January: Nilikuta ofisi inaitwa kijiwe

Muktasari:

Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, January amesema alifanya hivyo ili kutengeneza ofisi hiyo ikae vizuri kwa ajili ya kutekeleza majukumu iliyopangiwa.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema alipoingia katika ofisi hiyo alikuta ikiitwa kijiwe na hivyo kazi aliyoifanya ni kubadili fikra za watu.

Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, January amesema alifanya hivyo ili kutengeneza ofisi hiyo ikae vizuri kwa ajili ya kutekeleza majukumu iliyopangiwa.

“Niliwazuia watumishi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi hapo watakapokamilisha mambo 13 ikiwamo kuandaa cabinet papers (nyaraka za mawaziri) 10,” alisema.

January ametoa kauli hiyo baada ya wabunge wa kamati hiyo kumpongeza kwa kuandaa mipango kazi bila kulalamika kuwa hakuna fedha, tofauti na mawaziri wenzake ambao wamekuwa wakilalamikia hata nauli wanapoitwa na kamati hiyo kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali.