Tetemeko lachelewesha mkutano wa Rais na viongozi wa dini kuhusu Ukuta

Picha na Ikulu

Muktasari:

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7 katika kipimo cha ritcher, lilitokea alasiri ya Jumamosi na kuua watu 17 na kujeruhi wengine zaidi ya 250 katika Mkoa wa Kagera.

Dar es Salaam. Athari za tetemeko la ardhi lilitokea Jumamosi iliyopita katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa, imeelezwa kuwa ni miongoni mwa sababu zitakazochelewesha mazungumzo kati ya viongozi wa dini na Rais John Magufuli kuhusu maandamano ya Chadema yaliyopewa jina la Ukuta.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7 katika kipimo cha ritcher, lilitokea alasiri ya Jumamosi na kuua watu 17 na kujeruhi wengine zaidi ya 250 katika Mkoa wa Kagera.

Katibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Leonard Mtaita alisema jana kuwa mpango wa viongozi wa dini kukutana na Rais Magufuli upo kama walivyokubaliana na viongozi wa Chadema, lakini umechelewa kutokana tetemeko hilo.

Hivi karibuni Rais Magufuli alifuta ziara yake ya Zambia ambako alikuwa ahudhurie sherehe za kuapishwa kwa Rais Edgar Lungu ili kushughulikia tatizo la tetemeko la ardhi.

Agosti 30, mwaka huu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kuahirisha mikutano na maandamano iliyoandaliwa na chama hicho kupinga kile ilichoeleza kuwa ni kuminywa kwa demokrasia nchini iliyokuwa imepangwa kuanza Septemba Mosi, baada ya viongozi wa dini kumtaka asitishe kwa muda hadi watakapozungumza na Rais Magufuli.

Hata hivyo, Mbowe alisema endapo jitihada za viongozi hao hazitazaa matunda kwa siku 30, mikutano na maandamano hayo ya amani vitaanza Oktoba Mosi.

“Mpango uko palepale, lakini hili tetemeko la Kagera limetufanya tuwe ‘busy’ na baadhi ya mambo yamesimama... Hata hivyo, kuna watu tumewaagiza kufuatilia mpango huu wa kukutana na Rais Magufuli kwa ajili ya mazungumzo. Naamini siku tulizopanga zitatutosha kufanya mazungumzo,” alisema.

Mchungaji Mtaita aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu na kuupuza maneno yanayosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba Rais Magufuli amekataa kukutana na viongozi kwa kuwa kila kitu kinakwenda kwa kufuata taratibu.

Katibu wa Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila aliungana na Mchungaji Mtaita kuwakata Watanzania kuwa na subira wakati wakisubiri kuonana na Rais Magufuli: “Tukiwa tayari tutawaeleza lini tunakwenda kuonana na Rais Magufuli kwa sababu nyinyi (waandishi) ni wadau muhimu,” alisema Sheikh Lolila.

Alisema Rais ni mtu mkubwa hivyo viongozi hao hawawezi kukurupuka kwenda kuonana naye na kwamba ni lazima wafuate itifaki zilizowekwa na mamlaka husika ili kuonana na kiongozi huyo wa nchi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alisema amepata taarifa kwamba viongozi hao wameandika barua na kwamba watajibiwa kwa utaratibu uliopo.