Trafiki aliyeuawa, mwenzake alikimbia

Muktasari:

Sajenti Nipishe anakuwa askari wa pili wa kikosi cha usalama barabarani kuuawa na watu wasiojulikana ndani ya miezi miwili, baada ya Ali Salum “Kinyogoli” kuuawa nyumbani kwake Mwandege wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani Mei 20.

Dar es Salaam. Watu waliomuua askari wa kikosi cha usalama barabarani, Sajenti Mensah Nipishe walifanikiwa kutekeleza azma hiyo baada askari mwenzake kukimbia eneo la tukio, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi.

Sajenti Nipishe anakuwa askari wa pili wa kikosi cha usalama barabarani kuuawa na watu wasiojulikana ndani ya miezi miwili, baada ya Ali Salum “Kinyogoli” kuuawa nyumbani kwake Mwandege wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani Mei 20.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema askari huyo wa kituo cha Oysterbay aliuawa juzi saa mbili usiku eneo la Sayansi Kijitonyama wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

“Alipigwa risasi kifuani na kusababisha mauti yake palepale. Chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana,” alisema Kamanda Fuime.