Jalada kesi ya Lwakatare lahitajika kortini

Muktasari:

Agizo hilo linalotakiwa kuwa limetekelezwa ifikapo Novemba 17, lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita kudai kwamba jalada la kesi hiyo lipo Mahakama ya Rufani na wanasubiri matokeo ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hivyo kuiomba Mahakama itoe tarehe ya kutajwa  kwa kesi hiyo.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph umetakiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatilia na kupeleka jalada la shauri hilo linalodaiwa kuwapo Mahakama Kuu.

Agizo hilo linalotakiwa kuwa limetekelezwa ifikapo Novemba 17, lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita kudai kwamba jalada la kesi hiyo lipo Mahakama ya Rufani na wanasubiri matokeo ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hivyo kuiomba Mahakama itoe tarehe ya kutajwa  kwa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo, Lwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini na mwenzake, Ludovick wanadaiwa kuwa  Desemba 28, 2013  katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni (sasa Ubungo), kwa pamoja walikula njama za kumdhuru kwa sumu aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.