Wednesday, April 19, 2017

TTB yaanza kutangaza vivutio Israel

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeanza mpango wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania  nchini Israel ikiwa mwendelezo wa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mwenyekiti wa TTB Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema leo kuwa mpango huo unalenga kuongeza idadi ya watalii kutoka Israel ambao wameonyesha mwamko wa kuja kuangalia vivutio vya utalii nchini.

Amesema kwa kuanzia bodi hiyo imeandaa ziara ya siku tatu kwa watu maarufu kutoka Israel kuja kutembelea hifadhi ya Gombe.

Jopo hilo la wageni 10 litahusisha waandishi wa habari, mawakala wa kampuni ya usafirishaji watalii ya Safari Company na mwigizaji maarufu kutoka Israel anayefahamika kama Rashef Polly.

Wednesday, April 19, 2017

Aliyempima mama anayedai kuzaa mapacha Temeke azua utata mpya

 

By James Magai na Jackline Masinde mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sakata la Asma Juma (29) anayedai kuibiwa pacha wake, limechukua sura mpya baada ya uongozi wa hospitali binafsi ya Huruma kusisitiza kuwa mtaalamu aliyechukua vipimo vya utrasound amekuwa akifanya kazi hiyo hata kwa mwajiri wake ambaye ni Serikali.

Kauli hiyo inapingana na iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Hopsitali ya Temeke, Amani Malima kwamba daktari aliyemfanyia Asma vipimo hivyo hana utaalamu huo na kwamba yeye kazi yake ni kupiga picha za x-ray na amekuwa akifanya vipimo vya ultrasound kama njia ya kumweka mjini.

Hospitali ya Temeke ndiyo inadaiwa na Asma kwamba imehusika na wizi wa mtoto wake mmoja baada ya ujauzito wake kuonyesha alikuwa na mapacha.

Lakini, jana Mganga Msimamizi wa Zahanati ya Huruma, Dk Erasmo Kuwendwa akiwa ameambatana na daktari aliyemfanyia mama huyo vipimo hivyo, alisema wana uhakika na vipimo vyao.

Dk Kuwendwa alisema kuwa mama huyo alifika katika zahanati hiyo na kufanya vipimo hivyo mara mbili na kwamba mara zote hizo alibainika ana mapacha na kwamba wote walikuwa na afya njema.

“Mara ya kwanza alifika hapa Februari 17 mwaka huu, alifanyiwa kipimo cha ultrasound na majibu yaliyoonekana ni kwamba ana mapacha ambao wote walikuwa salama na walikuwa na umri wa wiki 33.” alisema Dk Kuwendwa na kuongeza:

“Lakini pia Asma Juma alifika tena hapa Machi 7, mwaka huu, pia alifanyiwa kipimo hicho hicho na mtaalam wetu na kilichoonekana ni kwamba ana mapacha wenye umri wa wiki 36.”

Dk Kuwendwa alisema taarifa hizo ndizo zilizoko kwenye kumbukumbu zao na kwamba baada ya kufanyiwa vipimo hivyo mtaalam wao huwa anaandika ripoti na kisha anabandika na picha (image) za vipimo vya kile alichokiona.

Kuhusu taarifa za daktari aliyefanya vipimo hivyo kutokuwa na utaalam, Dk Kuwendwa alisema:

“Ninachojua mimi ni kwamba huyu mtaalam wetu aliyefanya hivyo vipimo ni mwajiriwa wa Serikali, ndani ya Manispaa ya Temeke, anafanya kazi Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, na huko anafanya x-ray, anafanya ultrasound na ni muda mrefu.”

Alisisitiza kuwa anaamini kuwa mtaalam huyo ana uzoefu na anajua kwamba ameajiriwa na Serikali kufanya kazi hizo hizo.

Alisema anashangaa kuwa picha za ‘ultrasound’ zimepotea na kusema kuwa hizo ndizo zingeleta majibu.

Wakati mkanganyiko huo ukitokea kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo imemaliza kazi na kukabidhi ripoti kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Mohamed Kambi.

Mganga Mkuu wa Hopsitali ya Temeke, Amani Malima jana alisema: “Tunasubiri tu majibu ya ripoti toka kwa waziri mwenye dhamana ila ripoti tayari imekabidhiwa kwa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ataipeleka kwa waziri kwa ajili ya hatua stahiki,” alisema Dk Malima.

Alisema kamati hiyo iliundwa na Mganga Mkuu wa Serikali kwa agizo la Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mwanamke huyo.

Alisema kamati ilifanya uchunguzi kwa muda wa wiki moja imekabidhi ripoti Ijumaa ya wiki iliyopita.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Dk Kingwangala hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopokelewa kwa siku nzima ya jana.

Asma ambaye alijifungua kwa njia ya upasuaji kwenye Hospitali ya Temeke Machi 17 na kuambiwa alikuwa na mtoto mmoja, alidai vipimo alivyofanyiwa kwenye Zahanati ya Huruma pia madaktari wawili wa Temeke walivithibitisha kwamba ujauzito wake ni wa watoto mapacha.

Alidai licha ya madaktari hao wawili kujiridhisha, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji, alipewa mtoto mmoja.

Asma na mumewe Aboubakar Pazi walisema wamewasilisha madai yao kwa uongozi wa hospitali na uchunguzi unafanywa.     

Wednesday, April 19, 2017

Wakurugenzi 120 waliotumbuliwa wanalipwa Sh480 milioni kwa mwezi

“Ikumbukwe kuwa wakurugenzi hawa bado wanalipwa

“Ikumbukwe kuwa wakurugenzi hawa bado wanalipwa mishahara yao pamoja na stahiki nyingine za kiutumishi kama nyumba, umeme, simu, matibabu na kadhalika. Wastani wa mshahara wa mkurugenzi ni Sh3.8 milioni mpaka Sh 4 milioni,” Japhray Michael 

By Sharon Sauwa, Mwananchi; ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Maoni ya upinzani ya wizara mbili, jana yaliibua hoja tofauti; ya kwanza ikidai Serikali inawalipa wakurugenzi 120 waliotumbuliwa Sh480 milioni, na ya pili ikikikishutumu kiti cha Spika kwa kuzuia mjadala wa wabunge kutishiwa maisha.

Katika sakata la kwanza, wapinzani walisema fedha za Serikali zinapotea kutokana na watumishi waliotumbuliwa au kuachwa katika uteuzi kuendelea kulipwa stahiki zao.

Msemaji wa kambi hiyo, Japhary Michael alisema wakati akitoa maoni kuhusu bajeti ya Tamisemi kuwa wakurugenzi hao wanalipwa mshahara wa Sh5.76 milioni kila mmoja kwa mwezi.

“Ikumbukwe kuwa wakurugenzi hawa bado wanalipwa mishahara yao pamoja na stahiki nyingine za kiutumishi kama nyumba, umeme, simu, matibabu na kadhalika. Wastani wa mshahara wa mkurugenzi ni Sh 3.8 milioni mpaka Sh4 milioni,” alisema.

Alisema wakurugenzi 120 wa zamani hawakuteuliwa kwa nafasi hizo katika Serikali ya Awamu ya Tano lakini bado wamo katika utumishi wa umma, na hata wale wapya walioteuliwa walitoka nje ya mfumo wa utumishi wa umma, wengi wao wakiwa makada wa CCM.

Alisema baada ya kutenguliwa kwa wakurugenzi hao 120 kutoka halmashauri mbalimbali nchini, walielekezwa kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa waliyotoka kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.

“Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa wakurugenzi hawa takribani wote wanahudhuria kwa makatibu tawala wa mikoa na kimsingi hawana kazi za kufanya,” alisema.

Alisema kambi hiyo inaishauri Serikali kuangalia upya sheria ya utumishi na ajira katika serikali za mitaa ili kuwe na utaratibu ambao mchakato wake utaanzia katika vikao kisheria vya halmashauri.

Michael, ambaye ni mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), alishauri Waziri ateue kutokana na orodha itakayopendekezwa na halmashauri baada ya watu kuomba ajira.

Katika sakata la pili, msemaji wa kambi ya upinzani bungeni anayehusika na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ruth Mollel alidai kiti cha Spika kilizuia mjadala wa wabunge kutishiwa maisha kwa mgongo wa kanuni za Bunge.

Suala hilo lilimfanya waziri husika, Jenista Mhagama kusimama na kutaka sentensi hiyo ifutwe kwa kuwa ilishaondolewa wakati kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akisoma maoni yao kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Lakini hoja hiyo ilipingwa na mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa aliyesema kuwa Katiba inawapa uhuru wa kusema maneno hayo.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alisema maoni hayo yaliandikwa na mtu ambaye haelewi taratibu za Bunge na hivyo kufuta sentensi hiyo.

Alihoji kama kuna mbunge aliyepeleka taarifa ya kutishiwa maisha.

Kuhusu hoja kwamba wapinzani wanadhibitiwa, Ndugai alihoji wanadhibitiwaje.

“Hivi kwa nini mnajiweka katika hali fulani ya kuona kwamba mnaonewa? Hivi unaonewa na nani kanuni ni za wote? Taratibu ni za wote hakuna mtu aliyedhibitiwa chochote,” alisema.

Tuesday, March 14, 2017

Ukata waliza madiwani

By Daniel Makaka, Mwananchi dmakaka@mwananchi.co.tz

Sengerema. Kutokana na kutolipwa posho za vikao vya kamati kwa mwaka mmoja, Madiwani wa Halmashauri ya Sengerema mkoani Mwanza, wamegoma kuendelea na vikao hivyo.

Wajumbe wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji pamoja na Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira zilikuwa zikutane juzi, lakini vikao havikuendelea baada ya madiwani kugoma hadi walipwe fedha zao zaidi ya Sh2 milioni.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema, Godwin Barongo alisikitishwa  na kitendo hicho kwa kile alichodai kuwa walishakubaliana kulipana baada ya vikao vya baraza, lakini wajumbe waliamua kugoma.

Diwani wa Igalula, Onesmo Mashili alisema wameamua kugoma kutokana na kutolipwa fedha zao kwa mwaka mmoja tangu waingie madarakani.

Mashili alisema wamekuwa wakipigwa danadana ya kulipwa fedha zao.

 

Tuesday, March 14, 2017

Magufuli awapa ‘makavu’ wabungeRais John Magufuli

Rais John Magufuli 

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dodoma. Rais John Magufuli amewapasulia jipu wabunge wa CCM kuwa anamuunga mkono Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hata kama wapo miongoni mwao wanaompinga.

Mbali ya kumkingia kifua Majaliwa, Mwenyekiti huyo wa CCM pia amewaonya wabunge wa chama hicho wanaotoa muda wao wa kuchangia bungeni kwa wapinzani, huku akieleza kukerwa na wabunge wanaofifisha vita dhidi ya dawa za kulevya na mmoja akimtuhumu kutoa siri za chama kwa upinzani.

Rais Magufuli aliyekutana jana na wabunge hao Ikulu ndogo ya Chamwino mjini hapa, pia aliwaambiwa kwamba yeye ndiye aliyeamua kusitisha mikutano ya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja katika televisheni.

Kikao hicho cha ndani kimefanyika siku moja baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa CCM mjini hapa na kupitisha mageuzi makubwa ya kikatiba na kanuni kwa chama hicho tawala.

 

 

Tuesday, January 3, 2017

Mtalii afariki dunia akipanda mlima

 

By Zainab Maeda, Mwananchi zmaeda@mwananchi.co.tz

Moshi. Raia wa Norway, Johan Signmundstad (54) amefariki dunia wakati akipanda Mlima Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa amesema raia huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria yenye namba 28890496  alipofika eneo la Simba Cane ndani ya hifadhi ya mlima huo  aliugua ghafla na kufariki dunia wakati akishushwa chini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hata hivyo, hakueleza ugonjwa uliosababisha kifo chake.

Mutafungwa alisema mwili wa mtalii huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu kabla ya taratibu nyingine kufanyika.

Tuesday, January 3, 2017

Madereva 33 mbaroni wakidaiwa kulewaKamanda Sirro

Kamanda Sirro 

By Pamela Chilongola, Mwananchi pchilongola@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Madereva 33 wamekamatwa kwa tuhuma za kuendesha magari huku wakiwa wamelewa wakati wa sikukuu ya Mwaka Mpya.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema walifanya operesheni dhidi ya madereva na kuwabaini hao wamelewa huku wakiendesha magari jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Sirro amesema katika operesheni hiyo Kinondoni walikamatwa madereva 15, Temeke 10 na Ilala wanane.

“Sasa hivi tukimkamata dereva akiwa amelewa hatumuandikii faini ya kulipa tumeona wengi wao wanaona rahisi na kuendelea kurudia makosa, hivyo tunawapelea mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.

Saturday, December 31, 2016

Misikiti isiwe chanzo cha mizozo- Dk Shein

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.com

Unguja. Waumini wametahadharishwa kuwa misikiti isiwe chanzo cha mivutano na migongano na badala yake iwe sehemu ya kuwaunganisha Waislamu.

Rais wa Zanzibar, Alhaji Dk Ali Mohamed Shein ametoa tahadhari hiyo baada ya kufungua Msikiti wa Muhammad uliopo Fujoni Mzambarauni, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk Shein amesema siyo vizuri msikiti kuwa chanzo cha mizozo na migongano kwani ni nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa ya ibada.

Amewataka waumini hao kuufanya msikiti huo kuwa sababu ya watu kushikamana na kuendeleza masuala ya dini na kutafuta uongozi madhubuti wa msikiti huo.

 

Sunday, January 1, 2017

Magufuli ashiriki ibada ya mwaka mpya Bukoba

 

By Phinias Bashaya, Mwananchi

Bukoba. Hatimaye Rais John Magufuli amewasili mjini Bukoba na kushiriki misa ya kufungua mwaka mpya 2017 katika Kanisa la Kuu Katoliki mjini Bukoba.

Katika misa hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo la Bukoba, Mhashamu Desderius Rwoma, Dk Magufuli amewataka viongozi wa dini wamvumilie kwa kuwa fedha zitaendekea kupotea hata kanisani.

Amesema zamani zilikuwepo fedha za hovyo hovyo na sasa anachotaka ni kila mtu aendelee kula anachostahili

Amesema uchumi wa nchi unaendelea kuimarika na Serikali imedhibiti mfumuko wa bei.

Akiwa Kagera, Rais Magufuli atapata fursa ya kuwasalimia wananchi waliopata maafa ya tetemeko la ardhi Septemba mwaka jana.

Sunday, January 1, 2017

‘Epukeni unafiki katika jamii’

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini wamewataka wananchi kuepuka roho ya unafiki inayosababisha chuki na uadui kwenye jamii.

Wito huo umetolewa jana kwenye mkesha wa Mwaka Mpya uliofanyika juzi kwa mara ya 19, ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi katika Uwanja vya Uhuru, Dar es Salaam akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Mbali na ibada hiyo ya Dar, mikoa mingine 16 chini ya uratibu wa Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste (TFC) nayo iliendesha misa kama hiyo ya Mwaka Mpya.

Kabla ya maombi hayo, Mchungaji wa Kanisa la City Christian Fellowship (CCF), Eden Geofrey aliyataja matatizo mengine kuwa ni tabia ya kusema uongo na umwagaji wa damu.

Alitolea mfano wa tukio la mkulima mkoani Morogoro aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni kwa sababu ya ugomvi wa ardhi.

 

-->