Mahakama Kuu yaitisha mafaili kesi ya Lwakatare

Wilfred Lwakatare

Muktasari:

Mawakili hao wanadai kuwa uamuzi huo ambao ulihusu dhamana ya watuhumiwa, ulitenguliwa na hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka washtakiwa hao, isivyo halali.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeiamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwasilishe majalada ya kesi ya ugaidi inayomuhusu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake katika kesi hiyo, Ludovick Joseph.

Hati ya kuitisha majalada hayo ilitolewa jana alasiri na Msajili wa Mahakama Kuu, baada ya mawakili wanaomtetea Lwakatare kuwasilisha maombi ya marejeo ya mwenendo wa kesi hiyo, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu.

Maombi hayo ya marejeo yaliwasilishwa mahakamani hapo jana chini ya hati ya dharura yakiambatanishwa na hati kiapo ya mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare, Peter Kibatala. Wengine ni Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu.

Habari ambazo gazeti hili lilizipata kisha baadaye kuthibitishwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare zilisema kuwa jana Msajili wa Mahakama Kuu alisaini na kutoa hati hiyo kwenda Mahakama ya Kisutu.

Mapema jana mawakili wanaomtetea Lwakatare waliwasilisha maombi hayo ambayo yalipokewa na kupewa usajili wa namba 14 ya 2013.

Mawakili hao wanaiomba Mahakama Kuu, iitishe majalada yote mawili ya kesi hiyo, jalada namba 37 ya mwaka 2013 na namba 6 ya mwaka 2013 kwa ajili ya uchunguzi ili iweze kujiridhisha usahihi na uhalali wa mwenendo wake.

Pia wanaiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo na/au kutengeua hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyowafutia mashtaka watoa maombi (Nolle Prosequi) kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayohayo.

Maombi yao mengine ni kutaka Mahakama ya Kisutu iamriwe kutoa uamuzi wa maombi ya dhamana, uliokuwa umepangwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emillius Mchauru, Machi 20, 2013, katika kesi namba 37.

Mawakili hao wanadai kuwa uamuzi huo ambao ulihusu dhamana ya watuhumiwa, ulitenguliwa na hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka washtakiwa hao, isivyo halali.

Maombi mengine ni kurejea na/ au kutengua mwenendo wa kesi namba 6 iliyofunguliwa baada ya hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi hao na badala yake iendelee kesi namba 37.

Wanaiomba pia Mahakama Kuu iamue kwamba utaratibu uliotumiwa na wajibu maombi (Jamhuri) kutoa hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi katika kesi namba 37 ilikuwa kinyume cha sheria na/ au haukuwa sahihi.

Wanadai kuwa utaratibu huo ulisababisha matumizi mabaya ya taratibu za kimahakama na matumizi mabaya ya mamlaka ya kiuendeshaji mashtaka na kushusha hadhi na uhuru wa mahakama.

Chimbuko la rufaa

Lwakatare na mwenzake, Ludovick wanakabiliwa na mashtaka manne ya ugaidi wakidaiwa kula njama na kufanya mipango ya kumteka na kisha kumdhuru kwa sumu Dennis Msacky, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Mwananchi.