Monday, October 16, 2017

Duru ya pili kuamua urais wa Weah Liberia

 

Monrovia, Liberia. Sasa ni dhahiri kwamba mwanasoka nyota wa zamani wa Liberia George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai watachuana katika duru ya pili ya kuwania urais Novemba 7.

Wagombea wawili hao watapambana katika hatua hiyo baada ya kila mmoja kukosa asilimia 50 jumlisha moja zinazohitajika kwa mshindi kutangazwa kuwa rais.

Baada ya kuhesabiwa asilimia 95.6 ya kura 1,550,923 zilizopigwa Oktoba 10, Weah wa muungano uitwao Coalition for Democratic Change (CDC) anaongoza baada ya kupata kura 572,453 sawa na asilimia 39.0 akifuatiwa na  Boakai wa Unity Party (UP) kwenye kura 427,550 sawa na asilimia 29.1.

Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo tangu baada ya uchaguzi wa vyama vingi kurejeshwa Waliberia kumpata rais kwa uchaguzi wa kidemokrasia. Pia, itakuwa mara ya tatu kwa Weah kuwania urais tangu Liberia irejee kwenye utulivu mwaka 2003 baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 14.

Kwa mujibu wa Katiba ya Liberia, Rais na Makamu wa Rais lazima wapate kura za kutosha ili kushinda. Kura hizo nyingi inamaanisha asilimia 50+1 ya kura zote halali.

Ikiwa hakuna mgombea atakayepata kura nyingi zaidi ya nusu, ndipo uchaguzi wa marudio unaandaliwa kwa wagombea wawili wa kwanza kuamua mshindi. Hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 83 (b) ya Katiba inayoilazimisha sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuandaa uchaguzi wa duru ya pili.

Katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea 20 walijitokeza huku Cllr. Charles Walker Brumskine wa Liberty Party (LP) akishika nafasi ya tatu baada ya kukujikusanyia kura 144,359 sawa na asilimia 9.8.

 

Monday, October 16, 2017

Uhuru, Ruto waonya mataifa ya kigeni

 

Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto wametoa onyo kali kwa mataifa ya nje wakiyashutumu kwa kujaribu kuingilia mambo ya ndani ya Kenya.

Wakizungumza wakati wa mikutano ya kampeni za kisiasa wakiwa Nyahururu na Karatina, viongozi hao walisema nchi haikuwa katika mgogoro wowote hata kustahili kuingiliwa kati na mataifa ya kigeni.

“Nataka kuiambia Jumuia ya kimataifa kwamba Kenya hakuna tatizo. Tatizo pekee tulilonalo ni mtu mmoja anayeitwa Raila Odinga (kiongozi wa Nasa),” alisema Rais Kenyatta.

Mkuu huyo wa nchi alisema nchi yake haitaruhusu mazungumzo kati yake na Odinga yatakayoongozwa na mataifa ya kigeni.

Huku akisisitiza kuwa Kenya ni nchi huru alisema: “Hatutaruhusu wazungu kuja na kutuambia nini cha kufanya. Kama watakuja Kenya, waacheni waje kama watalii. Waacheni waende Wamasai Mara, waje Laikipia na maeneo mengine, lakini wasije hapa na kutuambia nini cha kufanya,” alisema Rais Kenyatta.

Pia alimlaumu Odinga kwa maandamano na uharibifu wa mali katika maeneo mbalimbai ya nchi, akisema mtu yeyote aliyeshiriki katika maandamano lazima ashughulikiwe ipasavyo. Rais aliwaomba wapigakura nchini kujitokeza kwa idadi kubwa ili kupigakura zao kwenye uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26. 

Aidha, Makamu wa Rauis Ruto alimshutumu Odinga kwa kuiomba Jumuia ya Kimataifa kulazimisha mazungumzo ya upatanishi kwa lengo la kuunda Serikali ya Muungano.

“Analialia mbele ya mataifa ya kigeni ili yamuonee huruma na iundwe timu ya kusimamia upatanishi. Lakini hata kama atakwenda Ulaya, Washington apite hadi Mexico au arudi Casablanca, haitakuwepo Serikali ya Nusu Mkate,” alisema Ruto.

Ruto amemtaka Odinga kusitisha maandamano, kuacha uchokozi na vitisho dhidi ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tume Ezra Chiloba na akamtaka ajiandae kwa uchaguzi.

“Kama Jubilee tungetaka kumwapisha Kenyatta kuwa Rais, tungekwisha fanya hivyo, lakini kamwe hatukutaka kuingiza nchi katika machafuko kwa sababu sisi ni wapenda amani. Hivyo tuliamua kurudi kupigakura. Hivyo naye pia asitishe maandamano, aache maonyesho na ajiandae kwa uchaguzi,” alisema Ruto

Akizungumza katika mkutano wa kampeni Karatina, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa suala la kugawana madaraka na wapinzani halipo.

Pia aliwatetea polisi kutokana na madai ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakiandamana dhidi yaIEBC.

Katiba inaruhusu maandamano yenye amani, lakini huwezi kuita maandamano ya amani wakati unawatuma watu wako kurushia mawe vituo vya polisi. Unatarajia kupata nini pale unapokirushia mawe kituo cha polisi?”alihoji rais.

Monday, October 16, 2017

Familia ya mpinzani yakana kukutwa na silaha hatari

 

Abia, Nigeria. Familia ya kiongozi anayedaiwa kuhamasisha jimbo kujitenga, Nnamdi Kanu imetupilia mbali madai yaliyotolewa na Kamishna wa Polisi wa Abia, Anthony Ogbizi kwamba jeshi hilo lilikamata silaha hatari kutoka makazi yake.

Kamishna huyo alitoa taarifa akisema walikamata silaha walipovamia makazi ya kiongozi huyo yaliyoko Afara Ukwu kwa ushirikiano na Jeshi Oktoba 8.

Lakini Emmanuel Kanu, msemaji wa familia hiyo amewaambia waandishi wa habari kwamba ikiwa kuna silaha zilikamatwa kwenye makazi ya ndugu yao basi zitakuwa zilitegeshwa na vyombo vya usalama.

Alimshutumu Ogbizi kwa kutunga hadithi ili kuhalalisha “uvamizi haramu” ili ionekane alikuwa akitekeleza majukumu yake, limesema gazeti la The Nation.

"Huyu Kamishna wa Polisi mpya ni mtu yuleyule aliyekuja nyumbani kwetu siku mbili baada ya uvamizi uliofanywa Septemba 14 akiwa na magari mawili aina ya Hilux na Prado SUV akavunja kibaraza cha kuegesha magari na akaharibu magari yaliyokuwa yameegeshwa.

"Ni Kamishna huyu huyo ambaye haraka haraka baada ya uvamizi wa Oktoba 8, alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari  akiuambia ulimwengu mzima kuwa wamegundua mabomu kwenye nyumba yangu. Jeshi kwa upande mwingine lilikanusha likisema hakuna uvamizi uliofanyika kwamba halikuwahi kuja nyumbani kwangu.

"Nyumba ambayo haikuwa na mtu ndani ispokuwa mlinzi aliyepewa kazi ya kuitunza, ghafla waliivamia na ndipo wakaja na habari hiyo kwamba walikuta bunduki, bunduki ya mitutu miwili na bomu la petrol. Nani aliyetengeneza? Nani aliyeweka? Hayo ndiyo maswali ya kujiuliza."

 

Monday, October 16, 2017

Vifo shambulizi ya al-Shabab vyafika 300

 

Mogadishu, Somalia. Idadi ya watu waliouawa katika mlipuko mkubwa wa bomu Jumamosi iliyopita katika eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara mjini hapa imefikia watu 300 huku wengine 300 wakiwa majeruhi.

Rais Mohamed Abdullahi "Farmajo" Mohamed alilaumu kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-Qaeda kwa kuhusika na shambulizi hilo baya zaidi kutokea nchini tangu kundi la al-Shabab lilipoanzisha harakati zake mwaka 2007.

"Tumethibitisha kuwa watu 300 waliuawa kwenye mlipuko huo. Idadi ya watu waliokufa huenda bado ikaongezeka kwa kuwa bado wengi hawajulikani waliko," Abdikadir Abdirahman, mkurugenzi wa idara ya magari ya kusafirisha wagonjwa aliliambia shiria la Reuters.

Mashirika ya habari ya kimataifa yameripoti kuwa mkasa huo ulitokea wakati lori lililokuwa limejazwa milipuko lilipolipuka karibu na lango la hoteli.

Shirika la habari la Reuters lilimnukuu Ahmed Ali, muuguzi anayefanya kazi kwenye hospitali moja akisema kuwa miili 160 haikuweza kutambuliwa kwa kuwa ilichomeka vibaya hivyo ilizikwa na serikali jana na miili mingine iliziwa na jamaa zao.

Wafanyakazi wa idara ya afya wanahangaika kutambua na kutibu majeruhi wa shambulizi hilo la kikatili zaidi kwani watu 100 hawajulini walipo.

Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezekana kwani wengi inaaminika wamefukiwa kwenye vifusi vya jingo hilo lililoharibiwa.

"Tunatarajia idadi ya vifo itaongezeka," alisema Abdirahman Omar Osman akiongeza kwamba wafanyakazi wa uokozi wanahitaji msaada kwa sababu vifaa walivyonavyo haviwezi kuondoa kifusi.

"Bado tunaendelea kukusanya habari kutoka hospitali mbalimbali na ndugu wa marehemu. Wengine wamefikishwa hospitani wakiwa na majeraka makubwa. Pia tumearifiwa kuna ndugu wengine wanawaondoa hospitalini jamaa zao majeruhi,” aliongeza.

"Baadhi ya majeruhi wanahitaji uangalizi maalumu kwa vile hawawezi kutibiwa hapa. Wengi watasafirishwa leo kwenda Uturuki baada ya kuitikia ombi letu la  msaada," alisema Osman.

Alisema timu ya madaktari kutoka Uturuki ikiongozwa na Waziri wa Afya, Ahmet Demircan wamewasili leo asubuhi mjini Mogadishu kwa ajili ya kusaidia kusafirisha watu zaidi ya 70 wanaohitaji matibabu ya ziada.

 

Monday, October 16, 2017

Viongozi NRM wakataa kututwa ukomo wa rais

 

Kampala, Uganda. Viongozi wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) mjini Buzaaya, Wilaya ya Kamuli mwishoni mwa wiki walipiga kura kupinga kufutwa ukomo wa umri wa rais kwenye Katiba.

Msimamo huo umekuja baada ya baraza la wazee kusema wabunge wanaoshinikiza marekebisho ya Katiba ili kuondoa ukomo wa umri wa rais wanafanya hivyo ili kumfurahisha mtu mmoja tu.

Jukwaa la wazee hao limemkumbusha Rais Museveni ambaye atakuwa na umri wa miaka 77 ifikapo mwaka 2021 atakapokuwa anamalizi muhula wa sasa kwamba “muda umefika kwa yeye kupumzika ili kizazi kipya kichukue kuanzia alipoishia” na kuiendeleza nchi.

Kikao cha NRM

Uamuzi huo ulifikiwa na viongozi hao katika kikao cha kuomba ushauri wao kilichoandaliwa Jumamosi na mbunge wa Buzaaya, Isaac Musumba na kufanyika kwenye Chuo cha Ufundi cha Nawanyago.

Kikao hicho kililenga kupata maoni kutoka kwa wafuasi kindakindaki wa NRM kwa lengo la kuweka uzito katika marekebisho ya Katiba ambayo baadhi ya Waganda wanaona ni mkakati wa kumsafishia njia Rais Yoweri Museveni, 73, kuwania urais mwaka 2021 atakapokuwa na miaka 77.

Kikao hicho kilibadilika na kuwa cha mvutano wakati viongozi wa chama katika eneo hilo walipokuwa wanajaribu kuwazuia baadhi ya wanachama kufika eneo la kikao. Baadhi ya wanachama waliozuiwa kuingia kwenye kikao hicho walitishia kujiunga na vyama vya upinzani kwa maelezo NRM imeamua kuwaacha “yatima”

Ikiwa Katiba haitafanyiwa marekebisho, Rais Museveni hatakuwa na sifa ya kuwania kwa sababu ukomo wa umri kwa wagombea urais ni miaka 75.

“Rais Museveni alikwenda msituni kupambana dhidi ya madikteta waliong’ang’ania madarakani na aliahidi kurejesha demokrasia. Sasa anaathiriwa na mabadiliko ya msingi aliyoyafanya. Ni vema akijijengea heshima na urithi uliotukuka kwa chama cha NRM,” alisema Hamis Dheyongera, diwani wa Wankole (NRM).

 

Saturday, February 18, 2017

Walanguzi Mexico watumia manati kuingiza dawa za kulevya Marekani

Manati hii ambayo ni mfano wa ndogo

Manati hii ambayo ni mfano wa ndogo zinazotumiwa na watoto ilifunguliwa kwa kukata kwa umeme kutoka mahali ilipochomelewa mahsusi kwenye ukuta kwa ajili ya kurusha dawa kuingia ndani ya Marekani. 

Arizona, Marekani.Walanguzi wa dawa za kulevya nchini Mexico wamebuni njia mpya ya kusafirisha hadi Marekani kwa kutumia manati kubwa yaliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kurusha mihadarati hiyo.

Haijafahamika njia hiyo imetumika kwa muda gani, lakini iligunduliwa wiki hii na maofisa wa Marekani waliokuwa wanalinda doria.

Manati, ambayo ni njia ya kienyeji kabisa ilikuwa imefungwa kwenye ua ulio kwenye mpaka wa taifa hilo na Mexico na imekuwa ikitumiwa na walanguzi wa dawa za kulevya kurusha dawa hizo hadi ndani ya Marekani ambako kundi jingine huchukua.

Kugundulika kwa manati hiyo ya aina yake ni mafanikio mengine kwa Marekani ambayo imekuwa ikikabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya na wahamiaji kutoka Mexico.

Rais Donald Trump ameahidi kujenga ukuta mrefu kuzuia wahamiaji na walanguzi wa mihadarati kuingia Marekani, lakini wamekuwa wakirusha dawa kupitia ukuta uliopo.

Habari zinasema manati hiyo iligunduliwa na maofisa hao kusini mashariki mwa Tucson, Arizona, wiki iliyopita.

Maofisa hao walisema waliwaona wanaume kadhaa wakitawanyika na kutoroka walipokuwa wanakaribia eneo husika.

Baada ya kufanya ukaguzi katika eneo hilo, maofisa hao  waligundua vifurushi viwili vya bangi vilivyokuwa na uzito wa kilo 21 vikiwa havijapakiwa na kurushwa na manati hiyo iliyobomolewa.

Ukuta

Hadi sasa umejengwa ukuta katika mpaka wa Mexico na Marekani umbali wa kilomita 1,770. Pamoja na mikakati ya Trump kutaka kujenga ukuta mrefu, walanguzi wamekuwa wakitumia mbinu tofauti kusafirisha dawa za kulevya hadi Marekani bila kukamatwa.

Njia nyingine zinazotumiwa ni kusafirisha kwa ndege ndogo zisizo na rubani na wakati mwingine kuchimba njia za chini kwa chini zinazofika hadi Marekani.

Machi mwaka jana, maofisa wa Marekani waligundua njia ya chini kwa chini ya umbali wa mita 380 kutoka kwenye mgahawa mmoja Mexico hadi kwenye jumba moja lililopo California.

Januari mwaka huu, maofisa waliokuwa wanafanya doria eneo la Pharr, Texas walikamata bangi yenye thamani ya Dola 789,467 za Marekani kwenye shehena ikisafirishwa kama ndimu. Bangi hiyo ya uzito wa pauni 3,947 ilisindiliwa katika ndimu ‘feki’ zaidi ya 34,000.

Mwaka jana katika mpaka huo huo, mamlaka zilikamata bangi ya uzani wa pauni 2,493 iliyokuwa ikisafirishwa kama karoti kwenye magari mawili aina ya Ford. Bangi hiyo ilikuwa na thamani ya Dola 500,000.

Wednesday, September 21, 2016

Bunge Kenya lapitisha mkataba wa Epa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwa zimejipa muda kutafakari Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya, Bunge la Kenya limepitisha uamuzi wa kusaini mkataba huo.

Katika kikao cha dharura kilichofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 9, wakuu wa nchi zinazounda EAC waliamua kujipa muda wa miezi mitatu kutafakari kwa kina makubaliano hayo, yanayoitwa EAC-EU Economic Partnership Agreements(Epa), kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa makubaliano hayo yamepitishwa na Bunge.

Kenya, inayozisukuma nchi nyingine za jumuiya kusaini makubaliano hayo ambayo, miongoni mwa vipengele vyake yanaruhusu bidhaa kutoka nchi wanachama wa EU kuingia bila ya ushuru, iliitisha kikao cha dharura cha Bunge kwa ajili ya kujadili suala hilo jana.

Friday, September 23, 2016

Zaidi ya 50 wauawa wakiandamana kumpinga KabilaRais Joseph Kabila

Rais Joseph Kabila 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Zaidi ya watu 50 wameuawa walipokuwa wakiandamana kumpinga Rais Joseph Kabila mjini Kinshasa. Watu hao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa muungano wa upinzani wa nchini huo

Mmoja wa walioshuhudia anasema polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji. Upinzani umevilaumu vikosi vya usalama kwa kutumia risasi dhidi ya maandamano yanayotaka kutangwazwe tarehe ya uchaguzi wa urais.

Upinzani umeitisha maandamano zaidi leo Jumanne.

Serikali ya DRC iliwalaumu waandamanaji waliokuwa wamejihami na kusema waliouawa ni watu 17 wakiwemo polisi watatu.

Waziri wa mambo ya ndani Evariste Boshab amesema mmoja wa maafisa hao wa polisi aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa bado yu hai.

Kuna wasiwasi kuwa rais Joseph Kabila ana njama ya kutaka kusalia madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake mwishoni mwa mwaka huu.

Kadhalika Shule nyingi na biashara katika mji huo mkuu zilifungwa.

Kwa mujibu wa katiba, muhula wa pili wa Rais Kabila, aliyeingia madarakani baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka 2001, unafaa kumalizika tarehe 20 Desemba.

Mwaka uliopita, watu 12 waliuawa katika maandamao sawa na hayo.

Tangu kujinyakulia uhuru zaidi ya miaka 55, hakuna kiongozi aliyewahi kumkabidhi mrithi wake madaraka kwa njia ya amani.

 

Monday, August 15, 2016

Wapinzani wataka wapewe nchi Zambia

 

Lusaka, Zambia. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa Zambia yanaonyesha kuwa Rais Edgar Lungu anaongoza, huku wapinzani wakipinga matokeo hayo kwa madai kuwa hesabu zao zinaonyesha mgombea wao ndiye anayeongoza kama kura hazijachakachuliwa.

Lungu anakabiliwa na upinzani mkali wa Hakainde Hichilema, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Muungano kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND).

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), Rais Lungu amepata kura 262,149 dhidi ya 243,794 alizopata mpinzani wake, Hichilema baada ya kura za majimbo 26 kati ya 156 kuhesabiwa.

Taarifa iliyotolewa na UPND imeeleza kuwa mfumo wao wa kuhesabu kura ulioenda sambamba na ule wa ECZ umeonyesha Hichilema amemshinda kwa kura za kutosha Lungu baada ya asilimia 80 ya kura zote kuhesabiwa.

Maofisa wa ECZ wamevionya vyama vya siasa kutoa taarifa za aina hiyo. Hata hivyo, vyama vyote vina uwezo wa kukusanya matokeo ya upigaji kura na kujumuisha kwa haraka kuliko tume hiyo.

Awali, ECZ ilitarajia kukamilisha kuhesabu kura jana katika uchaguzi huo ambao Wazambia waliwachagua pia wabunge, mameya na madiwani na kuamua juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, maofisa wa tume hiyo wamesema matokeo rasmi yanatarajiwa  kutangazwa baadaye bila ya kutaja siku na muda maalumu.

Thursday, August 11, 2016

Trump:Obama, Cliton waanzilishi wa IS

 

Washington, Marekani. Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump amesema Rais Barack Obama na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hillary Clinton ndiyo walioanzisha kundi la kigaidi la Islamic State (IS) hivyo wanaopaswa kulaumiwa.

Trump ambaye amehutubia wafuasi wake katika mji wa Florida akisema  kundi la IS linampa heshima maalumu Rais Obama kwa kuwa ndiye mwanzilishi wake.

Amesema  kuwa Rais Obama na aliyekuwa msaidizi wake katika mambo ya nje ya Marekani,  Clinton ndiyo walioasisi na kuanzisha kundi hilo ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi nchini Iraq na Misri.

Katika miezi ya hivi karibuni wafuasi wa kundi hilo wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na kuua mamia ya watu.

Mgombea huyo wa Republican,   pia amekosoa uamuzi wa Rais Obama kuondoa jeshi Iraq akisema hatua hiyo inatoa nafasi kwa IS kupanua huduma zake duniani.

 Amesema Marekani ilipaswa kubakiza baadhi ya majeshi yake katika ardhi ya Iraq ili kutoruhusu magaidi kudhibiti ardhi ya nchi hiyo.

 

Trump kwa mara nyingine tena ametoa matamshi yanayodhihirisha misimamo yake ya chuki na ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na wageni nchini Marekani.

Trump amedai wakimbizi wa Syria nchini Marekani wanapanga njama ya kufanya shambulizi la kigaidi kama la Septemba 11 mwaka 2011 katika kituo cha biashara cha kimataifa mjini Washington.

Trump alidai lazima Marekani itashuhudia mashambulizi mengine ya kigaidi kama hilo kutoka kwa wakimbizi wa Syria wanaopewa hifadhi katika nchi yao.

“Mambo mengi mabaya yatafanyika nchini, sina shaka kwamba mashambulizi mengi ya kigaidi yatafanyika,yote haya yatasababishwa na kuruhusu wakimbizi wa Syria kumiminika katika nchi yetu,” alisema.

Trump ambaye amekuwa akikosoa siasa za kigeni za nchi hiyo na kuziita  kama msiba kwa sababu zimekosa  mwelekeo alidai  wakimbizi hao hawafai kuruhusiwa Marekani kwani  ni wanaiweka katika hatari ya kukumbwa na shambulizi jingine kama la Septemba 11 lililouwa zaidi ya watu 3,000.

Wachambuzi wa siasa za Marekani na baadhi ya wanachama wa Republican wamekuwa wakikosoa matamshi ya chuki na kibaguzi ya Trump na kusisitiza siyo tu kuwa yanahatarisha usalama wa Marekani bali  dunia nzima.

 Mwanasiasa huyo bilionea pia amekuwa akitoa kauli za chuki dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika na kudai atajenga ukuta ili kuwazua wahamiaji wa Mexico kuingia nchini Marekani.

Juzi, baadhi ya viongozi waandamizi wa Republican waliandika barua ya wazi wakimkosoa Trump kwa kuwa hafai kuwa rais wa Marekani kwa vile ni mlopokaji.

Walisema kuwa Marekani inaweza kuingia katika historia ya ajabu iwapo mwanasiasa huyo atachaguliwa katika uchaguzi wa Novemba.

 

 

Friday, August 12, 2016

Mchuano mkali urais Zambia

 

Lusaka, Zambia. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zambia imeanza kuhesabu kura kufuatia uchaguzi wa wabunge na urais huku kukitarajiwa kuwepo mchuano mkali baina ya Rais Edgar Lungu na mfanyabiashara tajiri Hakainde Hichilema.

Mamia ya wananchi wamejitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura licha ya kuwepo hali ya wasiwasi kutokana na ghasia zilizozuka wakati wa kampeni.

Lungu anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama tawala  cha Patriotic Front (PF) huku mpinzani wake mkuu Hichilema akisimamia kuwania urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND).

Lungu alimshinda kwa taabu mfanyabiashara huyo tajiri katika uchaguzi mdogo wa rais wa mwaka jana ulioitishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Michael Sata ambaye alifariki dunia Oktoba 28, 2014. Wasiwasi umetanda katika baadhi ya miji kutokana na kampeni za uchaguzi huo kumalizika kwa vurugu na machafuko.

Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, uchaguzi huo utaingia duru ya pili kutokana na kuwa, hakuna mgombea yeyote wa kiti cha urais atakayeweza kujipatia zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Jumuiya za kimataifa zimetuma waangalizi wake katika uchaguzi huo unaotajwa kuwa ni kipimo cha ukomavu wa demokrasia katika taifa hilo maarufu wa uchimbaji wa madini ya shaba. Kuporomoka kwa bei ya shaba nyekundi kumesababisha kufungwa kwa migodi na maelfu ya watu wakipoteza kazi.

Wednesday, August 3, 2016

Hollande amshambulia Trump kwa maneno

Mgombea urais wa chama cha Republican nchini

Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump 

PARIS. Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amemshambulia hadharani mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump akiyataja matamshi yanayotolewa na mgombea huyo kama yanayotia kichefuchefu.

Hollande amemshutumu Trump kutokana na matamshi yake makali dhidi ya wazazi wa mwanajeshi wa Marekani aliyefia vitani nchini Iraq akisema yanatia fedheha.

Rais wa Marekani, Barack Obama pia amemtaja Trump kuwa mtu asiyestahili kuwa Rais wa Marekani na kuwahimiza vigogo wa Republican kutomuunga mkono mgombea huyo kwani hana uelewa wa masuala ya kiuchumi na ya kigeni.

Friday, July 29, 2016

Bingwa wa kubikiri Malawi abainika ana VVU, akamatwa kwa amri ya Rais

 

Blantyre, Malawi. Rais wa Malawi, Peter Mutharika juzi alitoa amri ya kukamatwa kwa Eric Aniva ambaye hivi karibuni alibainika kufanya kibarua cha kuwabikiri mabinti wa chini ya umri wa miaka 13 zaidi ya 100.

Amri hiyo ya Rais imekuja baada ya kubainika kuwa mwanamume huyo maarufu kwa jina la ‘Fisi’ anaishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).

Mutharika alisema lazima mwanamume huyo akamatwe na hatua kali zichukuliwe dhidi yake kwa kuwa, kwa makusudi alifanya vitendo viovu akijua anaishi na VVU na lengo lake lilikuwa kuwaambukiza mabinti hao.

Aniva aliingia matatani baada ya kukiri katika mahojiano akijinasibu kuwa anaendesha maisha kwa kuwabikiri mabinti na kwamba hulipwa kuanzia dola nne za Marekani mpaka saba ambayo ni wastani wa Sh10,000 kwa kila mtu.

Mwanamume huyo alisema wazazi wa mabinti huwa wanampa kibarua cha kuwavusha kutoka utoto kuingia katika utu uzima na kwamba hatua hiyo ni sawa na tambiko.

Wednesday, July 13, 2016

Museveni aweka foleni Kampala

 

Kampala, Uganda. Rais Yoweri Museveni wa Uganda amevuta  hisia za wapita njia pale alipolazimika kusimamisha kwa muda msafara wake ili apate fursa ya kuzungumza na simu.

Museveni alikuwa safarini kurejea Kampala akitokea Wilaya ya Isingiro alikokwenda kushiriki maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Julai 11.

Akiwa njiani kurejea Ikulu, Rais Museveni ghafla aliamuru msafara wake usimame ili azungumze na simu aliyodaiwa kuwa ilikuwa muhimu.

“Tulikuwa katika barabara ya Kyeirumbi kurejea Kampala, ghafla rais aliamuru msafara wake usimame mara moja ili azungumze na simu yake ambayo tulielezwa ilikuwa muhimu,” kilieleza chanzo kimoja cha habari.

Baada ya kusimamisha msafara wake, Rais Museveni alisogea mbele kidogo kisha kuketi katika kitu na kuendelea na mazungumzo yake.

Wakati wote walinzi walikuwa wamesimama kando ya magari yaliyokuwamo kwenye msafara huo huku wengine wakiwa wamesalia ndani ya magari hayo.

Haikuweza kufahamika mara moja kiongozi huyo alikuwa akizungumza na nani wale jambo alilokuwa akilijadili. Barabara ya Kyeirumba yenye umbali wa kilometa 75 inaunganisha Uganda na Tanzania.

 

Friday, June 24, 2016

Hisa na Paundi zadoda Uingereza

By London, Uingereza

Soko la hisa la London limeanguka ghafla ikiwa ni saa chache kupita baada ya matokeo ya Uingereza kujiondoa Jumuiya ya Ulaya (EU) kupitia sanduku la kura kutangazwa mapema leo.

Mara baada ya tukio hilo la kihistoria, kiwango cha hisa cha makampuni makubwa 100 yaliyojiorodhesha katika soko la hisa la London kimeporomoka kwa zaidi ya asilimia nane kabla ya kupanda hadi pungufu ya asilimia nne.

Katika sekta ya fedha, kibenki za Barclays na RBS hisa zimeshuka kwa karibu asilimia 30 lakini hali imerudi na kuwa asilimia 20.

Mapema leo, Paundi ya Uingereza iliporomoka kwa kasi mara baada ya matokeo hayo yalipotangazwa. Anguko hilo ni mara 10 tangu sarafu hiyo ishuke kwa kasi 1983.

Hata hivyo, baadaye leo mchana sarafu hiyo ilipanda lakini ikiwa iko chini bado kwa asilimia nane.

 “Suala la Uingereza kujitoa EU limeleta wingu katika uchumi wa dunia kwa takribani mwezi mmoja sasa na sasa wingi limekuwa giza kabisa,” amesema Denis de Jong, mkurugenzi wa UFX.com.

BBC

Wednesday, June 29, 2016

Shambulio la Uturuki laua 28

By Istanbul, Uturuki.

Istanbul, Uturuki. Shambulio la kujitoa mhanga lililofanywa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ataturk mjini Istanbul, limeua watu 28 huku wengine wanaokadiriwa kufikia 60 wakijeruhiwa.

Idadi hiyo ya kuongezeka wa vifo imetolewa na gavana wa Istanbul usiku huu, inaelezwa mashambulio hayo yalihusisha watu watatu huku mmoja akidaiwa kutumia SMS kudhibiti mlango wa kuingilia uwanjani.

Milipuko hiyo inahusishwa na ama Wakurdi waliojitenga, au Kundi cha Islamic State (IS). Uwanja huo unaonekana kulengwa wa makundi ya kigaidi, licha ya kuwapo kwa mashine za kukagua usalama lakini ukaguzi kwa magari yanayoingia  siyo wa kuridhisha.

Klabu ya Yanga wiki mbili zilizopita iliweka kambi mjini Istanbul wakati ikielekea Algiers, Algeria kucheza na timu ya Mo Bejaia Juni 19 hata baada ya kumaliza mechi yake kabla ya kurejea nchini iliweka tena kambi mjini humo.

Wednesday, July 6, 2016

Pistorius ahukumiwa miaka sita jela

Mwanariadha mlemavu wa miguu wa Afrika Kusini

Mwanariadha mlemavu wa miguu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius leo amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela  kwa kosa la mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp . 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mwanariadha mlemavu wa miguu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius leo amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela  kwa kosa la mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp .

Kesi ya Mwanariadha huyo iliendelea kwenye mahakama kuu nchini humo na hukumu kutolewa muda mfupi uliopita.

Awali Pistorius alikuwa anakabiliwa na kifungo cha miaka 15 jela baada ya vita ya kisheria iliyochukua takriban miaka mitatu.

Mwanariadha huyo Oscar Pistorius tayari ameshatumikia kifungo cha takribani miezi tisa jela katika kosa la awali wakati alipopatikana na hatia ya kuua bila kukusudia mwaka 2013.

Wednesday, July 6, 2016

Messi, baba yake jela miezi 21

Mshambuliaji wa Argentina na Barcelona, Lionel

Mshambuliaji wa Argentina na Barcelona, Lionel Messi na Baba yake, Jorge Messi wamehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela. Picha ya Getty Images 

Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Argentina na Barcelona, Lionel Messi amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kutokana na kukwepa kulipa  kodi, vyombo vya habari vya Hispania vimeripoti.

Baba yake, Jorge Messi, pia amehukumiwa kifungo kwa kukwepa kulipa kodi inayokadiriwa kufikia Euro 4.1 milioni kwa kipindi cha kuanzia 2007 hadi 2009.
Pia, wawili hao watakumbanana na faini ya mamilioni ya Euro kwa kutumia njia za ulipaji wa kodi wa Belize na Uruguay, ambako kuna kiwango cha chini, zilizokuwa na lengo la kujipatia kipato cha haki za picha zake (Messi).
Hata hivyo, Messi mwenye tuzo tano za mchezaji bora wa dunia wa Fifa na baba yake wanaweza kukwepa maisha ya jela.
Kwa mujibu wa sheria za Hispania, kipengele cha kwenda jela chini ya miaka miwili kinaweza kutumikiwa kwa makubaliano maalumu.
Mshambuliaji huyo wa Barca na baba yake walikutwa na hatia ya makosa matatu katika kodi wakati wa hukumu ya jana katika Mahakama ya Barcelona.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Lionel Messi alisema kwamba 'hajui chochote' juu ya usimamizi wa fedha zake, akidai kuwa kazi yake ni 'kucheza mpira'.

Thursday, July 14, 2016

Marekani yatuma jeshi Iraq

 

Baghadad, Iraq. Marekani imeamua kutuma wanajeshi wengine 560 nchini Iraq kusaidia kupambana na kundi la Dola ya Kiislamu(IS).

 Nyongeza hiyo itafanya idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini Iraq kufikia 4650.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter akiwa nchini Iraq kwa ziara ya ghafla baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Haider al-Abadi.

Wanajeshi hao 560 ni pamoja na wapiganaji, wahandisi na wafanyakazi wa kawaida .

Wanajesh hao watakuwa karibu na kambi ya jeshi la anga ya Qayyarah. IS imeweka ngome yake nchini Iraq.

 

 

Thursday, July 14, 2016

Theresa atangaza baraza la mawaziri

 

London, Uingereza.. Ikiwa ni muda mfupi tu kukabidhiwa funguo za ofisi zilizopo zilizopo mtaa wa Downing nchini Uingereza Thereza May amemteua Boris Johnson kuwa waziri wa Mambo ya Nje pamoja na Philip Hammond kuwa Waziri wa Fedha.

Pia amemteua Amber Rudd kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Michael Fallon ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.

Akizungumza baada ya kupokea ufunguo wa makao rasmi ya waziri mkuu May amehakikishia washirika wake na mataifa ya muungano wa ulaya kuwa licha ya taifa hilo kuamua kujiondoa,Uingereza inapania kujiunga na mataifa shirika na kutekeleza wajibu wake katika muungano wa mataifa huru duniani.

Amesema kuwa serikali yake haitanaswa na mtego wa kuwasikiza mabwenyenye walio wachache na kusahau wananchi wa kawaida.

Theresa May anakuwa  waziri mkuu wa 13 kuwahi kuiongoza Uingereza katika enzi ya Malkia Elizabeth wa pili.

David Cameron amehutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Uingereza na kujibu maswali ya wabunge.

Kisha kuwasilisha  barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa Pili katika Kasri la Buckingham.

Malkia  amemtaka mrithi wa Cameron, May kuunda Serikali ikiwa ni historia ya pekee kwa Uingereza kupata kiongozi wa pili mwanamke baada ya Magreth Thatcher.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya  (EU) wameitaka Serikali ya Uingereza kuharakisha mchakato wa kujitoa rasmi katika umoja huo, lakini May amedokeza kuwa hatauharakisha mpango huo mashuhuri kwa jina la Brexit.

Changamoto  kubwa inayomkabili ni pamoja na kuizuia Scotland inayounga mkono Umoja wa Ulaya dhidi ya kuitisha kura ya uhuru wake ili kubakia katika EU na kuimarisha mahusiano mapya ya kibiashara na kidiplomasia ili kujiandaa kwa hali ya baadaye ya baada ya kujiondoa katika umoja huo.

 

-->