Kupatwa kwa Jua, Macho yote duniani yapo Mbarali leo

Muktasari:

Mkuu wa wilaya Mbarali Rueben amewasili kwenye tukio na ulinzi usalama waimarishwa

Kupatwa kwa Jua tena kunaelezwa na wataalam wa anga kuwa kutatokea 2032

12:52 RC Makalla: Endeleeni kufurahia kupatwa kwa Jua ulinzi upo. Wafanyabiasha endeleeni na shughuli yenu

11:58amKipete chakamilika na kutimiza Rujewa

11:33am Zaidi ya nusu ya jua imekwishafunikwa, kaubaridi kameanza.

11:03 Takribani theluthi moja ya jua imefunikwa  na mwezi

9:48AM Watu waambiwa wajikusanye katika makundi yenye watu 30 ili wapewe vifaa vya kutazama kupatwa kwa jua

9:30am Mkuu wa wilaya Mbarali Rueben anawasili kwenye tukio na ulinzi usalama waimarishwa

9:21am  Umati wa watu wamiminika Rujewa, Mbarali kushuhudia kupatwa kwa jua kipete

Jua laanza kupatwa Rujewa

Jua limeanza kufunikwa taratibu likiashiria kuanza kupatwa . Hadi sasa takriban theruthi moja imeshafunikwa na watu wengi wanaendelea kutizama kwa kutumia miwani waliopatiwa huku wengine wakitumia vifaa vingine vyenye uwezo wa kuwawezesha kuona tukio hilo.

Miwani iliyoletwa imetolewa kwa waliokuwa wamejipanga katika makundi ya watu 30 lakini imeshindwa kutosheleza mahitaji. Viongozi mbalimbali wa mikoa ya Songwe na Mbeya wanaendelea kuwasili eneo hili sambamba na makundi ya shule mbalimbali.

Mbali na kushuhudia tukio hilo, wananchi wengi wanalalamika kuwa kuna vyombo vya  habari vya kimataifa lakini Serikali imeshindwa kuweka hata bendera ya taifa kutofautisha eneo la Rujewa na maeneo mengine ulimwenguni wanakoshuhudia kupatwa kwa jua.

Viongozi wa serikali,  wanahabari wa ndani na nje ya nchi na wananchi wameshawasili katika eneo linalotumika kushuhudia kupatwa kwa jua.

Eneo hili lililopo Rujewa, Mbarali ambalo hutumika zaidi katika kuchimba mawe na kupasua kokoto leo limefurika watu ambao wapo hapo si kwa ajili ya kununua bidhaa hiyo ya ujenzi bali kusubiri kushuhudia tukio hilo la aina yake duniani.

Walimu wakiongozana na wanafunzi wa shule kutoka Mkoa wa Mbeya na jirani wamewasili hapa kama sehemu ya kuwafundisha wanafunzi kivitendo.

Askari wanarandaranda kila kona kuhakikisha usalama unaimarishwa.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala aliyewasili pia katika eneo hili, amesema tukio hilo limefungua fursa kwa kila mtu Mbeya hasa Mbarali.

Amevishukuru vyombo vya habari kwa kuutangaza mkoa  na amewaambia wananchi wajikusanye katika makundi ya watu 30 ili wapewe vifaa vya kutazama kupatwa kwa Jua Tanzania.

Makalla amewataka wananchi kuwa makini kuangalia tukio hilo akisisitiza "Huu siyo mwisho wa dunia."

Waendesha bodaboda na bajaji wanaendelea kuwaleta watu hapa Rujewa kushuhudia kupatwa kwa jua.