwamba hatuna Intelijensia… watu wanatekwa na kuteswa…viongozi wa dini wanauawa? Usalama wa Taifa uko wapi,” alihoji Lema.

Lema alisema enzi za Nyerere ilikuwa vigumu kumfahamu nani ni Usalama wa Taifa hali iliyowasaidia kujichanganya.