Wednesday, September 13, 2017

Bei elekezi kupunguza maumivu kwa wakulima Tanzania

 

By Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Wakulima wa Kyela mkoani Mbeya ni miongoni mwa watakaonufaika kwa kiasi kikubwa na bei elekezi za mbolea zilizotangazwa na Serikali baada ya bei hizo mpya kuonyesha kuwa wataokoa wastani wa zaidi Sh22,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Katika bei hizo mpya zitakazoanza kutumika Ijumaa Septemba 15, wakulima wa Kyela watanunua mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya DAP kwa bei ya rejareja ya Sh54,289 ikilinganishwa na wastani wa bei ya sasa ya Sh79,375.

Kwa mujibu wa bei hizo elekezi zilizotangazwa jana Septemba 12 na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba wauzaji wa pembejeo watatakiwa kuuza mbolea ya Urea wilayani Kyela kwa Sh41,710 kutoka wastani wa Sh64,285 kwa mfuko wa kilo 50.

Takwimu za bei za sasa zilizotolewa na wizara hiyo zinaonyesha wakulima wilayani Kyela ndio waliokuwa wakinunua mbolea kwa bei ghali zaidi katika kanda ya Nyanda ya Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Njombe.

Kwa bei hizo mpya, Serikali inatarajia iwapo mbolea ya Dap itanunuliwa kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa pamoja (PBS), gharama za ununuzi wa mbolea hiyo Kyela itapungua kwa asilimia 32 wakati Urea itapungua kwa asilimia 35.

Dk Tizeba amesema ibara ya 56 ya Kanuni za Mbolea na marekebisho yake ya mwaka 2017 inataka mbolea za aina zote ziuzwe kwa bei iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

“Kwa jumla bei elekezi ya mbolea imepangwa kwa kuzingatia gharama za ununuzi wa mbolea kutoka kwenye chanzo, usafirishaji wake kwa meli, tozo mbalimbali na faida ya wafanyabiashara. Gharama ya uingizaji kutoka nje ya nchi imejumlishwa na gharama za usafirishaji mbolea nchini,” amesema Dk Tizeba katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Iwapo mbolea zitauzwa kama Serikali ilivyopanga, wakulima wa Halmashauri ya Lindi watakuwa na ahueni kubwa kitaifa kwa kuwa bei ya sasa ya mbolea ya Dap ni Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50 lakini Serikali imeagiza iuzwe kwa Sh51,621. Wakulima wa halmashauri hiyo ndiyo wanaonunua mbolea kwa bei ya juu zaidi nchini.

Hii ina maana kuwa mkulima wa Lindi baada ya kuanza kutumika bei mpya Ijumaa hii wataweza kununua mifuko miwili ya mbolea ya Dap kwa kuongeza Sh3,250 tu badala ya mfuko mmoja wanaonunua sasa.

Hata hivyo, baadhi ya wadau mkoani Songwe wameomba Serikali kuangalia upya bei hizo kutokana na kutompa ahueni mkulima kwa kuwa bei elekezi ni kubwa kuliko ile iliyokuwa ikiuzwa mwaka jana.

Mapema mwezi huu, gazeti hili lilimnukuu mjumbe kutoka wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah kuwa bei ya mbolea aina ya Dap msimu uliopita wa 2016/17 ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh52,000 na Sh62,000.

Bei elekezi iliyotolewa kwa sasa na Serikali wilayani Mbozi katika kituo cha Vwawa, mfuko wa kilo 50 wa Dap utauzwa kwa Sh54,014.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFRA, Lazaro Kitandu ameiambia MwananchiData kuwa bei walizorekodi sokoni kwa sasa ni za wastani na sahihi.

“Hakuna eneo ambalo bei elekezi ipo juu kuliko ile tuliyoirekodi kuwa ndiyo inatumika sokoni,” amesema Kitandu.

Wednesday, September 13, 2017

Wajichimbia kuondoa vikwazo vya biashara

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Wadau kutoka nchi za Afrika wanakutana jijini hapa kwa siku tatu kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Pia, watajadili kuanzisha mfumo utakaotatua changamoto za kufahamu usalama wa masoko katika nchi hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,  Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda amesema changamoto inayolikabili Bara la Afrika katika biashara ni kuwepo kwa utitiri wa vikwazo kibiashara.

Amesema warsha hiyo imewakutanisha wadau kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuia ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas),  Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na taasisi za kibiashara katika Bara la Afrika kujadili namna ya kuondoa changamoto hizo.

Amesema mkutano huo pia utajadili namna ya kujenga mifumo ya kuongeza taarifa za kibiashara na upatikanaji wa fedha katika nchi za Afrika.

“Kama mtu anataka kuuza bidhaa anatakiwa kufahamu viwango, malipo, usalama, kuhakikisha taarifa zinakusanywa na Bara zima la Afrika kujenga mfumo ili ziweze kutumika na wafanyabiashara wote,” amesema.

Profesa Mkenda amesema changamoto ya ufanyaji biashara inajionyesha wazi katika Bara la Afrika, kwa kuwa licha ya kuwa la pili kwa wingi wa watu na kuwa na rasilimali za kutosha, mchango wake katika biashara duniani hauzidi asilimia tatu.

Amesema “Kwa kiwango hiki hata uzalishaji utapungua, hivyo kuna mambo ya kujadili kwa pamoja ili kuongeza uzalishaji. ”

Profesa Mkenda amesema ufanyaji biashara ndani ya Bara la Afrika ni asilimia 14, kulinganisha na ilivyo Ulaya ambayo ni asilimia 70.

Mkuu wa kitengo cha biashara cha Umoja wa Afrika, Nadir Merah amesema mkutano huo utatumika kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kiuchumi katika nchi za Afrika.

Pia, watajadili namna ya kupata fedha za kufanya biashara na miundo ya upatikanaji wa taarifa.

“Kama kuna mtu anataka kuuza bidhaa Ivory Coast anatakiwa kupata taarifa namna anavyoweza kuingia katika soko la nchi hiyo, viwango vya fedha vikoje na hata akitaka kuwekeza katika nchi hiyo afahamu akiwa nchini mwake, badala ya kulazimika kwenda huko,” amesema.

Amesema mfumo wa taarifa ukiwepo utarahisisha kupanua uzalishaji wa ndani wa kila nchi.

Wednesday, September 13, 2017

Wasaini mkataba kunufaika na bomba la mafuta

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz

Umoja wa watoa huduma za mafuta na gesi nchini (Atogs) umesaini mkataba wa makubaliano na wenzao wa Uganda ili kunufaika na fursa zilizopo katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga.

Mkataba huo umesainiwa leo Jumatano siku moja baada ya mkutano wa kimataifa wa wadau wa mafuta na gesi uliofanyika jijini hapa.

Makamu Mwenyekiti wa Atogs, Abdulsamad Abdulrahim amesema mkataba huo utasaidia wawekezaji wazawa katika nchi hizi mbili kunufaika na fursa zitakazojitokeza.

Mwenyekiti wa umoja huo nchini Uganda (Auogs), Emmanuel Mugarura amesema maandalizi yalianza tangu mwaka 2012 lakini wana jukumu la kutoa uzoefu wao kwa nchi rafiki ambazo zimechelewa katika maandalizi.

"Kampuni zilizopo katika nchi zetu bado hazijawa na uwezo wa kuhudumu katika mradi mkubwa kama huu lakini zikiungana zinaweza," amesema Mugarura.

Amesema endapo kampuni hizo zitashirikiana zitaweza kutoa huduma kwa haraka.

Mugarura ametoa mfano wa usafirishaji wa vifaa, akisema kampuni ya Tanzania inaweza ikavipokea bandarini na kuvipeleka mpakani mwa Uganda na baadaye kampuni ya Uganda ikamalizia safari.

Wednesday, September 13, 2017

Kutuma fedha airtel money bure kuanzia laki mbili

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

 Kama ni mteja wa simu za mkononi na unaogopa kutumia huduma za kifedha kutokana na gharama, basi kampuni ya Airtel wamekufikiria. Kampuni hiyo imeanzisha utaratibu mpya ambao mtu ambaye anatuma fedha kuanzia Sh200,000 na zaidi hatotozwa ada yoyote.

Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando amesema kuanzia sasa wateja wa Airtel Money wanaweza kutuma pesa bila tozo yoyote iwapo atatuma kuanzia kiasi cha Sh200,000 au zaidi.

“Huduma hii ni kwa wale wanaotuma kwenda mtandao wowote ule, iwe Airtel kwa Airtel au kutoka Airtel kwenda mitandao mingine,” amefafanua Mmbando.

Mmbando amesema kampuni hiyo inalenga kutimiza ahadi wanazozitoa kupitia kauli mbiu zao.

“Airtel Money bado tunawaambia wateja wetu relax (tulia)… huduma hii itakuwa na tija sana kwa wafanyabiashara au wateja wote wanaotaka kulipana pesa kuanzia kiwango cha Sh200,000 na kuendelea kwa kuwa wataokoa pesa nyingi sana watakazoweza kuzitumia kwa matumizi mengine,” anafafanua na kuongeza:

“Airtel Money tunaondoa tozo hizo kwa wateja wetu ili kuongeza ulinzi kwa kuwajengea wateja utaratibu wakutobeba pesa nyingi kwa wakati mmoja hivyo kuimarisha swala la usalama wa pesa zao kwa kuwa akaunti ya Airtel Money ni salama muda wote.”

Mmbando alifafanua kuwa wateja wanaotuma pesa chini ya kiasi hicho wataendelea kutozwa ada ingawa kiwango cha ada hizo ni kidogo sana ukilinganisha na kampuni nyingine.

Wednesday, September 13, 2017

Apple yazindua iPhone ya ajabu

 

Kampuni ya Apple imezindua simu mbili za kisasa za iPhone 8 na iPhone 8 Plus jijini California na papo hapo imeitambulisha nyingine ya iPhone X

Simu za iPhone 8 na 8 Plus zimeboreshwa kutoka zilizopo za iPhone 7 na 7 Plus kwa kuongeza baadhi ya vitu vinavyopatikana sasa katika bidhaa za kampuni ya Apple.

Simu ya iPhone X imetengenezwa ikitofautishwa na zingine za kampuni hiyo ambayo ili kuifungua jicho la mtumiaji ndilo litaitambua sura yake.

Oda kwa ajili ya simu hiyo zitaanza kuwekwa Oktoba 27 mwaka huu.

Iphone X haina kitufe ambacho huwa katikati ya simu kwa chini kama zilizo simu nyingine za kampuni hiyo.

Simu hiyo tofauti na nyingine, itachajiwa kwa kutumia vifaa visivyo na waya (wireless) na ukubwa wa kioo umeongezwa katika mfumo wa kisasa.

Iphone X imeongezewa uwezo wa kamera kwa kuwa na 3D, huku ya mbele ina megapix 7 na nyuma megapix 12.

Awali, wabobezi wengi waliamini iPhone 8 ndiyo itakuwa aina mpya ya simu za Apple lakini ni tofauti, kampuni hiyo imetambulisha iPhone X.

Kampuni ya Apple imesema lengo lake siku zote ni kutengeneza kitu cha ajabu na chenye nguvu ambacho teknolojia yake itadumu kwa muongo ujao.

 

Tuesday, March 28, 2017

Utafiti: Asilimia 90 ya wanawake hutamkiwa lugha chafu sokoni

 

By Saddam Sadick, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mwanza. Ripoti ya utafiti imeonyesha kuwa wanawake wengi hufanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwamo kutolewa lugha chafu wawapo sokoni.

Utafiti huo uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Equality for Growth (EfG) la jijini Mwanza mwaka 2014 hadi 2015, umebaini kuwa licha ya kuwa na idadi kubwa la wanawake katika masoko kulinganisha na wanaume, ni asilimia 10 pekee ya wanawake ndiyo hupewa fursa za uongozi katika masoko.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Mratibu wa Shirika la EfG Mkoa wa Mwanza, Ikupa Mwakisu alisema utafiti huo ulifanyika katika Soko Kuu la Jiji la Mwanza na lile la Makuyuni.

“Ukatili unaoongoza kwa wanawake sokoni ni maneno na lugha chafu kutoka kwa wanaume,” alisema Mwakisu.

Mfanyabiashara, Pili Mussa anashauri elimu itolewe kwa wanawake na wanaume wafanyabiashara katika masoko yote kukabiliana na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.

“Pamoja na kukosa elimu na mwamko wa kuwania fursa za uongozi, mila na desturi zinazomchukulia mwanamke kama kiumbe duni kulinganisha na mwanaume pia inachochea sisi (wanawake), kunyimwa fursa za uongozi katika kamati za soko,” alisema Mussa.

Sunday, March 26, 2017

Wabunge wataka mahindi yaliyohifadhiwa yauzwe

 

By Suzy Butondo, Mwananchi sbutondo@mwananchi.co.tz

Wabunge wameitaka Serikali kuwauzia wananchi chakula kilichohifadhiwa kwenye ghala mkoani Shinyanga.

Uamuazi huo umetolewa na wabunge wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na uhaba wa chakula.

Wajumbe wa kamati hiyo wameamua hivyo baada ya ziara katika ghala la chakula lililopo Shinyanga ili kuona kama bajeti ya Serikali imetumika na kukuta likiwa na tani 8,622 za mahindi zilizohifadhiwa. Kutokana na hatua hiyo, wameagiza chakula hicho kiuzwe kwa wananchi kwa bei nafuu ili kisiharibike.

Wabunge hao wamesema inasikitisha kuona mahindi yanahifadhiwa ndani ya miaka mitatu huku wananchi wakiendelea kulia njaa na kununua chakula kwa bei ya juu.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini amesema NFRA haina budi kuangalia sehemu zenye uhitaji wa chakula na kuwauzia wananchi chakula hicho.

“Ushauri wetu ni kuwaomba mfanye utaratibu muuze mahindi haya hata kwa Sh20,000 kwa debe moja ili kukiokoa chakula hiki na kupunguza malalamiko ya njaa kwenye jamii,” amesema mbunge huyo.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Deusdedit Mpanzi amesema hadi kufikia Machi 20, mwaka huu wameshanunua tani 62,099.319 na kati ya hizo tani 38,162.280 sawa na asilimia 61.5 zimenunuliwa katika vituo vya ununuzi, na tani 23,937. 03 sawa na asilimia 38.5 zimenunuliwa kwenye vikundi vya wakulima.

Sunday, March 26, 2017

Ushirikiano wa AQRB, wahandisi wa nje wapigiwa chapuo

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo kwenye mafunzo endelevu ya 27 ya bodi  hiyo yanayofanyika jijini Mwanza. 

By Ngollo John, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mwanza.  Serikali imeitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majengo nchini (AQRB) kushirikiana na wataalamu kutoka nchi jirani katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ujenzi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo kwenye mafunzo endelevu ya 27 ya bodi  hiyo yanayofanyika jijini Mwanza.

Profesa Mbarawa amesema kwa kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi, itasaidia kubadilishana uzoefu pamoja na kuendana na soko la ushindani.

Pia, amewataka wanachama wa bodi hiyom kutumia elimu waliyo nayo kwa uadilifu wakati wanapopata fursa za ujenzi katika miradi mbalimbali kwa ajili ya masilahi ya Taifa.

Naye Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Albert Munuo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wataalamu na wadau wa sekta ya ujenzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi, Dk Ambwene Mwakyusa, amesema wameanza kutoa vifaa vya maabara za sayansi, vyenye thamani ya Sh3 milioni ili kuhamasisha vijana wanaosoma masomo ya sayansi.

Amesema mpango huo utakuwa endelevu na ni kwa ajili ya vijana wote wa Kitanzania wanaopenda masomo hayo.

                                                              

Sunday, March 26, 2017

Tanesco Mwanza kukomalia deni la Sh4.5 bilioni

 

By Jesse Mikofu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Wakati notisi ya siku 14 iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhusiana na wadaiwa sugu kuwa wamelipa inamalizika leo, mkoani Mwanza wadaiwa wana Sh4.5 bilioni za shirika hilo.

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Mwanza, Flaviana Moshi amesema katika kundi hilo kuna taasisi za umma na watu binafsi.

Amesema tabia ya wateja kushindwa kulipa madeni yao kwa wakati wanalifanya shirika hilo lishindwe kukamilisha kazi zake au kukwama kabisa.

Hata hivyo, wakati Tanesco inakusudia kuanza leo kuchukua hatua dhidi ya wateja wake wasiolipa madeni, Meneja Mkuu wa Pepsi (SBC) nchini, Nico Coetzer ameitaka kujiridhisha kabla ya kutekeleza uamuzi huo ili usilete athari hasa katika maeneo yanayotoa huduma za afya, maji na viwanda.

Pia, ameshauri kutolewa kwa muda zaidi kwa wadaiwa hao badala ya kuwakatia umeme ambao ungeweza kuwasaidia kuendelea na uzalishaji utakaowasaidia kulipa madeni yao.

Tuesday, January 3, 2017

Wachumi washtushwa na kasi ya kufungwa biashara Dar, Arusha

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wataalamu na wadau wa uchumi na biashara wameeleza kushtushwa na taarifa za wafanyabiashara kufunga biashara zao na kushuka kwa ukuaji wa kilimo, huku wakiitaka Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kusisimua uchumi.

Juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali imebaini kuwa karibu wafanyabiashara 2,000 wamefunga biashara zao Dar es Salaam na Arusha lakini akasema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia saba na unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka huu.

Pamoja na ukuaji huo, Waziri Mpango alisema kilimo kimeshuka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2015 hadi asilimia 0.3 mwaka 2016.

Wataalamu wa uchumi na kilimo waliopigiwa simu na mwandishi wetu kuhusu taarifa hiyo ya Waziri Mpango aliyoitoa alipokuwa akizungumzia hali ya uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, walisema hiyo ni ishara mbaya na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja alisema taarifa ya wafanyabiashara kufunga biashara zao inatokana na kilio chao cha muda mrefu kisichosikilizwa na Serikali.

“Tunachokijua ni kuwapo kwa mtikisiko wa uchumi kwa mwaka 2016 kiasi kwamba wafanyabiashara wanalalamika kukosa wateja. Siyo kufunga biashara tu, wengine wamerudisha hata TIN (namba ya utambulisho wa mlipakodi) kwa kushindwa masharti,” alisema Minja. “Tunachotofautiana na Serikali ni kuhusu sababu, sisi tunachojua chanzo ni masharti magumu ya kufanya biashara ndicho kinachowashinda watu. Sasa kama Waziri Mpango hajui basi kuna udhaifu kiuongozi.”

Alikuwa akizungumzia kauli ya waziri kwamba sababu za kufungwa kwa biashara hizo hazijabainika kutokana na ugumu wa kupata taarifa kwa wahusika, lakini akabainisha sababu tano za jumla zinazoweza kuwa chanzo ambazo alizitaja kuwa ni kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara, kushindwa kusimamia biashara, gharama kubwa za uendeshaji na wabia katika biashara kutoelewana.

Minja aliitaka Serikali kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara: “Unapoona mlipakodi mmoja kati ya 99 anajitoa, unatakiwa uwaache hao 99 umrudishe huyo mmoja, lakini kama hujui hata sababu, basi huo upungufu kiuongozi,” alisema Minja.

Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema kushuka kwa ukuaji wa kilimo kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 0.3 ni ishara kuwa umaskini umeongezeka.

“Ni wazi kwamba katika mwaka mmoja, tumetengeneza maskini wengi kuliko miaka mingine iliyopita. Tusijidanganye kwamba kuna sekta nyingine kama madini au gesi ndivyo vitabeba uchumi wetu. Hata uchumi wa viwanda unategemea kilimo,” alisema Rukonge.

Akizungumzia hali ya kilimo na biashara, Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Sokoine, Ntengua Mdoe alisema imekuwa mbaya kwa sababu Serikali haiwekezi.

“Wananchi wengi wanategemea kilimo, japo kuna baadhi ya sekta zinazokuza uchumi. Kama ukuaji wa kilimo umeshuka, basi kuna asilimia 75 ya Watanzania wanaendelea kuwa maskini,” alisema.

Profesa Mdoe aliongeza, “Hata biashara zimekuwa ngumu, tunaona hoteli zikifungwa hapo Dar es Salaam na nyingine zikibadilishwa matumizi, ni kwa sababu hakuna mzunguko wa fedha, uwezo wa watu kununua umeshuka. “Serikali inapaswa kuongeza fedha kwenye mzunguko hasa kwenye sekta binafsi ili uwezo wa kununua uongezeke.”

Mtaalamu aliyebobea katika uchumi, Profesa Samuel Wangwe alisema ukuaji wa uchumi hautakuwa endelevu kama kilimo hakikui.

“Kama hali ya hewa itakuwa nzuri basi na uchumi nao utakuwa mzuri, lakini hali ikiwa mbaya na mavuno yasipopatikana, uchumi hauwezi kukua.”

Profesa Wangwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ameishauri Serikali kujenga uhusiano na sekta binafsi ili iweze kuajiri na kulipa kodi.

Tuesday, October 25, 2016

Walionunua Sumsung Galaxy Note 7 kurudishiwa gharama zao

 

By Peter Elias, Mwananchi

Dar es Salaam. Kampuni ya Sumsung Afrika Mashariki (SEEA) imetangaza kuwabadilishia simu au kuwarudishia gharama zao wateja wote walionunua simu za Samsung Galaxy Note 7 popote duniani.

Hatua hiyo imefuata baada ya kubainika kwamba simu hizo ni hatari kwa sababu betri zake zinalipuka. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga marufuku uingizaji wa simu hizo nchini kwa sababu za kiusalama.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, watu walionunua simu hizo watabadilishiwa na kupewa simu ya Galaxy S7 au Galaxy S7 Edge au Galaxy Note 5 na watarudishiwa gharama za ziada.

Mbali na kuwabadilishia simu, kampuni hiyo imefafanua kwamba wateja wanaotaka kupewa fedha taslimu watarudishiwa fedha kamili walizonunulia Samsung Galaxy Note 7 kama wana uthibitisho wa risiti.

 

Tuesday, October 25, 2016

Wajasiriamali 280 kukutana Pwani

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage 

By Julieth Ngarabali, Mwananchi jngarabali@mwananchi.co.tz

Pwani. Wajasiriamali 280 kutoka mikoa ya Kanda ya Mashariki, wanatarajiwa kushiriki maonyesho ya tisa yatakayofanyika wilayani Bagamoyo, Pwani.  Maonyesho hayo yanayoratibiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido), yanatarajiwa kuzinduliwa kesho na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage  katika Viwanja vya CCM wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amewataka wananchi na wadau kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao, kwani zimetengenezwa kwa ubora unaotakiwa.

 Meneja wa Sido Mkoa wa Pwani, Agnes Yesaya amesema kaulimbiu ya maonyesho hayo ni ‘Uchumi wa viwanda unategemea viwanda vidogo’. Yesaya alisema lengo ni kukuza ubora wa bidhaa na kujifunza mbinu za ushindani, kusaidia wajasiriamali hasa wa vijijini  kutangaza bidhaa zao.

Tuesday, October 25, 2016

Wakulima Mkonge waanza safari, waomba pembejeo za ruzuku

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi rsaid@mwananchi.co.tz

Korogwe. Katika kuhakikisha wanajikomboa, wakulima wa mkonge wameshauriwa kununua hisa kwenye viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuondokana na kuendelea kuzalisha malighafi pekee.

Mkoa wa Tanga mwaka 1964 ulifikia uzalishaji wa asilimia 65 ya tani 234,000 za mkonge zilizozalishwa nchini.

Uzalishaji wa mkonge uliendeshwa katika mashamba makubwa ambayo yalikuwa na eneo la wastani wa hekta 3,000, huku asilimia 75 yakimilikiwa na wageni kutoka nje.

Mkonge uliingizwa nchini kwa magendo kutoka nchini Mexico mwaka 1893 na Mtafiti wa Mimea na Udongo wa Kijerumani, Dk Richard Hindorff. Inaelezwa kuwa alichukua miche 1,000 kutoka Jimbo la Yucatan, Mexico ambako ndiko asili ya jina Katani.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kiwanda cha Kusindika Mkonge katika Shamba la Magoma wilayani Korogwe juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte alisema iwapo watapigania kuwa na hisa viwandani, itawasaidia kujua kinachoendelea sokoni.

Shamte alisema kilimo bila ya viwanda siyo endelevu na kwamba, kitakuwa ni kuganga njaa.

“Tanzania ya viwanda lazima ianzie katika viwanda ambavyo vitabadilisha mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge wa Shamba la Magoma, Omar Athuman alisema wanaomba kupewa hati miliki ya mashamba wanayotumia ili wawe na uhakika wa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.

Athuman alisema wanashindwa kukopa kutokana na kukosa hatimiliki za mashamba.

Pia, alisema wakulima wanaomba ruzuku kama wenzao wa mazao mengine kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella aliipongeza Kampuni ya Katani Limited kwa uamuzi wa kuinua na kuendeleza kilimo cha mkonge.

Shigella aliwaeleza kuwa wakulima wa katani ni wajasiriamali na wawekezaji wa kweli ambao kwa pamoja wanatekeleza kwa vitendo vita dhidi ya umasikini, hivyo kutengeneza ajira na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.

Monday, October 24, 2016

Wafanyabiashara wamtajia JPM kero saba zitakazomkwamisha

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfumo wa ukusanyaji kodi na tozo mbalimbali nchini, umebainika kuwa kero namba moja miongoni mwa saba zilizotajwa na viongozi wafanyabiashara ambazo huenda zikamkwamisha Rais John Magufuli kufikia ndoto ya viwanda.

Utafiti huo unaonyesha kero nyingine zinazowatesa wafanyabiashara ni uhaba au ukosefu wa huduma ya umeme, makato makubwa ya kiwango cha kodi, rushwa, ukosefu wa mitaji na ubovu wa barabara.

Wafanyabiashara hao walisema utitiri wa kodi usiokuwa na mpangilio au usiotambuliwa rasmi umekuwa ukiwakatisha tamaa kuendeleza au kukuza biashara zao.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), uliopewa jina la Mtazamo wa Viongozi Wafanyabiashara Juu ya Mazingira ya Uwekezaji Tanzania 2015, unaonyesha kati ya viongozi wafanyabiashara 597 waliohojiwa, nusu walisema biashara zinakabiliwa na kikwazo cha ukusanywaji wa kodi unaofanywa na halmashauri na taasisi za Serikali.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Agosti na Septemba, 2015 katika mikoa mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema: “Tulipowauliza sababu (wafanyabiashara hao) wakasema siyo kwamba hawataki kulipa kodi, ila walilalamikia zile zisizokuwa na utaratibu maalumu, wakapendekeza kwa nini kusiwapo na mfumo unaozitambua tozo na kodi wanazotakiwa kulipa.”

Hata hivyo, Simbeye alisema matokeo ya utafiti huo hayahusiani na uongozi uliongia madarakani Novemba mwaka jana.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Hussein Kamote alisema Serikali inaweza kuchelewa kufikia ndoto ya viwanda endapo haitabadilisha mfumo wa makusanyo ya tozo kwa mamlaka zinazofanya kazi zinazofanana.

“Kwa mfano Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango (TBS), halafu Osha (Wakala wa Usalama na Afya Sehemu za Kazi) na Zimamoto wanatoa huduma zinazofanana, lakini kila moja inataka tozo kwa mmiliki wa kiwanda anayetaka huduma zao,”alisema.

Monday, October 24, 2016

Miradi ya Tasaf yaajiri Wahadzabe

Maji nio miongoni mwa huduma zitakazopatikana

Maji nio miongoni mwa huduma zitakazopatikana baada ya miradi kukamilika. 

By Gasper Andrew, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mkalama. Watu wa kabila la Wahadzabe wanaoishi Kijiji cha Kipamba, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wanatarajia kupata ajira za muda katika miradi ya ujenzi itakayoanzishwa eneo hilo.

Miradi hiyo yenye thamani Sh562 milioni imeanzishwa na mpango wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa ajili ya kabila hilo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji juzi, Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida, Patrick Kasango alisema Sh562.7 milioni zimenunulia vifaa vinavyotumika kwenye miradi hiyo inayotoa fursa za ajira za muda kwa walengwa.

“Ajira hizi za muda zimelenga kuziongezea kipato kaya zilizoandikishwa kwenye mpango wa Tasaf III. Pia, wakati huohuo zitakuwa zimeshiriki kuondoa kero zinazowakabili katika maeneo yao, ikiwamo uhaba wa maji, zahanati na barabara,” alisema Kasango.

Kasango alisema licha ya mafanikio hayo, wanakabiliwa matatizo mbalimbali ikiwamo uhaba wa magari, barabara mbovu ambazo wakati wa masika hazipitiki na baadhi ya kaya kutembea umbali mrefu kwenda kituo cha uhaulishaji fedha na maeneo kutokuwa na huduma za simu.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Edward Mkumbo licha ya kuipongeza Serikali na wadau kwa kushirikisha Wahadzabe kwenye mpango wa Tasaf, wanaomba kuwajengea barabara.

“Kama mpango huu usingeanzishwa kwetu, hali ingekuwa mbaya kwa sababu vyakula vyetu vya asili havipatikani tena. Kama mnavyojua hatuna utamaduni wa kulima, niiombe Serikali itupatie wahudumu wa afya,” alisema Mkumbo.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Wolter Soer alisema timu yao imeridhishwa na utekelezaji wa Tasaf mkoani humo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza mpango huo. “Kwa Kabila la Wahadzabe tumeguswa zaidi, tutachukua hatua maalumu kulisaidia. Tunataka ifike wakati na Wahadzabe wawe na maisha bora kama walivyo Watanzania wengine,” alisema.

Kasango alisema Tasaf III mkoani humo imetumia zaidi ya Sh18.8 bilioni kunusuru kaya masikini 40,218, kati ya Septemba hadi Oktoba.

Hata hivyo, alisema kaya 281 zimeondolewa katika mpango huo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya kukosa sifa.

Sunday, September 25, 2016

IPTL wairuka benki ya Standard Chartered - Hong KongPicha na Omari Fungo.

Picha na Omari Fungo. 

By Peter Elias, Mwananchi

Dar es Salaam. Kampuni ya kufua umeme ya IPTL imesema haiitambui benki ya Standard Chartered - Hong Kong kama mdai wao wala haina haki ya kupata malipo yoyote kwa niaba yao.

Kampuni hiyo inaunga mkono hatua ya Tanesco kukata rufaa katika màhakama ya ICSID kwasababu hukumu iliyotolewa ina mapungufu mengi kisheria.

Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege amesema watu wasifanye makosa kuilipa benki  hiyo Kwa sababu wanataka kutapeli.

"Hii benki ya Standard Chartered haistahili kulipwa fedha yoyote kwa niaba yetu. Hatuwatambui kama wadai wetu, ndiyo maana wanakimbia mahakama za ndani na kwenda nje."

Sunday, September 25, 2016

Mchakato vitambulisho vipya vya Taifa Oktoba 3

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana Dar es Salaam. Picha na Said Khamis 

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wizara ya Utumishi na Utawala Bora iliyo chini ya Ofisi ya Rais, imesema kazi ya uhakiki wa watumishi hewa itakwenda sambamba na utoaji wa vitambulisho vipya vya Taifa kwa watumishi wa umma.

Katika mchakato huo, wizara hiyo itashirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), ambayo itaratibu mchakato wote wa utambuzi, kuhakiki taarifa za watumishi  na kuchukua alama za vidole.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki amesema mchakato huo utafanyika kwa wiki mbili kuanzia Oktoba 3 na utawahusisha watumishi wa wizara, taasisi za Serikali zinazojitegemea, tawala za mikoa, mamlaka za Serikali za Mitaa na mashirika ya umma.

 

Sunday, August 14, 2016

Tanzanite ya Sh7.4 bil yapigwa mnada

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi

Arusha. Madini ya Tanzanite yenye thamani ya Dola 3.4 milioni za Marekani (Sh7.4 bilioni), yameuzwa kwenye mnada uliofanyika kwa siku nne jijini Arusha, huku Serikali ikipata mrabaha wa Sh378 milioni.

Katika mnada huo, Kampuni ya TanzaniteOne na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ziliongoza kwa kuuza madini ya Dola 3.3 milioni (Sh7.3 bilioni), huku Serikali ikiweka kibindoni mrabaha wa Sh367 milioni.

Katika mauzo mengine, Kampuni ya Franone iliuza madini ya Dola 100,000 (Sh215 milioni) na Serikali ilipata mrahaba wa zaidi ya Sh10 milioni.

Mkurugenzi wa Uthaminishaji Madini ya Almasi na Vito Wizara ya Nishati na Madini, Archard Karugendo amesema  hayo  Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera akifunga mnada wa Tanzanite.

Karugendo amesema wachimbaji na wanunuzi walioshiriki mnada huo ni kampuni 37, wachimbaji watano waliojitokeza ni TanzaniteOne na Stamico, Tanzanite Africa/J.S Magezi, Chusa Mining, Kurian Laizer na Franone Gems.

Amesema kampuni zinazonunua na kuuza madini ndani na nje ya nchi zilishiriki mnada huo, lengo likiwa ni kuhakikisha bei ya Tanzanite ambayo ilikuwa imeshuka inapanda na kuweka ushindani kwa njia ya minada.

Bendera amesema Tanzanite inapatikana eneo moja la Mirerani wilayani Simanjiro, hivyo Serikali itaendelea kudumisha ulinzi na usalama kwa wachimbaji.

Amesema kwa mnada huo, bei ya Tanzanite itauzwa bei inavyostahili na Wilaya ya Simanjiro itakusanya mapato yake ya kodi ya huduma kwa urahisi zaidi, hivyo kutoa huduma za jamii kwa ufanisi.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amesema kupitia mnada huo mapato ya nchi yataongezeka hasa kwa madini ya Tanzanite, kwani mnada unafanyika eneo moja.

Profesa Mdoe amesema kwa sababu mnada huo ni wa kwanza, zipo changamoto zilizojitokeza kwani  maandalizi yamekuwa ya muda mfupi. “Kwa njia hii ya mnada huu tunakabiliana na suala la utoroshaji Tanzanite kwenda nchi za jirani, kwani wanunuzi watapata fursa ya kufika kununua wenyewe,” amesema Profesa Mdoe.

 

Sunday, August 14, 2016

Kaya 900 zanufaika na umeme jua

By Godfrey Kahango, Mwananchi

Mbeya. Zaidi ya kaya 900 za mikoa ya Mbeya na Songwe, zimenufaika na nishati ya umeme wa jua unaotumia vifaa vya Kampuni ya Mobisol.

Meneja wa Mobisol Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Vedast Thadeo alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika kuhusu kazi zilizofanywa na kampuni hiyo vijijini.

Thadeo amesema kampuni hiyo imejikita zaidi kuwekeza vijijini ambako nishati hiyo ni adimu, huku akitaja wilaya zilizoanza kunufaika kuwa ni Mbeya, Rungwe za Mbeya na Mbozi ya Songwe.

Amesema lengo la kampuni hiyo ni kusaidia Serikali kuhudumia wananchi hususan suala la umeme, ndiyo maana wamekuja na njia  mbadala ya nishati hiyo ambayo mteja ananunua kati ya Sh1 milioni hadi Sh3 milioni.

Meneja Masoko wa Mobisol, Lusajo Mwakapoje alisema tangu kuanzishwa na kuanza kufanya kazi nchini mwaka 2011, wamefanikiwa kufunga mitambo kwa zaidi ya kaya  55,000 mikoa 16  ya bara.

Mwakapole amesema kampuni imetoa fursa kwa wateja wake kulipa kidogokidogo na kwamba, wapo wanaolipa Sh51,740 kwa mwezi, Sh73,140 na wengine Sh115, 140.

Amesema wateja wa aina hiyo wanakopeshwa kwa muda wa miaka mitatu, baada ya hapo wanaendelea kutumia umeme bila kulipia.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika amepongeza mipango ya kampuni hiyo akisema  Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni zote zinazofanya kazi za maendeleo nchini.

 

Tuesday, July 12, 2016

ATCL kupata ndege mpya Septemba

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imelipa Sh36 bilioni, sawa na asilimia 40 kwa ajili ya kununua ndege mbili za shirika la ndege la ATCL.

"Kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano tutahakikisha hatua za ununuzi wa ndege mpya zinafanyika kwa haraka ili kuweza kulifufua shirika letu la ndege na kuweza kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga ifikapo mwezi Septemba mwaka huu," amesema

Waziri huyo ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma na kusema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya upanuzi wake.

 "Mradi huu umetupa mfano kama tukijipanga vizuri hata kwenye miradi mingine tunaweza kutekeleza kwa haraka na ubora unaotakiwa, kwa upande wetu kama Serikali tutahakikisha uwanja huu unakamilika haraka ili kuruhusu ndege kubwa kuanza kutua," amesema.

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz

Tuesday, July 12, 2016

Mnorway aipigia chapuo gesi mpya

 

By Mwandishi wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni yenye mradi wa nishati hiyo nchini Norway, Thomas Abraham-James amesema  Tanzania inaweza kuingiza fedha nyingi za kigeni kutokana na kugunduliwa kwa gesi adimu ya helium.
“Gesi ya helium ina biashara kubwa katika soko la kimataifa,  lakini ukosekanaji wa soko unatokana na bidhaa hiyo kuwa adimu hivyo huenda Tanzania ikasaidia kuongeza soko la gesi ya helium katika soko la kimataifa pale itakapoanza kuzalishwa na kuuzwa nje ya nchi," amesema.
Gesi ya helium ambayo ni adimu hutumiwa kwenye vifaa vya kitabibu kama mashine ya kuchukulia vipimo vya MRI Scanner, kubashiri moto viwandani, kuunganisha vyuma na nishati ya nyuklia.
Gesi hiyo pia hutumika kubaini alama kwenye za utambulisho wa bidhaa. Kwa Tanzania gesi ya helium iligunduliwa na wataalamu kutoka Uingereza Juni mwishoni mwaka huu.

Sunday, July 10, 2016

Waziri Mkuu India ameondoka nchini

 

Waziri Mkuu India ameondoka nchini jioni hii kwenda nchini Kenya kukamilisha ziara yake ya kwanza Afrika baada ya kutembelea Tanzania, Afrika Kusini na  Msumbiji

Saturday, July 9, 2016

Wasaka wafanyabiashara wakubwa

 

By Dinna Maningo, Mwananchi dmaningo@mwanachi.co.tz

Tarime. Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, Charles Lawrence amesema wanafanya jitihada kuwashawishi wafanyabiasha wawili wakubwa mkoani humo ambao watauziwa sukari ya Serikali kwa bei nafuu.

Lawrence amesema uamuzi huo unalenga sukari hiyo inunuliwe yote ili iweze kusambazwa kwa wananchi kwa bei nafuu. 

Ofisa huyo ambaye hakuwa tayari kuwataja majina wafanyabiashara hao, amesema uuzaji wa sukari hiyo unatokana na wafanyabiashara wengi kuisusia kutokana na bei ya jumla ya mfuko kuwa kubwa, hivyo kuwafanya wapate hasara. 

“Tunaamini kwa utaratibu huu wananchi watapata sukari kwa bei nafuu kabisa,” amesema.

Saturday, July 9, 2016

Kizungumkuti chaibuka ununuzi wa pamba

 

By Shija Felician, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kahama. Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Pamba nchini, George Mpanduji ameiomba Serikali kuutafutia ufumbuzi wa haraka mgogoro wa ununuzi wa zao hilo.

Mpanduji amesema hayo kufuatia wanunuzi wa zao hilo kugoma wakishinikiza Serikali kuondoa ongezeko la Sh200 kwa kilo katika bei elekezi ya Sh1, 000 iliyotangazwa hivi karibuni. 

Aliitaka Serikali kudanya hivyo ili kuwaondolea kero wakulima ambao wamebaki njia panda wasijue pa kuuzia zao hilo baada ya mavuno. 

“Serikali ipunguze utitiri wa kodi na ushuru wa mazao kuanzia zile zinazotozwa na Serikali kuu na halmashauri za wilaya. Hii itapunguza gharama za uendeshaji kwa makampuni na wanunuzi wa pamba,” alishauri Mpanduji

Friday, July 8, 2016

Muhongo ataka mchakato wa kufungua biashara uwe mwepesi

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amefunga maonyesho ya biashara ya kimataifa huku akisisitiza kasi ya kufungua biashara na mikataba kwa wawekezaji.
Amesema ni Tanzania pekee ndiyo nchi ambayo ili kuanzisha biashara inabidi ufuate hatua tisa.
Amesema ili kuendana na kasi ya dunia na kukimbizana na harakati za kukua kiuchumi inabidi siku za kuanzisha biashara zipungue na kubaki tatu.
"Naomba mwaka ujao mniite kufunga maonyesho tena ili niangalie kama Wizara ya Viwanda, biashara na Uwekezaji mmelifanyia Kazi hili" amesema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo amesema hatua ambazo mtu anachukua kuanzia kufuatilia vibali, leseni hadi kuanza biashara zipo 21 na kutaka zipungue na zibaki tano.
" Hatuwezi kwenda hivi zibaki tano , mtu akianza kufuatilia leseni Jumatatu hadi ijumaa awe amepata , tutumie kompyuta tuachane na kukusanya makaratasi, mafaili inawezekana ndiyo inachangia kuchelewa" amesema.
Wakati huo huo rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa wafanyabiashara wadogo watafutiwe masoko ili kuwainua kiuchumi.
na biashara zao zinavutia hivyo watafutiwe masoko ya uhakika ili wasonge mbele"amesema Kikwete.

Saturday, July 9, 2016

Kodi ya utalii yazua jambo

 

By Florence Majani, Mwananchi fmajani@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nchi 30 za Ulaya zimeiandikia barua Serikali ya Tanzania zikiomba ifikirie upya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii iliyoanza mwezi huu au isianze kutumika hadi mwaka ujao.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema walipata wazo la kuanzisha kodi hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya.

Wakati sheria hiyo ikianza kutumika nchini, nchi hizo za Ulaya ambazo ni wadau wakuu katika sekta ya utalii zimemwandikia barua hiyo Dk Mpango, naibu wake, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Chama cha Kitaifa wa Mawakala wa Usafiri na Wasimamizi wa Utalii (ECIAA) kutoka nchi 30 za Ulaya ndicho kinachoziwakilisha kampuni zaidi ya 70,000 za utalii barani humo.

Nchi hizo ndizo zinazotoa asilimia 50 ya watalii wote duniani.

 

Friday, July 8, 2016

Muhongo ataka mchakato wa kufungua biashara uwe mwepesi

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amefunga maonyesho ya biashara ya kimataifa huku akisisitiza kasi ya kufungua biashara na mikataba kwa wawekezaji.
Amesema ni Tanzania pekee ndiyo nchi ambayo ili kuanzisha biashara inabidi ufuate hatua tisa.
Amesema ili kuendana na kasi ya dunia na kukimbizana na harakati za kukua kiuchumi inabidi siku za kuanzisha biashara zipungue na kubaki tatu.
"Naomba mwaka ujao mniite kufunga maonyesho tena ili niangalie kama Wizara ya Viwanda, biashara na Uwekezaji mmelifanyia Kazi hili" amesema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo amesema hatua ambazo mtu anachukua kuanzia kufuatilia vibali, leseni hadi kuanza biashara zipo 21 na kutaka zipungue na zibaki tano.
" Hatuwezi kwenda hivi zibaki tano , mtu akianza kufuatilia leseni Jumatatu hadi ijumaa awe amepata , tutumie kompyuta tuachane na kukusanya makaratasi, mafaili inawezekana ndiyo inachangia kuchelewa" amesema.
Wakati huo huo rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa wafanyabiashara wadogo watafutiwe masoko ili kuwainua kiuchumi.
na biashara zao zinavutia hivyo watafutiwe masoko ya uhakika ili wasonge mbele"amesema Kikwete.

-->