Mrembo wa kimasai anayewania taji la Miss Tanzania

Miss Kinondoni 2016, Diana Edward ni mmoja wa washiriki wa Miss Tanzania

Muktasari:

Mratibu wa Mashindano hayo, Hashimu Lundenga akizungumza jana alisema warembo waliopo kambini wanaandaliwa kuchuana kimataifa hivyo yeyote atakayeshinda atakuwa mwakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo ya Marekani.

Mrembo atakayenyakua taji la Miss Tanzania katika fainali zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, atakwenda Marekani kushiriki mashindano ya kutafuta mrembo wa dunia.

Mratibu wa Mashindano hayo, Hashimu Lundenga akizungumza jana alisema warembo waliopo kambini wanaandaliwa kuchuana kimataifa hivyo yeyote atakayeshinda atakuwa mwakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo ya Marekani.

“Fainali zitafanyika Rock City Mall jijini Mwanza na wasichana 30 watachuana kumpata mmoja atakayetuwakilisha baadaye mwaka huu nchini Marekani,” alisema.

Miongoni mwa warembo wanaowania taji hilo ni Diana Edward ambaye aliibuka mshindi katika ngazi za vitongoji na kunyakua taji la Miss Kinondoni.

Mrembo huyo anataja siri ya mafanikio yake kuwa ni hamu ya kutamani kusaidia jamii za pembezoni ikiwamo ya Wamasai.

“Sikuwa na wazo kama nitakuja kushiriki mashindano ya urembo, lakini wakati natafakari na kupitia shughuli wanazotakiwa kufanya washindi, nikagundua nimepata nafasi ya kutimiza ndoto zangu.

“Hasa baada ya kuanza kufuatilia shughuli anazofanya Hoyce Temu ambaye ndiyo role model wangu, niliona kama mwanga mbele wa kutimiza kile nilichokuwa nakiwaza kwa muda mrefu, kusaidia wasiokuwa na uwezo, ” anasema.

Pamoja na kujiridhisha sababu za kushiriki katika mashindano hayo, alipata kikwazo kutoka kwa wazazi wake kumkubalia.

Anafafanua kuwa aliwaaminisha kuwa hataingia katika skendo na hatalewa ustaa badala yake atautumia kuisaidia jamii. “Walinielewa kwa shingo upande hadi niliposhiriki kwa mara ya kwanza ndiyo wakaanza kunipa moyo na kuniunga mkono,” anasema.