Waganga wa jadi wasaka ofisi kwa RC

Muktasari:

Katibu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (Wawata) Mkoa wa Dodoma, Lukas Mlipu alisema walianza maandalizi ya kuipokea Serikali mkoani hapa kwa kupeleka andiko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuomba jengo la ofisi.

Dodoma. Waganga wa jadi wamejipanga kupokea makao makuu ya Serikali kuhamia mjini hapa, kwa kuomba jengo la ofisi serikalini kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wao.

Katibu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (Wawata) Mkoa wa Dodoma, Lukas Mlipu alisema walianza maandalizi ya kuipokea Serikali mkoani hapa kwa kupeleka andiko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuomba jengo la ofisi.

Mlipu alisema Dodoma itakuwa na watu wengi ambao kwa vyovyote watahitaji huduma zao kama ilivyo nyingine zinazotolewa na Serikali na mashirika mengine.

“Makao makuu tunayangoja kwa hamu, kwa sasa tuko katika mchakato wa kuyapokea ikiwamo kuwakaribisha na wenzetu wengine maana najua watakuja, lakini sisi tuliopo huku lazima tuwe mfano kuboresha huduma zetu,” alisema Mlipu.

Alitoa onyo kwa waganga vihiyo ambao wamekuwa wakitumia kivuli cha uganga kuwatapeli watu kuwa watachukuliwa hatua. Mlipu alisema mganga mzuri ni yule anayetambua hospitali kuwa zina uwezo wa kutoa vipimo sahihi na tiba na si kupiga ramli chonganishi.