Lissu na wenzake washindwa kusomewa mashtaka mapya

Muktasari:

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo mapya.

Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeshindwa kuwasomea washtakiwa hao mashtaka mapya baada ya wakili anayewatetea, Peter Kibatala kudai kuwa yaliyofutwa yamerudishwa kwa ‘staili’ tofauti.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo mapya.

Wakili wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba kuwasomea hati mpya ya mashtaka washtakiwa hao na Mahakama iliipokea na kuruhusu isomwe, lakini Wakili Kibatala alipinga kwa madai kuwa hayatofautiani na yale yaliyofutwa Juni 28, 2016.

Kibatala amedai katika hati mpya shtaka la kwanza na la tano ni sawa na yale yaliyokuwamo kwenye hati iliyofutwa mahakamani hapo baada ya kupingwa na kuonekana hayakustahili kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi mwezi ujao atakapotoa uamuzi wa hoja hizo.