Bunge: Hatutazuia Tv kurusha vikao‘laivu’

Watangazaji wa TBC wakirusha matangazo ya bunge moja kwa moja kutoka Dodoma.

Muktasari:

Wakati Bunge likieleza kuwa haliwezi kuzuia vituo vya televisheni nchini kuonyesha moja kwa moja matangazo ya shughuli za vikao vya Bunge, Serikali imetoa sababu tatu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupunguza matangazo hayo ya shughuli za chombo hicho chenye mamlaka ya kutunga sheria.

Dodoma. Wakati Bunge likieleza kuwa haliwezi kuzuia vituo vya televisheni nchini kuonyesha moja kwa moja matangazo ya shughuli za vikao vya Bunge, Serikali imetoa sababu tatu za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupunguza matangazo hayo ya shughuli za chombo hicho chenye mamlaka ya kutunga sheria.

Uamuzi wa Serikali kuhusu TBC ulizua sintofahamu bungeni na kusababisha polisi kutumika kuwatoa katika Ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani waliokuwa wakishinikiza kusitishwa kwa mjadala wa hotuba ya Rais John Magufuli, badala yake lijadiliwe suala hilo la shirika hilo.

Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema jana kuwa hakuna televisheni yenye mkataba na Bunge kurusha moja kwa moja matangazo hayo, zote zinazorusha zinatumia gharama zao wenyewe.

Baada ya TBC kupunguza matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge, televisheni zilizobaki ambazo zinarusha moja kwa moja matangazo hayo, ni Star TV kupitia chaneli yake ya Star Bunge pamoja na Azam TV. “Sisi hatuna mkataba nao, wao wanarusha kwa gharama zao na Bunge haliwezi kuwazuia, labda waulizwe wenyewe kama wataendelea kurusha matangazo hayo ama laa,” alisema Joel huku akisisitiza kuwa hakuna zuio lolote.

Juzi jioni Waziri wa Habari, Nape Nnauye alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kueleza sababu tatu za kupunguzwa kwa matangazo hayo.

Nape aliitaja sababu ya kwanza kuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji, “Kwa mwaka TBC ilikuwa inatumia Sh4.2 bilioni kurusha moja kwa moja matangazo haya. Fedha hizi hazilipwi na Bunge wala Serikali, zinatokana na matangazo madogo ya TBC, sasa pia hesabu tangu 2005 mpaka sasa zimetumika kiasi gasi.”

Alisema sababu nyingine ya kupunguza kurushwa kwa Bunge ni kutaka wafanyakazi wa Serikali kufanya kazi kikamilifu, kwa madai kuwa wengi badala ya kufanya kazi walikuwa wakifuatilia vipindi hivyo.

Alisema utafiti uliofanywa na Serikali umebaini kuwa waendesha bodaboda, mamalishe, wamachinga, wakulima, wafugaji na watu wenye shughuli nyingi wanashindwa kufuatilia vipindi vya Bunge asubuhi na mchana kutokana na kubanwa na shughuli zao.

Kwa upande mwingine, Chadema imepinga TBC kusitisha kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya Bunge kikisema hiyo ni mbinu ya Serikali kuficha maovu yanayofanywa na baadhi ya viongozi wake.

Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu alisema sababu za kuwapo kwa gharama kubwa za matangazo hayo hazina msingi.

“Nape atueleze amezikokotoa vipi gharama hizo kwa sababu mimi ni mwana habari niliyefanya kazi katika televisheni, nafahamu gharama haziwezi kuwa kubwa kiasi hicho,” alisema Mwalimu aliyewahi kuwa mtangazani wa Channel Ten.

 

Tamwa wanena

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga alisema anaungana na Watanzania kupinga uamuzi huo wa Serikali na kuwataka watawala kufikiria upya uamuzi huo.

Edda alisema matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ni kipindi pekee ambacho wananchi wanapata fursa ya kuwasikia na kuwaona wawakilishi wao wakitoa hoja.

 

Misa-Tan

Naye Rais wa Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Misa Tanzania (Misa-Tan), Simon Berege alisema taasisi yake inapinga uamuzi huo wa Serikali kwasababu unaminya uhuru wa wananchi kupata taarifa ambayo haijachunjwa chunjwa.

“Ukiwanyima wananchi kupata taarifa za moja kwa moja na za uhakika, utawalazimisha kuzitafuta kila mahali na kusababisha wapate taarifa zisizo sahihi na hapo wanaweza kupotoshwa kirahisi,” alisema.

*Imeandikwa na Fidelis Butahe, Joyce Mmasi, Raymond Kaminyoge na Bakari Kiango.