Mwanamke anayehangaika kutafuta haki baada ya kupata ulemavu wa mguu

Fatma Semdoe aliyekatwa mguu kutokana na kupata ajali ya gari baada ya gari hiyo kumgonga wakati akitoka bandani anakifanya Biashara zake. Picha na Burhan Yakub

Muktasari:

Hayo ni maneno yaliyochanganyika na swali na ombi yaliyotolewa na Fatma Semdoe (35), aliyekatwa mguu baada ya kugongwa na gari wakati akifanyabiashara ya mamalishe kwenye vibanda vya kutoa huduma ya chakula vilivyopo Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Handeni. Alipomaliza kulia na kufuta machozi ikiwa ni ishara ya kuonyesha hisia zake, alianza kueleza yaliyomsibu mpaka akawa katika hali hiyo.

“Sijui niseme maneno gani au nilie kilio gani ili walimwengu watambue namna ninavyohisi. Nimegongwa na kuwa mlemavu, mume wangu ameniacha lakini kama haitoshi walionigonga hawataki kunilipa haki yangu, nani atanisaidia?” Hayo ni maneno yaliyochanganyika na swali na ombi yaliyotolewa na Fatma Semdoe (35), aliyekatwa mguu baada ya kugongwa na gari wakati akifanyabiashara ya mamalishe kwenye vibanda vya kutoa huduma ya chakula vilivyopo Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Handeni. Alipomaliza kulia na kufuta machozi ikiwa ni ishara ya kuonyesha hisia zake, alianza kueleza yaliyomsibu mpaka akawa katika hali hiyo.

“Mimi ni mtoto wa mzee Semdoe wa hapa mjini Handeni, nilizaliwa mwaka 1981 na kupata elimu yangu ya msingi na sekondari hapahapa Handeni, kwa hiyo mimi ni mtoto wa mji huu,” anasema Fatma.

Chanzo cha ulemavu

Ilikuwa saa tisa alasiri ya Februari 2010 nilikuwa natoka kwenye banda langu la mamalishe nakwenda kumpelekea chakula mteja. Nikiwa nipo mlangoni gari (iliyosajiliwa kwa kufanya biashara - teksi) ikanigonga na kunikandamiza ukutani.

“Iliponikandamiza nilijikuta nikipata maumivu makali ambayo siwezi kuyaelezea uchungu wake, nilipiga kelele wakaja watu kuninasua, wakanipeleka Hospitali ya Wilaya ya Handeni,” anasema Fatma.

Fatma ambaye ni mama wa watoto wawili, Abdi Ramadhan (13) na Hadija Ramadhan (8) anasema kutokana na kujeruhiwa, hakukaa muda mrefu katika Hospitali ya Handeni kwani saa kumi siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga, Bombo, ambako alilazwa kwa siku tisa baadaye akahamishiwa KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Aprili 25, 2010 madaktari wangu wa KCMC walikuja kunielezea hawana njia nyingine zaidi ya kunikata mguu wa kushoto uliokuwa umekandamizwa, kama nataka kupona na kuendelea na shughuli zangu,” anasema Fatma na kuongeza:

“Maelezo hayo yalinichanganya, niliwaza sana nikaona sasa nimekwisha, nikajiuliza nitaishije na mguu mmoja. Lakini kwa sababu mguu huu ulikuwa na maumivu makali, nikakubali kwa shingo upande.

“Aprili 27, sitaisahau maishani mwangu, kwani ndiyo siku ambayo madaktari waliopanga kunikata mguu walinifanyia upasuaji, nilipoamka nikajikuta mguu wangu wa kushoto umekatwa juu ya goti.

“Ajali hiyo pia ilinipa mshtuko kichwani ambao hadi sasa nikikaa mara nyingine najikuta nikipoteza kumbukumbu, hata kama nilikuwa nazungumza nakuwa siwezi kukumbuka tena, inabidi niende kitandani kulala kwa muda fulani hadi hali irejee kuwa sawa.”

Mwanamke huyo anasema alikaa KCMC kwa zaidi miezi sita akiuguza majeraha na kusubiri utulivu wa ubongo, kutokana na ajali kutingisha kichwa chake.

Kutokana na maelekezo ya kitaalamu ya daktari wake, alishauriwa kukaa muda mrefu kabla ya kwenda mahakamani kufungua kesi kwa sababu kichwa hakikuwa katika hali nzuri.

“Baada ya kukaa nyumbani kwa kipindi cha miaka mitatu, nikamfuata daktari kumuomba ruhusa ya kwenda mahakamani, akaniruhusu.

“Hatua hii ndiyo ikawa chanzo cha mahangaiko, kwani huko nimeambiwa sina changu chochote,” analalamika Fatma.

Mama huyu anasema alipopata ruhusa akaamua kwenda polisi akakabidhiwa askari wa kikosi cha usalama barabarani aliyepima siku ya ajali, ambaye alimwita mmiliki wa gari lililomgonga, lakini cha kushangaza alikana kwamba yeye si mmliki.

“Nilipopelekwa Bombo alitoa Sh250,000 za matibabu, alitoaje fedha zile wakati gari si lake?” anahoji.

Fatma anasema alipotaka kufungua kesi ya madai aliambiwa ameshalipwa fidia ilhali siyo ukweli na kwamba hata hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Handeni imemnyima haki kwa maana kwamba alishindwa.

Hata alipokata rufaa Mahakama Kuu, anasema alifahamishwa kwamba kesi ilikwisha tangu Juni 24, 2015 na alipofuatilia alielezwa kuwa iliwekwa pini kutokana na wakili wake kutohudhuria tarehe za kesi.

“Nimefika mahali pa kukata tamaa, hivi kumbe walimwengu ndivyo walivyo, unapewa ulemavu na aliyekupa ulemavu anakuwa salama, uliyelemaa unakuwa mkosefu?” anahoji Fatma na kuongeza:

“Kwa nini nadhulumiwa hata haki yangu ya kulipwa bima.”

Fatma ambaye licha ya kuwa hakutaka kueleza kwa undani juu ya maisha yake ya ndoa, anasema baada ya kugongwa mumewe alimtelekeza, hakwenda hospitalini kumjulia hali, lakini aliamua kuoa mke mwingine huku akiwa amelazwa KCMC.

Anaomba wanaharakati wa haki za wanawake nchini wamsaidie mahakamani ili apewe haki yake kwani anaamini kama angekuwa na uwezo wa fedha asingedhulumiwa.

Pia, anasema iwapo watakaoguswa watajitokeza wamsaidie kwa kumnunulia mguu wa bandia ili aweze kuendesha shughuli alizokuwa ameanza za ujasiriamali katika kibanda kidogo cha kuuza vocha na kukaanga mihogo, alichofunguliwa na mfanyabiashara wa mjini Handeni.